
Amissi Tambwe.
Nicodemus Jonas,
Dar es Salaam
WAKATI Yanga ikishuka dimbani leo ugenini kumenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kinara wa mabao Amissi Tambwe, amewekewa mitego na Wanajelajela hao kwa kile kilichoelezwa kuwa ndiye anayewanyima usingizi.
Kichapo cha mabao 2-0 walichokumbana nacho Yanga mbele ya Coastal Union wikiendi iliyopita, kimewapa kiburi Prisons ambao wanaamini kama waliweza kuifunga Simba uwanjani Sokoine, basi sasa ni zamu ya Yanga.
Ajabu ni kwamba Donald Ngoma wamemchukulia poa, huku wakisema Malimi Busungu ndiye mtu mwingine hatari katika mchezo wa leo.
Beki wa Prisons, Benjamin Asukile amesema kuwa Tambwe na Busungu ndiyo watahakikisha wanabanwa kama kweli wanataka pointi muhimu kama Coastal.
“Kwetu ni mchezo wa kawaida, Yanga wanafungika kama tukijipanga vizuri, muhimu ni kucheza na watu muhimu kwenye kikosi chao. Tambwe na Busungu ndiyo ambao kila tunawatazama maana hawatabiriki wale.
“Jamaa (Tambwe) anaweza kuwaumiza muda wowote kama msipokuwa makini, ndiyo maana tumeliona hilo na tunalifanyia kazi…Ngoma siyo kivile,” alisema Asukile.