×

Mjane: Askofu ananidhulumu nyumba

Na Joseph Ngilisho, Risasi Jumamosi

ARUSHA: Askofu wa Huduma ya Jesus Call Mission International, Paulo Jonas Macha iliyopo jijini hapa analalamikiwa na mjane Lina Ngowi kwamba anataka kumdhulumu nyumba yake yenye thamani ya shilingi milioni 800 iliyopo Levolosi, Ploti Namba 460 Block X, tambaa na Risasi Jumamosi.
Aidha, askofu huyo anadaiwa kukataa kulipa kiasi cha shilingi milioni 10 ikiwa ni kodi ya pango huku akidaiwa kubadilisha matumizi ya nyumba hiyo kinyemela na kuwa kanisa kinyume na makubaliano ya mkataba wa upangaji.
Akizungumza na Risasi Jumamosi hivi karibuni, mama huyo ambaye alikuwa muumini wa kanisa hilo alisema aliingia makubaliano ya kumpangisha nyumba askofu huyo mwaka 2004.
“Nyumba ina ukubwa wa vyumba 8 vya kuishi. Nilimpangisha kwa makubaliano ya kunilipa kodi ya shilingi elfu 80 kwa mwezi na alikuwa akilipa kila baada ya miezi 6.
“Kodi hiyo ilikuwa ikiongezeka hadi kufikia shilingi laki 4, Desemba 2013. Akaamua kusitisha malipo ya pango,” alisema mjane huyo.
Aliongeza kuwa, Januari ya mwaka 2014, Manispaa ya Jiji la Arusha walimuandikia barua wakisema majirani zake wanamlalamikia kuhusu mpangaji wake huyo kuendesha maombi katika nyumba hiyo yaliyokuwa yakiwakera kwa muziki nyakati za mchana na usiku.
“Ilinilazimu kumfungulia mashitaka kwenye Mahakama ya Ardhi sambamba na kumtaka ahame.
“Juni 5, mwaka 2015, mahakama ilitoa hukumu ya kumtaka askofu alipe stahili zote ninazo mdai na kumwambia ahame, lakini alishindwa kutekeleza badala yake amehamishia kanisa eneo la Mbauda na kuendelea kujimilikisha nyumba yangu huku na yeye akipangisha watu wengine kinyume na hukumu ya mahakama.
“Hivi tunavyozungumza hajanilipa kodi ya miaka miwili inayofikia shilingi milioni 10. Nimemwambia aniachie nyumba yangu lakini amekataa. Ninaiomba jamii inisaidie mimi ni mjane,’’ alisema mama Ngowi.
Kwa upande wake, Askofu Macha alikana kudaiwa na mjane huyo kiasi hicho cha fedha na kueleza kuwa, yeye ndiye anayemdai mwenye nyumba hiyo shilingi milioni 4 baada ya kufanya marekebisho kwenye nyumba yaliyogharimu shilingi milioni 38.
“Huyu mama hanidai. Hii nyumba wakati naanza kupanga ilikuwa mbovu sana, tukakubaliana nimlipe shilingi elfu 80 mwaka 2004, kati ya hizo shilingi elfu 40 zilikuwa zikibaki kwa ajili ya matengenezo ya nyumba na yeye akipokea shilingi elfu 40. ’’
Aliongeza kuwa, makubaliano hayo yaliendelea hadi mwaka 2013 ambapo gharama za marekebisho ya nyumba zilifikia shilingi milioni 38 jambo ambalo lilimfanya asitishe kuendelea kumlipa kodi ya nyumba.
Askofu huyo alisisitiza kuwa, yupo tayari kuhama kwemye nyumba hiyo endapo wataafikiana na mwenye nyumba juu ya gharama za matengenezo alizotumia.
Alisema yeye ni askofu hawezi kudhulumu haki ya mtu na anasikitika kwa nini suala hilo limefika mbali wakati lilipaswa limalizwe na wao wenyewe.

Leave a Comment