×

Mkuki moyoni mwangu – 45

Catarina kumbe hakufa! Kabla ya kufukiwa na udongo ndani ya shimo lililochimbwa kama kaburi lake alizinduka na kupiga kelele, vijana waliopewa kazi ya kumzika wakashangaa, walichokifanya mara moja ni kuutoa mfuko aliokuwa ndani yake hadi nje ya shimo na kuufungua, wakashangazwa na kiumbe kilichokuwa ndani yake; msichana mrembo ambaye macho yao hayakuwahi kuona.

Wakatumia ujanja wao na kumwondoa uwanjani hapo bila kujulikana na kumpeleka nyumbani kwa mmoja wa rafiki zao, huko walimtafutia daktari aliyefika na kuanza kumtibu mpaka Catarina akapata nafuu kabisa na kuamua kupiga simu nyumbani kwa wazazi wake Tanzania akiwa tayari amekwishawasimulia vijana hao kilichomtokea.
Aliyeongea naye ni mama yake, ambaye hakuamini kama alikuwa akisikia sauti ya Catarina baada ya muda mrefu, akamuuliza kama amekwishaonana na Kevin, Catarina akakataa! Maongezi kati yao yakaendelea, mama akitaka kufahamu ni wapi mtoto wake alikokuwa, alichojibu Catarina ni kwamba “Mama ni kama nilikuwa kuzimu”
Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

