×

Bayo na Imbori-36

ILIPOISHIA:

Watuhumiwa wengine wakizidi kusakwa kwenye kesi ya kupigwa risasi Imbori, Dickson na Dk. Mand wanapanga kumuua Bayo. Sumu kali inawekwa kwenye chakula alichotakiwa kula kijana huyo katika mlo wake wa mchana, Dickson na Dk. Mand wanabanisha mahali fulani Bayo akiwa mezani anataka kula chakula hicho huku wakiwa na matumaini ya kulifanikisha zoezi lao.

Telemka nayo…

WAKIWA eneo hilo wamebanisha walimshuhudia Bayo akiinua kijiko chenye chakula lakini kabla hajakifikisha mdomoni mara simu yake iliita, Bayo akakishusha na kukiweka pembeni kisha akapokea simu.

Muda usiopungua dakika tano ukakatika akiongea kupitia simu yake na mtu ambaye si Dickson wala Dk. Mand  waliweza kumfahamu, baada ya kukata simu kijana huyo aliinuka bila kukigusa chakula tena, akaanza kuelekea chumbani kwake jambo ambalo liliwashangaza sana a                          kina Dickson.

 “What’s goin’on?” (Nini kinaendelea?) Dickson alimuuliza Dk. Mand.

“I can’t know.” (Siwezi kufahamu.)

* * *

Nchini Tanzania baada ya Bayo kuondoka biashara zake zote zilibaki mikononi mwa Fransic Stambuli, rafiki yake na meneja mkuu waliyeshirikiana katika mambo mengi kwa muda mrefu.

Fransic akiendelea kuzisimamia biashara hizo, katika hali ya kushangaza wiki moja baada ya Bayo kwenda Marekani, bila sababu za kueleweka vituo vyake vyote vya mafuta kwa nyakati tofauti vililipuka kwa moto hali iliyosababisha sintofahamu ndani ya jiji zima la Dar es Saalam.

Lakini matukio hayo ya kutisha yakiwa bado hayajatulia, pia nyumba yake kubwa iliyokuwa maeneo ya Madale, Tegeta, iliteketea kwa moto kutokana na shoti ya umeme iliyoelezwa kusababishwa na mmoja wa walinzi waliokuwa wanailinda nyumba hiyo.

Kila siku matukio mapya na ya kutisha yalitokea kwenye mali za Bayo, maneno yakaanza kuenea kila kona kuwa huenda mali zake zilikuwa ni za kishirikiana na ziliteketea baada ya kukosea masharti. Hayo yote yalisemwa lakini hakuna aliyekuwa na uhakika wa uvumi huo kuwa na uhusiano na matukio hayo yaliyokuwa yanatokea.

Taarifa hizo za kuurudia umaskini ndizo zilimfanya Bayo ahisi kuchanganyikiwa baada ya kupigiwa simu na mmoja wa wafanyakazi wake akiwa mezani anajiandaa kula chakula.

Aliinuka mezani hapo na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye chumba alichokuwa anakitumia nyumbani hapo kwa Dickson kisha kuanza kulia kama mtoto mdogo maana umaskini ni kitu ambacho alikuwa amekwishakisahau wakati huo na hakuwa anahitaji kabisa kuusikia katika maisha yake yote.

Aliwaza angeanzia wapi baada ya kurudi Dar es Salaam lakini hakupata jibu.  Mawazo yalimpeleka mbali hadi kufikiria kitendo alichokuwa amekifanya kwa ajili ya kuyaokoa maisha ya msichana aliyekuwa anampenda sana Imbori, kutoa figo.

Akajutia kosa kubwa alilolifanya la kuyakataa mamilioni ya pesa ambayo alitakiwa kupewa na Dickson. Roho ilimuuma mno Bayo,  akajihesabu kuwa mjinga wa kwanza miongoni mwa wajinga wote duniani, lakini akiwa bado anaelekea kwenye kilio hicho kilichoambatana na msongo wa mawazo, mlango ulifunguliwa na akaingia ndani Imbori.

“Bayo!” msichana huyo aliita, Bayo aliinua uso na kumtazama.

“Mbona unalia?” aliongeza kwa kuuliza swali.

“Imbori unanipenda kweli?”

“Ndiyo! Kwani vipi?”

“Hakuna zaidi ila kama unanipenda naomba tuondoke hapa nyumbani kwa Dickson.”

“Tutawezaje?”

“Hilo niachie mimi.”

Imbori hakuwa na kauli yoyote kwa Bayo, kweli alikuwa anampenda sana Dickson kutokana na mambo mengi aliyokuwa amemfanyia wakati ambao Bayo hakuwa kwenye upeo wa macho yake.  Lakini hilo lisingefanya ashindwe kuuthamini upendo wa kijana huyo ambaye alimuua Sangika kwa ajili yake, alimuokoa kifo katika Msitu wa Dikwe ulioko mkoani Manyara na amethubutu kutoa figo ili kuokoa maisha yake.

“Nakupenda sana Bayo!”

“Mimi pia Imbori.”

“Niko tayari kufanya lolote kwa ajili yako, naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea, nilikuwa ndani ya fumbo ambalo sikuweza kulifumbua.”

“Usijali mpenzi, upendo wetu uko ndani ya damu.”

“Kweli kabisa.”

Wawili hao walikumbatiana huku machozi yakiwabubujika, baada ya kuachiana walipanga mipango juu ya kuikamilisha dhamira waliyokuwa nayo ya kutoroka nyumbani kwa Dickson na kukubaliana kulifanya zoezi hilo asubuhi ya siku iliyofuata.

Bila Bayo kufahamu kuwa wakati anapanga mipango hiyo na Dickson alikuwa anapanga yake, usiku wa manane akiwa anasubiri kwa hamu kupambazuke ili atoroke na Imbori nyumbani hapo kwa Dickson, alishangaa kuona mlango wa chumba chake ukifunguliwa kwa kishindo kikubwa wakaingia ndani vijana watano waliovaa mavazi meusi. Kabla hata hajajitetea wala kufahamu afanye nini walimvamia na kumfunga kitambaa cheusi usoni.

Je, nini kitaendelea? Bayo atatekwa na kupelekwa wapi? Vipi kuhusu Imbori? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment