×

Unending Love – 67

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake kwa mara nyingine kwa madai kwamba anajihisi anakaribia kufa hivyo ni lazima aonane na Jafet ili amueleze kilichokuwa ndani ya moyo wake. Hali hiyo inasababisha baba yake Anna afunge safari mpaka jijini Dar es Salaam kumfuata Jafet ambaye naye anampeleka mpaka kwa wazazi wake.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya salamu, wote waliingia mpaka sebuleni ambapo Jafet alivunja ukimya na kuwaeleza wazazi wake kilichowafanya wafunge safari ya ghafla asubuhi hiyo.

“Hivi wewe Jafet una akili kweli wewe? Huyu mzee na familia yako si ndiyo waliosababisha ukanusurika kupoteza maisha kwa maradhi ya figo? Au umesahau? Sikia mzee mwenzangu, kwa mlichomfanyia mwanangu, nakuomba uondoke, mlango ule pale, ondoka haraka kabla hatujakorofishana,” alisema baba yake Jafet huku akisimama kwenye kiti alichokuwa amekaa, watu wote wakabaki kimya kabisa kwa sababu alichokisema baba yake Jafet, japokuwa alikuwa na sifa ya ulevi, kilikuwa na maana kubwa.

“Lakini mume wangu, hebu ngoja kwanza, tutumie busara katika hili, nakuomba utulize jazba zako,” alisema mama yake Jafet na kuingilia kati mazungumzo hayo lakini baba yake Jafet hakutaka kusikia la muadhini wala la mchota maji.

“Baba, naomba umsikilize baba Anna, amefunga safari kutoka India mpaka hapa kwa ajili ya suala hilo, nipo chini ya miguu yako, naomba umsikilize,” alisema Jafet. Kauli hiyo ya mhusika mwenyewe, ilimfanya baba Jafet ashushe pumzi ndefu na kutulia, akawa anatazamana na baba Anna kama majogoo yanayotaka kupigana.

“Yaliyopita yalishapita mume wangu, hebu tushirikiane kuokoa maisha ya Anna, unajua hata kama walimuumiza mtoto wetu, wamekuwa kama ndugu kwetu, nakuomba mume wangu, hebu zungumzeni wawili kwanza mfikie muafaka,” alisema mama yake Jafet huku akimpa ishara mwanaye ya kutoka nje, wakawaacha baba yake Anna na baba yake Jafet ambao waliendelea kujadiliana na hatimaye muafaka ukafikiwa.

Jafet na mama yake wakaitwa na kuelezwa muafaka uliofikiwa, Jafet akafurahi sana kusikia wazazi wake wakimruhusu japokuwa walimpa masharti kwamba hatakiwi kutolewa kiungo kingine chochote kwa sababu yeye mwenyewe afya yake haikuwa imetengemaa.

Baba yake Anna aliwashukuru sana wazazi wa Jafet na kuahidi kutowaangusha. Hawakuwa na muda wa kupoteza, baada ya kupata baraka za wazazi wa Jafet, waliaga na kuondoka, wakapanda baiskeli zilizowafikisha mpaka kwenye barabara kubwa yanakopita magari. Wakapanda kwenye basi na safari ya kurejea jijini Mwanza ikapamba moto.

Hatimaye waliwasili jijini Mwanza ambapo walipitia nyumbani kwa akina Anna, Capri Point walikopumzika kidogo kisha wakatoka na kuelekea uwanja wa ndege. Wakapanda ndege iliyowapeleka mpaka jijini Dar es Salaam walikowasili saa nne za usiku.
“Kwa hiyo si tutaondoka kesho? Naomba nikawaage marafiki zangu chuoni,” alisema Jafet.

“Siyo kesho Jafet, tunaondoka na ndege ya saa nane usiku, hapa tuna saa chache tu,” alisema baba yake Anna, hali iliyomfanya Jafet aishiwe nguvu. Hakuna jambo ambalo alikuwa hataki litokee kama kumkasirisha Suleikha. Mpaka muda huo alikuwa ameshamkosea kwa kusafiri kuelekea Mwanza bila kumpa taarifa na alikuwa na uhakika kwamba msichana huyo atakuwa anamtafuta kila sehemu.

Ilibidi amueleze baba yake Anna ukweli ambapo walikubaliana kwamba ili wasije wakapishana, waongozane pamoja mpaka chuoni hapo, Jafet akaagane na rafiki zake kisha waondoke pamoja kuelekea uwanja wa ndege.

“Jafet! Oooh my God! Are you okay?”
(Jafet! Ooh Mungu wangu! Uko sawa?)
“Im okay Suleikha, im sorry i left without your notice.”
(Niko sawa Suleikha, samahani niliondoka bila wewe kujua.)
“Where were you bae? I was really worried.”

(Ulikuwa wapi mpenzi? Nilipatwa na hofu kubwa)
“I had an emergence, im really sorry. Can we talk please?” (Nilipata dharura, niwie radhi sana. Tunaweza kuzungumza tafadhali?) alisema Jafet huku akimtoa Suleikha mwilini mwake kwani alikuwa amemganda kama ruba.

Wakasogea pembeni huku watu wakiendelea kuwakodolea macho, Jafet akamshika Suleikha mikono na kuanza kumueleza kwamba anatakiwa kusafiri usiku huohuo kuelekea India, kauli iliyomshangaza sana Suleikha.

“No! Haiwezekani Jafet! Mbona ghafla kiasi hicho?”
“Ni dharura mpenzi wangu, hali ya Anna naambiwa ni mbaya sana, anaweza kukata roho muda wowote na amesisitiza ni lazima nifuatwe nikaonane naye, nakuomba uniwie radhi kwa hilo,” alisema Jafet, kauli iliyosababisha Suleikha aanze kuangua kilio kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Hakuwa tayari Jafet aondoke na kwenda mbali naye, ikabidi kijana huyo awe na kazi ya ziada ya kumbembeleza mpaka alipotulia.
“Unaniahidi nini Jafet.”
“Nakuahidi kwamba nitakupenda daima na namuomba Mungu anisaidie niende salama kisha nirudi salama.”

“Isije kuwa mmepanga muende kurudiana na huyo Anna wako huko India, nakuomba usifanye hivyo mpenzi wangu, wewe ndiyo moyo wangu,” alisema Suleikha na kumkumbatia tena Jafet kwa nguvu huku akiendelea kulia kwa hisia kali.

“Muda umeisha Jafet,” alisema baba yake Anna, kauli hiyo ndiyo ikamzindua kutoka kwenye hali aliyokuwa nayo, akajitoa kwenye mikono ya Suleikha na kumbusu kwenye midomo yake kisha akamalizia kwenye paji lake la uso. Akaondoka na kumuacha Suleikha akiendelea kulia kwa uchungu. Waliingia kwenye teksi na safari ya kuelekea uwanja wa ndege ikaanza.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

4 Comments

Leave a Comment