ILIPOISHIA:
Japokuwa mwanzo nilikuwa mgumu lakini nilijikuta nakubali ofa za wanaume, lakini nilichagua wanaume wenye pesa kutokana na umbile na uzuri niliokuwa nao, hakuna mwanaume aliyekataa dau nililomwambia.SASA ENDELEA…
Maisha yangu hayakutetereka, kila mwanaume niliyekutana naye alitaka kunioa lakini nilikataa kwa kuhofia kuingizwa kizuizini. Nilijua ndoa ni utumwa na kuwaonea huruma wote walio ndani ya ndoa. Niliamini hawayafurahii maisha kwa kukosa uhuru.
Nilijiuliza wasichana wazuri kama mimi wanakimbilia kuolewa sijui uzeeni kwao watahadithia nini. Nilikuwa sikai na mwanaume mmoja zaidi ya wiki moja.
Niliyaanza maisha ya kujiuza kimwili kwa kwenda kwenye klabu za starehe usiku. Kutokana na umbile langu wanaume walinikimbilia kama mpira wa kona. Wapo niliokwenda nao muda mfupi na kunilipa malipo yangu na wapo niliokwenda kulala nao mpaka asubuhi.
Mradi ule kidogo ulinisaidia hasa baada ya kuanza wizi wa kuwapekua wanaume tukiwa tumelala, usiku wakilala niliamka na kuwapekua kwenye nguo zao na kutoroka wakiwa wamelala. Kuna siku nililala na mzungu na kufanikiwa kumuibia pesa nyingi na kutimka usiku. Asingeweza kunitafuta kwa sababu hakuwa na ushahidi wa kunifunga.
Baada ya kupata pesa niliamua kuachana na kazi ya kujidhalilisha na kuanzisha biashara ya saluni na duka la vipodozi. Amini usiamini kwa muda mfupi hali yangu ya maisha ilibadilika.
Wakati huo nilikuwa nimekuja na mtindo mwingine ambao nilijua mimi ndiye msemaji mkuu kwa kuchukua mwanaume kijana na kumfuga kwa kumpa kila kitu ili tu aniridhishe kimapenzi.
Kijana mmoja kwa kweli nilitokea kumpenda tangu siku ya kwanza nilipomuona. Nilitupa chambo na yeye akakimeza chote na kumfanya mpenzi wangu.
Nilimpa kila kitu alichotaka mpaka gari la kutembelea, nilijikuta nayainjoi maisha kwa kupata kijana shababi ambaye alikuwa akinikata kiu ya mapenzi kisawasawa. Wakati huo shughuli zangu zilikuwa zikienda vizuri.
Kijana huyo mwanzo alikuwa akinisikiliza muda wowote niliokuwa nikimtaka nilimpata. Lakini ghafla yakatokea mabadiliko kila nikiwa na shida naye simpati kwa wakati muafaka.
Taarifa zilinifikia kuwa mmoja wa wafanyakazi wangu wa saluni ndiye alikuwa akitumbua naye pesa ninazompa. Roho iliniuma kwa kukumbuka nilipomtoa kwenye mtaro wa kuoshea magari mpaka kupendeza na kutamaniwa na wanawake ambao mwanzo wangemtema mate kwa kikwapa alichokuwa akinuka.
Nakumbuka siku ya kwanza kumuona kijana huyo alikuwa pembeni akiwa mwenye njaa na kwa bahati mbaya hakupata kazi kwa siku ile kwa kuwahiwa na wenzake magari ya kuosha.
Nikiwa nje nasubiri gari langu lisafishwe nilimuona kwenye mavazi machakavu. Japokuwa mavazi yake yalikuwa machakavu lakini umbile lake lilikuwa limekakamaa kiume haswa. Nilijikuta nikimuangalia kwa matamanio kwa kuwaza kuwa kama nitammiliki yule kijana nitafaidi. Nilipomwita alinisogelea kwa wasiwasi.
“Vipi sister kuna ishu maana mambo mabaya,” alisema huku akipiga miayo.
“Wewe tu..unaitwa nani?”
“Bantu.”
“Ooh! Bantu jina zuri unakaa wapi?”
“Temeke Mikoroshoni.”
“Sasa Bantu tukitoka hapa tuongozane kuna kazi nataka kukupa, ukiifanya kwa umahiri nitakupa zawadi nzuri,” nilimchombeza bila kujua nilimtaka kimapenzi.
“Yaani sister nilivyo na usongo utafurahi mwenyewe,” maskini Bantu alikubali bila kujua kazi ninayotaka kumpa.
“Hiyo ndiyo shida yangu.”
Baada ya kusafishiwa gari niliongozana na Bantu kuelekea nyumbani kwangu. Moyoni niliona kwa mtindo ule siwezi kuwekewa mipaka hata kama nitakuwa na mwanaume wa nje hawezi kunizuia.
Tukiwa njiani nilimuuliza maswali kadhaa juu ya maisha yake
“Bantu ina maana hii ndiyo kazi yako ya kila siku?”
Itaendelea Risasi Jumamosi