×

Asanteni kwa kuja

SIMBA-YANGA-4.jpgKikosi cha timu ya Simba.

Waandishi Wetu,
Dar es Salaam na Tanga
ASANTENI kwa kuja ndiyo kauli inayotawala kwa makocha wa Simba na Coastal Union ambao leo Jumamosi wataziongoza timu zao dhidi ya Africans Sports na Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara.

SIMBA-YANGA-3.jpg

Kikosi cha timu ya Yanga.

Ni mechi za kwanza za mzunguko wa pili wa ligi hiyo lakini zimebeba hisia kubwa kwa kutegemea kuwa, moja inachezwa Tanga na nyingine Dar es Salaam ikihusisha timu za miji hiyo.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Coastal Union inacheza na Yanga ambayo inapambana kubaki kileleni ikiwa na pointi 39, kama Azam FC isipokuwa inaongoza kwa tofauti ya mabao.
Coastal Union ambayo ipo nafasi ya 14 katika msimo wa ligi, imekomaa kwa kusema haitakubali kufungwa tena na Yanga kwani awali katika mzunguko wa kwanza, walifungwa mabao 2-0 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Coastal Union, Salim Bawazir, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, timu yao ipo vizuri tangu Kocha Ally Jangalu ajiunge nao akichukua nafasi ya Jackson Mayanja aliyejiunga na Simba.
“Timu yetu imebadilika na ilivyo sasa siyo kama zamani, wachezaji walikuwa wanacheza kipindi cha kwanza tu halafu kipindi cha pili wanaishiwa pumzi. Safari hii hatukubali kabisa,” alisema Bawazir.
Kwa upande wake, Jangalu alisema: “Najua Yanga ni timu kubwa na iliyo imara, lakini sisi pia tuna kikosi kizuri pia, halafu tuna faida ya kucheza nyumbani, tutapambana kupata ushindi.
“Tulicheza na African Sports (katika Kombe la FA) tukashinda mabao 3-0, moto ule tutautumia katika mechi hii na Yanga, mashabiki watuunge mkono tutashinda.”
Hii ni mechi ya tatu ya ligi kuu kwa Jangalu tangu atue Coastal Union, ya kwanza ilikuwa dhidi ya Majimaji akatoka sare ya bao 1-1, ya pili dhidi ya Prisons jijini Mbeya akafungwa mabao 2-1 na leo ni ya tatu.
Yanga jana asubuhi ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkwakwani na Kocha Hans van Der Pluijm alionekana akisisitiza kuhusu soka la pasi ndefu tu kwa wachezaji wake.
“Uwanja huu tutautumia kwa mechi kesho (leo) haupo katika ubora kama vile tulivyovizoea vya Dar es Salaam, tunatakiwa kucheza pasi ndefu zenye manufaa na si zaidi ya hapo,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.
“Najua wapinzani wetu watacheza kwa kukamia sana, sasa katika hali hiyo na kulingana na hali ya uwanja, hatutakiwi kucheza soka la siku zote, tunachotaka ni matokeo na tumejiandaa kwa hilo.”

SIMBA, AFRICAN SPORTS
Katika mchezo mwingine wa ligi kuu leo Jumamosi, Simba itaikaribisha Afican Sports kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Mayanja amesema hana presha kwani wamejiandaa vizuri.
Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33 na imezidiwa pointi sita tu na Yanga inayoongoza ligi, hivyo Mayanja ameliambia gazeti hili kwamba, ushindi ni lazima kwake ili wakae sehemu nzuri ya kuwania ubingwa.
“Tuna ndoto za ubingwa na kikosi chetu kinazidi kuimarika, hapa tutahakikisha tunaifunga African Sports halafu zitabaki pointi tatu tu na tunaomba walio juu yetu wafungwe,” alisema Mayanja.
Mayanja aliyechukua nafasi ya Dylan Kerr, tayari ameiongoza Simba katika mechi mbili za ligi kuu na kushinda zote ambazo ni dhidi ya Mtibwa Sugar (1-0) na JKT Ruvu waliyoshinda mabao 2-0.
“Naijua kwa kiasi fulani African Sports, tutafanya vizuri dhidi yao na kuwapa asante ya kuja na wachezaji wangu wana ari kubwa ya ushindi,” alisema Mayanja, raia wa Uganda.

AFRICAN SPORTS MCHECHETO
Ni kama ina mchecheto, kwani jiji zima la Tanga jana asubuhi taarifa zilizokuwepo ni timu hiyo iliondoka kwenda Dar es Salaam tayari kwa mchezo huo lakini Kocha Ramadhan Aluko akazuga eti wanaondoka leo kwa ndege.
Taarifa kutoka Tanga zimeeleza kuwa, timu hiyo imeondoka kwa msaada mkubwa wa serikali ya mkoa ili ishinde mechi hiyo na kuiweka katika nafasi nzuri kwani ina pointi tisa katika nafasi ya 15.
“Tupo vizuri kucheza na Simba na wala hatutishiki na jina la timu, tunaingia Dar es Salaam kwa ndege ili kutoweka mazingira ya kupoteza mechi hii muhimu,” alisema Aluko ambaye ni mtaalamu wa soka la vijana.
Gazeti hili limehakikishiwa kuwa African Sports ilifika Dar es Salaam tangu jana Ijumaa mchana na kujichimbia mafichoni tayari kwa mchezo wa leo.

MECHI NYINGINE
Katika michezo mingine ya leo Jumamosi ya ligi kuu, JKT Ruvu inacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar dhidi ya Stand United (Manungu), Mwadui na Toto Africans (Mwadui Complex) na Kagera Sugar dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Mgambo JKT itaikaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.

Imeandaliwa na Sweetbert Lukonge na Abdallah Juma

Leave a Comment