Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.
Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari na kuacha gumzo kubwa jijini Arusha, wanasafiri mpaka kwenye Visiwa vya Hawaii kula fungate.
Wakiwa kwenye fungate, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego.
Anaificha siri hiyo moyoni mwake na kumfanya Msuya aamini kwamba ni mimba yake. Baada ya kukaa mwezi mzima Hawaii, hatimaye wanaianza safari ya kurejea jijini Arusha.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Wakaingia ndani ya ndege kubwa na ya kisasa iliyokuwa na maandishi makubwa ubavuni yaliyosomeka KLM, Msuya akawa anamsaidia Arianna kwa kila kitu, mpaka kupanda ngazi za kuingia ndani ya ndege hiyo.
Dakika kadhaa baadaye, tangazo lilisikika kutoka kwa mhudumu wa ndege akiwataarifu abiria wote kufunga mikanda kwani ndege ilikuwa ikijiandaa kupaa. Msuya akamsaidia Arianna kufunga mkanda kisha akamtegulia siti yake ili aendelee kulala.
Safari ya kurejea Tanzania ikaanza huku wakitarajiwa kubadilisha ndege mara mbili njiani, Doha, Qatar na Nairobi, Kenya. Njia nzima Arianna alikuwa ameuchapa usingizi, hakuwa na habari na kilichokuwa kinaendelea.
Msuya akawa na kazi ya kumgeuza na kumlaza vizuri ili asiumie shingo kwani kuna wakati alikuwa akilala vibaya kwenye siti aliyokuwa amekaa. Baada ya safari ndefu iliyochukua saa nyingi angani, hatimaye wanandoa hao waliwasili jijini Nairobi ambapo walishuka kwenye ndege waliyokuja nayo na kupanda nyingine, Kenyan Airways iliyowasafirisha mpaka jijini Arusha.
“Thanks God finally we are back home safely,” (Ahsante Mungu hatimaye tumerudi nyumbani salama) alisema Msuya wakati wakiteremka kwenye ngazi za ndege hiyo, Arianna akaachia tabasamu hafifu kwenye uso wake.
Wakateremka na kuingia kwenye jengo la uwanja huo, wakasubiri mizigo yao na hatimaye wakatoka uwanjani hapo mpaka nje ambapo dereva wao alikuwa akiwasubiri sambamba na ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wameshika maua kama ishara ya kuwakaribisha wanandoa hao.
Jambo hilo lilikuwa ni kama ‘sapraizi’ kwa wote wawili kwani walitegemea kumkuta dereva wao tu uwanjani hapo, wakabaki wamepigwa na butwaa. Kwa dakika kadhaa, shughuli nyingine nje ya uwanja huo zilisimama kwa muda wakati Msuya na mkewe wakipokelewa kwa shangwe, nderemo na vifijo.
Msafara wa magari manne ukaondoka uwanjani hapo na safari ya kuelekea nyumbani kwa Msuya ikaanza. Kwa muda wote huo, wanandoa hao walikuwa wamekumbatiana kwa furaha kutokana na mapokezi ya nguvu waliyoyapata.
Walipofika nyumbani, nako walikuta baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wanawasubiri kwa shauku kubwa, ambako sherehe ndogo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya kuwakaribisha wanandoa hao wapya.
“Karibuni sana dada na shemeji, vipi habari za safari,” Diego aliwasalimu Arianna na Msuya huku akijitahidi kuvaa tabasamu la bandia. Kitendo cha kumuona Diego, kilisababisha mapigo ya moyo ya Arianna yaanze kumwenda mbio kuliko kawaida. Hakuna kitu kilichokuwa kinamsumbua kama kukubaliana na ukweli kwamba ujauzito aliokuwa nao, Diego ndiye aliyekuwa mhusika.
Hata hivyo, ili kumfanya Msuya asigundue chochote, Arianna naye alijilazimisha kuvaa tabasamu bandia usoni, akapeana mikono na Diego kisha wakaingia ndani ambako waliwakuta ndugu wengine wakiwasubiri kwa shauku.
