KEVIN akiwa na tumaini kwamba wazazi wake watakubaliana na uamuzi ambao ameufikia wa kutoa uboho wake ili Catarina awekewe ghafla tumaini hilo linapotea, wazazi wake hawako tayari kabisa kukubaliana na kile ambacho mtoto wao anataka, wanahisi kufanya hivyo ni kumpoteza mtoto wao pekee.
Kwa muda Kevin huku akilia anajaribu kuwaeleza wazazi wake juu ya kile ambacho daktari amemweleza na kwamba hakuna madhara yoyote atakayoyapata baada ya yeye kutoa uboho wake na kumpa mwanamke aliyempenda jambo ambalo wazazi wake hawataki kabisa kulisikia.
Wakiwa katika majadiliano hayo nyumbani kwao huku Kevin akilia akiendelea kusisitiza apewe ruhusa ili aweze kumsaidia Catarina, ghafla mlango unagongwa na mama yake Kevin anakwenda kufungua macho yake yanakutana na Dk. Ngamila daktari wa Hospitali ya Saratani Ocean Road na baba yake Catarina mzee David.
Anawakaribisha ndani na baada tu ya salamu, Dk. Ngamila anaanza kuelezea dhumuni la uwepo wao hapo akianza kwa kuwaeleza kama watakuwa tayari wakubaliane na hitaji la mtoto wao atoe uboho wake na kumpa Catarina kwani hakukuwa na madhara yoyote yale ambayo yangetokea, baada ya kuelezea kwa kina wazazi wote wawili wa Kevin wanakubaliana na daktari wakieleza wazi kwamba hofu yote waliyokuwa nayo ilikuwa imekwisha.
Kevin anatabasamu huku akisimama na kwenda kuwakumbatia wazazi wake kisha mzee David na Dk. Ngamila, chumba kikajawa na furaha tena, wazazi pia wakakumbatiana na mwisho wakakubaliana kuondoka tena kurejea hospitalini ili taratibu za Kevin kutoa uboho zikaanze mara moja.
Tayari Kevin ameshatolewa uboho, kinachosubiriwa ni madaktari kutoka India wakisaidiana na wenyeji wao wa Tanzania, wafanye kazi yao ya kupandikiza uboho kwa Catarina. Tayari jopo la wataalamu wote lipo ndani ya chumba cha upasuaji. Je, Catarina atafanikiwa kupona?
KILICHOFANYIKA siku iliyofuata ni madaktari kukutana na kujadili namna ambavyo matibabu ya Catarina yangefanyika, uboho uliotolewa na Kevin ulikuwa umehifadhiwa kwenye jokofu lenye baridi kali ili usipoteze uhai kabla haujaingiza mifupani mwa mgonjwa. Wote wakakubaliana kwanza ilikuwa ni lazima kumfanyia Catarina mionzi ili kuua kabisa chembechembe za saratani zilizokuwa zimebaki mwilini mwake na pia kukausha uboho uliokuwemo ndani ya mifupa ili kutoa nafasi kwa chembechembe za uboho mwingine kuingia.
“We need to do TBI!” (Tunahitaji kufanya TBI)
“What do you mean by TBI Dr. Hitesh?”(Unamaanisha nini unaposema TBI Dk. Hitesh?)
“I mean Total Body Irradiation!”(Ninamaanisha kupiga miozi mwili mzima!)
“That is important!”(Hiyo ni muhimu!)
“Before we do the Transplant!”(Kabla hatujapandikiza uboho mwingine!)
“Also we need to prepare a lot of blood pints as she will need to be transfused with blood after the Transplant before the Bone Marrow gets on duty!”(Pia tunahitaji damu nyingi maana atahitaji kupewa damu kabla uboho tunaoweka haujaanza kufanya kazi!)
“Our blood bank is full!”(Benki yetu ya damu ina damu nyingi!)
“As she will be having no immunity, we need a special private room to avoid infections!”(Vilevile kwa sababu hatakuwa na askari wa kutosha mwilini, tunahitaji chumba maalum kuepusha yeye kupatwa na maambukizi!)
Ulikuwa ni mjadala mrefu lakini mwisho madaktari wakakubaliana Catarina aanze mionzi siku hiyohiyo na kuendelea nayo kwa wiki nzima, hali yake ikadhoofika sana, madaktari kutoka India wakawa wanawaondolea wazazi wasiwasi kwa kuwaambia hivyo ndivyo matibabu hufanyika kabla mgonjwa hajapona maana ni lazima chembechembe zote za saratani ziondolewe zote ndipo awekewe uboho mpya.
