×

Jini Mweusi – 68

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa amehamishia fedha zake zote katika akaunti yake ya siri, hakuna aliyejua fedha zimehamishwaje kwani aliyefanya kazi hiyo ni mtaalamu sana katika mambo ya kompyuta, anachokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Mwanza.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hivi kuna sehemu ya kupumzika humu?” aliuliza Dickson huku akimwangalia dereva aliyekuwa amempakiza.

“Unamaanisha sehemu ya kulala?”

“Ndiyo!”

“Ingia hapo nyuma, wewe tulia, pumzika kwanza, nahisi umechoka na una safari ndefu sana,” alisema dereva huku akimuonesha Dickson sehemu ambayo alitakiwa kuingia na kutulia.

“Nasikia kichwa kinauma sana, nataka nilale, nahisi kufa-kufa..” alisema Dickson huku akiingia sehemu aliyokuwa ameelekezwa ambayo ilikuwa na godoro, akatulia huko.

Hakuwa na amani hata kidogo, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili ulitetemeka mno kwani alihisi siku hiyo, tena katika usiku huohuo ndiyo ilikuwa siku ya kukamatwa kwake.

Moyo wake ulisikitika mno, alipania kuondoka jijini Dar es Salaam na kuingia jijini Mwanza ambapo huko angechukua boti ambayo ingempeleka mpaka katika Kisiwa cha Ukerewe ambacho ndicho angekitumia katika kujificha kwake.

Hata kabla theluthi ya safari haijakamilika, tayari polisi walikuwa njiani, walilisimamisha gari alilopanda ambapo aliamini kama kweli polisi hao wangelipekua, basi ingekuwa rahisi sana kukamatwa.

“Unakwenda wapi babu?” aliuliza polisi aliyelisimamisha gari lile kwa kulitaka lisogee pembeni kabisa, mkononi alikuwa na bunduki yake.

“Nakwenda Singida mkuu!”

“Kufanya nini?”

“Kuna mizigo napeleka, si unaona huko nyuma…” alijibu mzee huyo.

“Upo na nani?” aliuliza polisi huyo. Dickson alilisikia swali hilo, alitamani mzee huyo ajibu kwamba alikuwa peke yake.

“Nipo na mwenzangu…”

“Yupo wapi?”

“Huyu huku amelala!” alijibu mzee huyo.

“Hebu teremka kwanza…” alisema polisi yule na mzee huyo kufanya hivyo.

Kila polisi mahali hapo alikuwa bize akiyakagua magari yaliyokuwa yakiendelea kupita mahali hapo. Hakukuwa na nafasi ya polisi wawili kulipekua gari moja kwani magari yalionekana kuwa mengi hata zaidi ya wao wenyewe.

Alichokifanya dereva yule ni kuteremka, polisi yule akapanda na kuingia ndani. Moja kwa moja macho yake yakatua kwa Dickson ambaye alikuwa amejifunika shuka pasipo kuacha sehemu yoyote ya mwili wake kuonekana.

Polisi huyo akamsogelea pale alipokuwa na kumgusa kwa bunduki yake, alitaka aamke na kumwangalia ili aone kama alikuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta au la.

Dickson alitulia, alijifanya kukoroma na wakati alikuwa macho kabisa, tena alimsikia polisi huyo tangu akiwa nje ya gari akiongea na yule mzee. Kujitetea lilikuwa ni jukumu lake, hakukuwa na kitu ambacho kingemfanya kuinusuru nafsi yake tofauti na kufanya kitu kingine ambacho kingemfanya kuwa huru.

“Wewe bwana funua shuka nikuone…” alisema polisi yule huku akiendelea kumgusa Dickson na bunduki yake ile.

“Wewe bwana unanisikia au hunisikii? Funua shuka nikuone…” alisema polisi yule kwa sauti yenye msisitizo, Dickson akazidi  kuogopa, mapigo ya moyo wake yakazidi kudunda kwa kasi, alichanganyikiwa, hakujua nini cha kufanya, hakujua ni kwa namna gani angeweza kujiokoa kutoka kwa polisi huyo.

“Funua shuka….” alisema polisi yule wakati Dickson alipoanza kujigeuzageuza katika godoro lile.