Siku hiyo ilikuwa ya kipekee kwao kwani wanandoa hao walikula, kunywa na kuburudika pamoja na ndugu waliofika nyumbani hapo. Baadaye, watu walianza kutawanyika kurejea makwao.
“Najisikia fahari sana kuwa mkeo wa ndoa,” alisema Arianna huku akijishikashika tumbo lake, Msuya akatabasamu na kumbusu mdomoni na kwenye tumbo lake.
“Nafurahi pia kuwa mumeo na kubwa zaidi, kuwa baba wa watoto wako.”
“Naomba Mungu atujalie maisha marefu na ndoa yenye amani na upendo,” alisema Arianna na kujilaza kwenye kifua cha mumewe. Siku hiyo ilipita, wawili hao wakawa wameyaanza maisha mapya, wakiwa mume na mke halali.
Hata hivyo, bado Arianna alikuwa na mzigo mzito ndani ya moyo wake, alitamani apate muda wa kuzungumza na Diego na kumueleza kilichokuwa kimetokea lakini haikuwa rahisi kwa sababu Msuya hakuwa akienda kwenye shughuli zake kwa maelezo kuwa anaendelea kuifurahia ndoa yake mpaka wiki moja itakapopita.
Arianna na Diego wakawa wanaishia kusalimiana na kuzungumza mambo ya kawaida tu, huku kila mmoja akiwa na shauku ya kuzungumza na mwenzake. Kuendelea kukosa nafasi ya kuzungumza na Diego na kumueleza kilichokuwa kimetokea, kulimfanya Arianna azidi kuwa na mawazo.
Ili kukabiliana na hali hiyo, kila alipokuwa anapata muda Arianna alikuwa akienda kujidunga madawa ya kulevya kwa siri kisha kuuchapa usingizi mzito. Japokuwa Msuya alikuwa akishinda naye kutwa nzima, wala hakuhisi kwamba mkewe anaweza kuwa anatumia madawa, tena katika kipindi hicho alichokuwa mjamzito. Alichojua ni kwamba mkewe analala sana kwa sababu ya hali yake ya ujauzito.
Hatimaye wiki moja iliisha, Msuya akaanza kwenda kwenye shughuli zake kama kawaida. Siku ya kwanza alipoondoka tu, Diego hakutaka kulaza damu, alimfuata Arianna mpaka sebuleni alipokuwa amekaa na kumuomba wakazungumze.
“Tuzungumzie tu hapahapa Diego, mimi mwenyewe nina jambo la muhimu sana la kuongea na wewe.”
“Hatuwezi kuzungumzia hapa, twende chumbani kwako.”
“Siwezi kukupeleka kwenye chumba ninacholala na mume wangu, utanisamehe kwa hilo.”
“Twende basi hata kwenye chumba cha wageni,” alisema Diego huku akionesha kuzidiwa na hisia za kimapenzi lakini Arianna aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba wazungumze hapohapo sebuleni.
“Arianna ‘nimekumisi’ mwenzio, twende ukanipe haki yangu japo kidogo,” alisema Diego huku akimshika mkono Arianna na kutaka kumuinua lakini bado msichana huyo hakukubaliana naye.
“Tuongelee hapahapa,” alizidi kusisitiza Arianna, Diego akawa hana cha kufanya zaidi ya kukaa kwenye sofa huku akimtazama Arianna kwa matamanio kama fisi aliyeona mfupa.
“Diego, mwenzio nipo kwenye matatizo makubwa sana, hapa nilipo nina ujauzito wako,” alisema Arianna, kauli iliyomshtua mno Diego.
“Unasemaaaa?” alihoji huku akiwa ni kama haamini, akasimama pale alipokuwa amekaa na kumsogelea Arianna.
“Nina mimba yako!” Arianna alirudia kwa msisitizo.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/