“Kuzimu wapi mwanangu?”
“Mama!” Catarina aliita huku kwikwi za kulia zikianza kusikika.
“Ndiyo mwanangu!”
“Tangu niondoke Tanzania kuja kufanya kazi ya mitindo ni mateso matupu, kuna kitu dunia haikifahamu kuhusu Uanamitindo wa Kimataifa, watoto wa kike wanageuzwa watumwa wa ngono, wakiuzwa kama bidhaa na mawakala wao kwa mabilionea! Mimi nilikuwa mgumu kukubali kwa sababu ya kumtunzia Kevin bikira niliyomuahidi kwamba angenikuta nayo wakati wa ndoa, lakini nikafanyiwa hila mpaka nikabakwa na tajiri aitwaye Jackson Motown, bilionea kabisa mwenye ushawishi, mara ya kwanza tukiwa Afrika Kusini na mara ya pili tukiwa kwenye ndege yake mpaka nikapoteza fahamu, wakadhani nimekufa na kuamua kunizika ndani ya uwanja wa ndege, ninavyoongea na wewe mama hivi sasa ningekuwa marehemu, Mungu tu aliingilia kati…” Catarina alishindwa kuendelea alipofika hapo akaangua kilio kwa sauti kubwa.
“Mwanangu! Mwanangu!Mwananguuuuuu! Ni bora urudi nyumbani.”
“Nakuja mama, lakini siwezi kumwacha Kevin huku, lazima nimtafute tukikutana tutarejea nyumbani pamoja!”
“Ongea na baba yako huyu hapa.”
Catarina alimsimulia baba yake yote yaliyompata bila kuona aibu, hasira zikampanda mzee David na kujikuta akipanga kusafiri kwenda Marekani siku iliyofuata, Catarina alijaribu kumsihi baba yake atulie lakini haikuwezekana, mwisho wa mazungumzo yao mzee David mwenyewe alikuwa akibubujikwa na machozi kwa uchungu wa mambo aliyotendewa binti yake.
“Kevin?”
“Sijamwona, ndiyo kwanza mama amenieleza, hapa nilipo nimejificha, waliotaka kuniua wanaamini mimi ni marehemu, wakijua niko hai wanaweza kunimalizia!”
“Ninakuja, kama ni kuniua waniue na mimi pia, nakufuata mwanangu!”
“Hapana baba tulia huko huko mpaka hali itakapokuwa sawa.”
“Lini?”
“Hawa walioniokoa wana mpango wa kuwasiliana na FBI ili nitoe maelezo yatakayofanikisha Jackson Motown kukamatwa, baada ya hapo ndiyo nitajitokeza hadharani na kuongea na waandishi wa habari, kisha kumtafuta Kevin mpaka nimpate!” aliongea Catarina bila kufahamu Kevin alichukuliwa kwenda kuuawa na pengine wakati huo yawezekana alishavimba na kuanza kuharibika chini ya ardhi.
“Nimekuambia nakuja!” baba yake alisema na kumrejeshea simu mke wake ambaye aliendelea kuongea na Catarina mpaka walipoagana nusu saa baadaye.
***
“I did not know Jackson Motown was such a bad person!”(Sikujua Jackson alikuwa mtu mbaya kiasi hiki!)
“Me too!”(Mimi pia!)
“How can he kill a beautiful girl like Catarina?”(Anawezaje kumuua msichana mrembo kama Catarina?)
“Leave alone killing, what about rapping?”(Achana na kuua, vipi kubaka?)
“He is rich he can date any girl he wants, why rape?”(Ni tajiri na anaweza kutoka na msichana yeyote anayemtaka, kwa nini abake?)
“He is just cruel, so he has to face the consequences, let’s go report the matter to FBI Department!”(Ni mkatili tu, kwa hiyo ni lazima akutane na madhara ya kitendo alichokifanya, twendeni tukaripoti hili suala ofisi za FBI!)
Yalikuwa ni mazungumzo ya vijana waliotakiwa kumzika lakini wakamwokoa Catarina, hata wao wenyewe uzuri wa msichana huyo uliwatisha, ki ukweli walimtamani lakini hawakuwa tayari kutumia wema waliomtendea kama njia ya kumpata, isipokuwa walitaka kuona haki inatendeka mbele ya sheria, hata kama Jackson Motown alikuwa tajiri kiasi gani.
Walipanda treni na kuwasili katikati ya Jiji la New York na kunyoosha kwa miguu mpaka stendi ya basi ambako walipanda lililowapeleka mpaka ofisi za FBI tawi la New York, wakapokelewa vizuri na baadaye kukutanishwa na mhusika wa kupokea taarifa , kwanza walimwomba asiweke majina yao hadharani naye akakubaliana na jambo hilo ndipo wakamsimulia mkasa mzima wa Catarina.
“Are you sure of what you talking about?”(Mna uhakika na mnachokiongelea?)
“Yes we are!”(Ndiyo tuna uhakika!)
“Where is the girl?” (Yuko wapi huyo msichana?)
“In my Appartment!”(Kwenye nyumba yangu!)
“Can you take us there?”(Unaweza kutupeleka?)
“Sure why not?”(Naweza, kwa nini nisiwapeleke?)
“But one thing you should know is; lying is an offence!”(Lakini kitu kimoja mnatakiwa kukifahamu kudanganya ni kosa!)
“I know and we know!”(Najua na tunajua!)
Wakanyanyuka na kutoka hadi nje wakiongozana na maofisa wawili wa FBI moja kwa moja hadi nyumbani kwa kijana huyo eneo la Brooklyn South ambako waliwasili dakika arobaini na tano baadaye na kuingia hadi ndani, hakuna aliyekuwa tayari kuamini walipokuta chumba kikiwa tupu, sakafuni kukiwa na damu!
“Catarinaaaa!Catarinaaa! Where are you?”(Catarinaaa! Catarinaa! Uko wapi?) waliita lakini hakuna aliyeitikia, nyumba ilikuwa kimya, wakaanza kuchanganyikiwa.
“So you lied?”(Kwa hiyo mlidanganya?)
“No! We left her here, something has happened, these are Jackson Motown’s evil plans, he has sent his people to hijack Catarina!”(Hapana! Tulimwacha hapa, kuna kitu kimetokea, hii ni mipango michafu ya Jackson Motown, ametuma watu wake kuja kumteka Catarina!) alijibu mmoja wa vijana hao akibubujikwa na machozi, wote walikuwa wakitetemeka, hofu kubwa iliwashika maana walielewa kwa kudanganya FBI wao wenyewe walikuwa wameingia matatani wangeweza kuishia Jela.
“Put your hands at the back!”(Wekeni mikono yenu nyuma!) mmoja wa maofisa wa FBI alisema, wakatii na kuzungusha mikono yao mgongoni, pingu zikaingia mahali pake na wakaanza kusukumwa kuelekea nje ambako walipakiwa ndani ya gari safari kuelekea makao makuu ya FBI ikaanza.

Je, nini kitaendelea? Catarina yuko wapi? Damu imetoka wapi? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

2 Comments

Leave a Comment