Mwisho wa wiki ya kwanza, Catarina alichukuliwa na kupelekwa chumba cha upasuaji ambako madaktari bingwa kutoka India walishirikiana kuingiza sindano ndani ya mshipa mkubwa wa damu kifuani wakitumia kifaa kiitwacho Central line Catheter na kuanza kuuachia uboho uingie kwenye damu na damu hiyo iliusafirisha taratibu kwenda kwenye mifupa.
“Did you do human Leucocytes associated antigen test? To see compatibility?”( Je, mlipima kipimo cha kuangalia kama chembechembe nyeupe za damu za aliyetoa uboho na anayepokea zinafanana?)
“Yes we did!”(Ndiyo tulifanya!)
“And the result were?”(Na majibu yalikuwa?)
“Compatible!”(Wanafanana!)
“Very good!”(Safi kabisa!) Dk. Mukesh Duvani, bingwa wa masuala ya kinga ya mwili aliongea wakati wote wakishuhudia uboho ukidondoka vizuri kuingia mwilini mwa Catarina ambaye alikuwa katikati ya dawa ya usingizi akiwa hatambui chochote kilichokuwa kikiendelea.
Ghafla wote wakashtuka na kusimama wima, Catarina alitoa macho na kuanza kukakamaa, madaktari kutoka India walipatwa na mshtuko mkubwa mioyoni mwao wakakiri hawakuwahi kukutana na hali kama hiyo kwa mgonjwa katikati ya shughuli ya kupandikiza uboho.
Shinikizo la damu la Catarina lilikuwa likishuka kwa kasi huku mapigo ya moyo yakienda mbio! Kuhema kwake ghafla kukabadilika na kuwa kwa harakaharaka kuliko kawaida, madaktari wakaanza kukagua kuona kama kila kitu kilikuwa sawa.
“What is wrong?”( Kitu gani kibaya kimetokea?) Dk. Ngamila aliuliza.
“I don’t know!’(Sijui!) daktari mwingine akamjibu.
***
Kevin, wazazi wake na wazazi wa Catarina walikuwa nje ya chumba cha upasuaji, akili yao yote ikiwa ndani ya chumba hicho. Mioyoni kila mmoja alikuwa akimwomba Mungu wake atende muujiza ili Catarina atoke ndani ya chumba hicho akiwa salama, hilo ndilo lilikuwa tamanio la kila mmoja wao.
Hawakuelewa kabisa taabu iliyokuwa ikiendelea ingawa walishangaa ni kwa nini shughuli ambayo walielezwa ingechukua muda wa saa tatu, sasa ilikuwa inaelekea saa ya saba bila mgonjwa wao kutolewa! Wote walikuwa na maswali yasiyo na majibu vichwani lakini hakuna aliyethubutu kumshirikisha mwingine alichokuwa akikiwaza.
“Mbona amechelewa sana kutoka?” baba yake Catarina hatimaye aliwauliza wenzake.
“Hata mimi sifahamu, ingawa si kawaida!”
“Au kuna tatizo limetokea lakini wameshindwa kutoka nje kutueleza?” Baba yake aliongeza swali jingine.
“Sidhani!” baba yake Kevin akajibu.
“Imewahi kutokea mahali fulani, madaktari wakapata tatizo chumba cha upasuaji kwa kuogopa watawaeleza nini ndugu wa mgonjwa waliokuwa nje ya chumba cha upasuaji, wakaamua kupitia mlango wa nyuma!”
“Mawazo mabaya hayo baba Catarina, hawawezi kufanya hivyo.”
“Kwa nini sasa angalau asijitokeze mmoja na kutueleza kinachoendelea?”
“Watatoka tu!”
Yalikuwa ni mazungumzo ya watu wenye wasiwasi, Kevin hakuongea chochote, alikuwa kimya akimwomba Mungu atende muujiza wake, moyoni mwake aliamini Catarina angetoka salama lakini akilini mwake kulikuwa na wasiwasi mwingi hasa baada ya kuwasikiliza wazee wake wakijadiliana bila kupata jibu.
“Mungu nakuomba utende muuji…”
Hakuweza kumaliza sentensi yake hadi mwisho mlango wa chumba cha upasuaji ukafunguliwa, akatokeza Dk. Ngamila mwili wake wote ukiwa umelowa jasho, kwa kumwangalia tu usoni alionekana wazi kabisa hakuwa na taarifa nzuri sana, palepale mama yake Catarina akaanza kububujikwa na machozi huku mume wake akimkumbatia kumbembeleza.
“Usilie mama Catarina, subiri kidogo tuone anataka kutueleza nini.”
Je, nini kitaendelea? Dk. Ngamila ana ujumbe gani? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/