ILIPOISHIA IJUMAA:
Niliposema hivyo ndiyo nilimpandisha.
“Kama ule ndiyo uchawi wa kwenu, hutaki viondoke mle chumbani, nakwenda kuutupa ule mkoba kwenye pipa la takataka!”
Akainuka na kuchanganya mwendo kuelekea chumbani. Na mimi nikanyanyuka na kumfuata.
“Hebu subiri,” nikamwambia tulipoingia chumbani.
Mwanamke akasimama na kunitazama.
SASA ENDELEA…
Nikainama mvunguni na kuutoa ule mkoba.
“Huu ni mkoba tu, una tatizo gani mpaka ukaja juu kiasi hicho?” nikamuuliza.
“Mkoba tuu…” alikariri maneno yangu kisha akaongeza.
“Mkoba tuu…na huo mkono wa mtoto mchanga humo ndani ni wa nini?”
“Hamna mkono wa mtoto mchanga humu,” nikamwambia huku nikitoka na ule mkoba.
“Hebu ufungue tuone kama hamna mkono wa mtoto.”
“Huu mkoba ni zindiko. Nilipewa na babu yangu, hujui hili jiji lina wachawi wengi!”
“Kama ni zindiko kaliweke ofisini kwako. Mimi silitaki humu ndani.”
“Basi nayaishe. Naona umezidi kupandisha sauti, mwisho nyumba ya pili watatusikia,” nikamwambia mke wangu kwa sauti ya upole.
“Unayataka mwenyewe. Mimi nimekwambia uondoe huo mkoba wako humu chumbnani, unaniletea maneno meeengi…”
“Basi nauondoa.”
Nilikuwa nimekasirika ingawa usoni mwangu nilijifanya natabasamu. Nikatoka mle chumbani na mkoba wangu mkononi.
Nilikuwa nataka kwenda kutafuta sehemu ya kuuweka huko uani hadi kesho yake ambapo ningejua nitaupeleka wapi. Nikaona mke wangu akinifuata nyuma.
Nikasimama ghafla na kumuuliza kwa ukali.
“Sasa unanifuata wapi?”
“Nataka nione huko unakoupeleka.”
“Uone, kwani inakuhusu nini?” nilimuuliza hivyo huku nikimtazama kwa ukali.
Mke wangu akanywea.
“Kwani unaupeleka wapi?”
“Unautakia nini?”
“Basi nayaishe.”
Mke wangu akageuka na kurudi lakini maneno yalikuwa yakimtoka.
“We uweke unapouweka lakini kesho uuondoe ukautafutie mahali pengine pa kuuweka, si humu ndani.”
Nikaenda uani. Nilikuwa nataka kuuficha lakini sikusumbuka tena kutafuta mahali pa kuuficha. Nilikwenda kuuweka sehemu huku nikijiambia kama mke wangu atakuja kuuondoa nitapambana naye.
Nikarudi ndani. Nilikwenda kuoga nikavaa nguo za nyumbani na kwenda kukaa kimya barazani mwa nyumba yetu.
Kusema kweli kile kitendo cha mke wangu cha kuingilia suala la mkoba wangu kilikuwa kimeniudhi sana. Nikaamua nikae peke yangu pale nje mpaka akili yangu itakapotulia.
Nikamuona mke wangu akinichungulia kwenye dirisha. Alinichungulia kwa muda mrefu akidhani nilikuwa simuoni. Mwisho alitafuta mbinu ya kunisemesha kwa vile aliona nilikuwa nimekasirika.
“Nikuletee mtoto umshike?” akaniuliza.
“Mlete,” nikamjibu kwa mkato.
Muda kidogo akamleta Mkanga.
Aliponipa mtoto huyo na yeye alikaa hapohapo. Ilikuwa ndiyo sifa mojawapo ya mke wangu. Alikuwa mkali sana kutetea kile alichoamini ni sahihi lakini ni mnyenyekevu pale anapoona ameniudhi. Hutafuta kila mbinu ya kuhakikisha yuko karibu na mimi ili atulize ghadhabu zangu.
“Mbona huzungumzi, upo kimya?” akaniuliza alipoona zimepita karibu sekunde sitini bila kumsemesha chochote.
Aliniuliza hivyo kwa hekima kwani alijua kuwa maneno yake yalikuwa yameniudhi.
“Hata wewe unaweza kuzungumza,” nikamwambia.
“Sawa. Mimi nilikuwa nakushauri tumfungulie akaunti mtoto wetu kwa ajili ya maisha yake ya baadaye. Wewe mwenyewe hujui utakuwa waziri hadi lini.”
Aliponiambia hivyo nilishindwa kujizuia kucheka.
“Mbona unanicheka au nimetoa wazo baya?” akaniuliza.
“Ni wazo zuri lakini ni mapema mno kumfungulia akaunti huyu mtoto, bado ni kichanga sana.”
Je, kilifuatia nini? Usikose kusoma katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.