Haruna Niyonzima akiwa na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko.
Nicodemus Jonas,
Dar es Salaam
KUREJEA kwa fundi wa pasi, Haruna Niyonzima kikosini baada ya matatizo yake na uongozi wa Yanga, kumezua minong’ono juu ya nani acheze dimba la juu, jukumu ambalo alikuwa amekabidhiwa Mzimbabwe, Thaban Kamusoko.
Katika kipindi chote ambayo Niyonzima hakuwepo Yanga iliendeleza moto wake wa kugawa dozi ya vipigo, huku Kamusoko akionekana kuimudu nafasi hiyo, ambapo amefanikiwa kutupia kambani mabao matano na akiwa ametoa asisti saba (kwenye ligi na Mapinduzi), lakini kurejea kwa ‘maestro’ huyo kumetafsiriwa kivingine.
Hata hivyo, Niyonzima amemaliza chokochoko hizo kwa kufunga hatima ya nafasi yake kwa kusema kuwa mchezaji anayehitaji mafanikio lazima akumbane na ushindani wa kutosha.
“Katika maisha yangu napenda ushindani na mchezaji anayetaka mafanikio lazima acheze katika timu yenye ushindani. Kweli, sikuwepo na timu ilikuwa inafanya vizuri na nimefurahi kwa hilo. Kurudi kwenye timu kubwa kama Yanga, moja kwa moja siwezi kuwa Haruna yule watu waliyemtegemea, maana nilikuwa kwenye matatizo lakini nitajitahidi kuhakikisha narejea katika kiwango changu,” alisema Mnyarwanda huyo.