ILIPOISHIA
“Unahitaji nini?’ aliuliza mzee Bashir, kikao kizima kilikuwa kimya, japokuwa walifika hapo kwa ajili ya kuzungumzia uchumi wa Afrika, lakini wakaacha vyote na kuanza kuzungumza na Elizabeth.
SONGA NAYO…
“Nataka kuwa trilionea!”
“Hilo tu?”
“Ndiyo! Nitafurahi sana kwani kuna mengi ninataka kuyafanya!”
“Ni vizuri, ila kuna vitu unatakiwa kuvifanya kabla ya kuwa trilionea.”
“Vitu gani?” aliuliza Elizabeth huku akiwa na hamu ya kutaka kusikia, akajiweka vizuri kitini.
“Umekuja kufanya nini Morocco?” aliuliza mzee Bashir.
“Kufanya uzinduzi wa mavazi yangu!”
“Sawa! Unaweza ukaanza na hicho kuwa trilionea. Zunguka sehemu mbalimbali, tumia kiasi kikubwa cha fedha katika kutafuta soko. Ngoja nikwambie kitu kimoja, unapoamua kutafuta utajiri, usijali kuhusu muda wako, unapokwenda kuonana na mfanyabiashara mkubwa, ukawekwa mapokezi kwa saa nne bila kutokea, usihuzunike, hata kama baada ya saa hizo ukaambiwa kwamba mfanyabishara huyo hayupo na urudi kesho, usilalamike, simama na uondoke zako, kesho rudi.
“Unapotafuta mafanikio, ni lazima ujue kwamba kuna kujitoa na kujinyima, hautakiwi kukata tamaa, unapoambiwa fanya jambo fulani, hata kama litahatarisha maisha yako, wewe fanya ila hakikisha hilo jambo halivunji sheria ya nchi.
“Wengi wanatamani kuwa mabilionea, sawa, wanaweza, ila swali ni kwamba wanaweza kupita tulipopita? Wanaweza kupigana kama tulivyopigana? Jibu ni kwamba hawako tayari, kama ni hivyo basi dunia itaendelea kuwa na mabilionea wachache,” alisema mzee Bashir, mabilionea wote waliokuwa kwenye meza ile wakaungana naye.
Muda wote Elizabeth alikuwa akitabasamu tu, maneno aliyokuwa akiambiwa na mzee huyo yalimfurahisha na kumpa nguvu ya kujua kwamba angeweza kusimama na kusonga mbele.
Ni kweli alikuwa bilionea, mwanamke mwenye fedha kuliko wanawake wote barani Afrika, hakutaka kuridhika, hivyo alitamani kuwa trilionea kama matajiri wale waliomzunguka.
“Umaarufu unaweza kuchangia kuwa bilionea? Kama jibu ni ndiyo! Vipi kuhusu nyie? Mbona mmekuwa mabilionea bila kuwa maarufu kabla?” aliuliza Elizabeth, matajiri wote wakaangaliana, wakatoa tabasamu, swali hilo liliwafurahisha mno.
“Hapa Morocco kuna sehemu inaitwa Tangier, hii ipo kaskazini mwa nchi hii, mtu wa kule anapotaka kwenda Hispania ambapo ni karibu sana, huwa haendi Rabat au Casablanca kupanda ndege, ili wafike Hispania, wanachokifanya ni kupata mtumbwi tu, wanatumia saa mbili mpaka kufika Hispania. Ila kama wangekuwa wanakwenda kwanza Rabat au Casablanca, wangetumia saa tano angani, kule wakichukua ndege wanatumia zaidi ya saa kumi mpaka Hispania,” alisema mzee Bashir.
“Unamaanisha nini?”
“Unapokuwa hauna umaarufu, utatumia nguvu nyingi sana mpaka kuwa bilionea, unaweza ukaanzisha biashara yako lakini kama huna watu wanaokufahamu, utakuwa na wakati mgumu kuwauzia watu kile ulichokuwa nacho, ila unapokuwa maarufu, amini kwamba utapata fedha nyingi kwa sababu kila mtu atataka kutumia kile ulichobuni,” alisema mzee huyo.
“Kuna kingine?”
“Ndiyo! Katika dunia ya sasa hivi ni vigumu sana kuwaona watu maarufu wakiwa mabilionea, unajua kwa nini? Wengi wanaridhika, wanapopata umaarufu wanaona wamepata kila kitu.
Kwa wanaume, wanalala na wanawake wanaowataka, kwa wanawake wanalala na wanaume wowote wanaowataka. Watahitaji nini kama magari wanayo, nyumba wanazo? Wengi wanaridhika na hivyo kushindwa kuendelea mbele.
“Kesho, mtoto wa maskini asiyejulikana anaibuka na kuwa tajiri mkubwa, anapopata umaarufu baada ya kutangazwa kila kona, utajiri wake unaongezeka zaidi, tatizo la watu maarufu wanaridhika sana ndiyo maana ni vigumu kuwa mabilionea,” alisema Bashir, wenzake wakatingisha vichwa kuonesha walikubaliana naye.
“Nashukuru sana, kuna la kuniongezea?”
“Ndiyo!” akadakia tajiri mwingine, huyu alikuwa Efrahim Noah kutoka Nigeria.
“Kipi?”
“Unatakiwa kuwadanganya watu katika biashara zako,” alisema Efrahim.
“Kuwadanganya?”
“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Kwa mfano umekwenda dukani, ukahitaji kununua kitu, pale ukamuona mwenye duka amekunja ndita, utaweza kwenda siku nyingine?”
“Hapana!”
“Kwa nini?”
“Kwa nini akunje ndita sasa?”
“Yeah! Unatakiwa kutabasamu. Huwa tunapitia katika matatizo mengi sana ambayo nitakueleza ili kuimarisha biashara yako,”
Noah akamwambia
Elizabeth.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/