Wazo lililomjia Dickson ni kupambana tu, hakuwa na kitu kingine alichotakiwa kufanya zaidi ya kuonesha umwamba wake na mtu wa kwanza kabisa kupambana naye alikuwa huyo polisi aliyeona kama amejipendekeza kuingia ndani ya gari hilo.

Wakati anaguswa na bunduki ile, akafunua shuka lake na kumwangalia polisi yule ambaye hakuwa ameuona sura vizuri hali iliyomfanya kutaka kuwasha tochi yake ili amtazame usoni, hata kabla hajawasha tochi hiyo, akashtukia akivutwa chini, akazibwa mdomo na kupewa kabali moja matata.

Polisi yule akabaki akikukuruka ili ajinasue kutoka katika mkono wa Dickson, alijitahidi kwenda huku na kule lakini kabali ile iliendelea kama kawaida. Alitamani kupiga kelele lakini kitendo cha kuzibwa mdomo wake ikilimfanya kushindwa kabisa kufanya hivyo.

Baadaya sekunde thelathini tu, polisi yule akaanza kulegea, mapovu yalianza kumtoka mdomoni, sekunde chache zilizofuata, mwili ukalegea na kutulia kimya.

“Kwisha habari yake…” alijisemea huku akiuchukua mwili wa polisi yule na kuuweka pembeni kwa kuuficha kisha akaenda katika kiti cha mbele na kumuita dereva aliyekuwa amesimama nje ya gari lile.

“Tuondoke…” alimwambia.

“Kivipi? Polisi yupo wapi?”

“Ametokea mlango huu mwingine, kwani hakukwambia?”

“Hapana! Ila ilitakiwa atokee mlango huu! Hawa polisi wa Tanzania bwana, huwa hawaeleweki,” alisema dereva kwa mashaka huku akipanda ndani ya gari tayari kwa kuanza safari.

Dereva hakujua kilichoendelea, alidanganywa kidogo sana na aliukubali uongo huo hivyo kuwasha gari kwa lengo la kuondoka mahali hapo. Polisi wengine walionekana kuwa bize na hawakuwa na habari kabisa kama mwenzao aliuawa ndani ya gari hilo.

Kwa kuwa walimuona wakati anaingia, hata gari hilo lilipoanza kuondoka, hawakulisimamisha, wakaliruhusu lipite pasipo kugundua kwamba hata yule mtu aliyewafanya kuwa mahali hapo usiku huo, alikuwa ndani ya gari waliloliruhusu kuendelea na safari.

Safari iliendelea ndani ya gari kulikuwa kimya, muda wote dereva alikuwa akijiuliza maswali mengi kichwani mwake, kitu ambacho kilimtatiza ni kwa namna gani polisi yule aliteremka ndani ya gari kwa kutumia mlango tofauti na ule aliopitia? Kila alichojiuliza alikosa jibu kabisa.

“Tukiwa tunakaribia kufika Mlandizi niambie…” alisema Dickson.

“Kuna ndugu yangu nataka nimshtue ili twende wote kijijini…” alijibu.

“Sawa! Sasa ungemwambia akae barabarani kabisa…”

“Sawa!”

Baada ya dakika kadhaa, tayari walikuwa wakikaribia Mlandizi ambapo Dickson alimwambia dereva asimamishe gari kwa ajili ya kumwangalia huyo mtu aliyemuita ndugu yake.

“Mbona porini?”

“Ndipo hapahapa aliposema…subiri nishuke, nikamfuate, kama ikichukua zaidi ya dakika kumi, wewe endelea na safari yako,” alisema Dickson.

“Sawa…”

Alichokifanya ni kuteremka na kuanza kuondoka mahali hapo. Kwenda Mwanza kwa kutumia usafiri wa gari hakukuwa na amani kabisa, roho mkononi na muda wote ule alihisi angekamatwa, alichokiona, kama kwenda Mwanza basi aende kwa miguu, pori kwa pori, msitu kwa msitu mpaka kufika huko. Hata ile maiti ndani ya gari, akaitelekeza.

Je, nini kitatokea mara yule dereva atakapogundua ndani ya gari nyuma ya siti kuna mwili wa  askari polisi? Tukutane wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment