×

Bodaboda auawa na kutelekezwa kanisani

Na STEPHANO MANGO,
Risasi Jumamosi
SONGEA: MWENDESHA bodaboda, Victoris Bonifasi (25) mkazi wa eneo la Msamala, Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma amekutwa ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.

Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, alisema tukio hilo limetokea Februari 14, mwaka huu majira ya saa za usiku.

Alisema baada ya tukio hilo siku hiyo, ofisi yake ilipokea taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna mtu ameuawa katika eneo la Msamala karibu na Kanisa Katoliki na baada ya kupata taarifa hiyo, askari walikwenda hadi kwenye eneo la tukio ambapo waliukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha kichwani ambayo inadhaniwa alichomwa na kitu chenye ncha kali.

Alifafanua kuwa uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Victoris alikuwa ni mwendesha bodaboda na wakati anauawa alikuwa anaendesha pikipiki yake yenye namba za usajili MC 426 AGV aina ya SANLG.

Alibainisha zaidi kuwa uchunguzi huo pia umebaini marehemu kabla hajauawa alikuwa na mwanamke ambaye jina lake limehifadhiwa anayedaiwa alikuwa na ugomvi mkubwa na mwanaume mwingine aliyekuwa akimtuhumu kuwa anajihusisha kimapenzi na mwendesha bodaboda.

Hata hivyo, Kamanda Mwombeji alieleza kuwa kufuatia kutokea kwa tukio hilo, polisi inawashikilia watu wanne ambao majina yao yamehifadhiwa kwa tuhuma za mauaji hayo na upelelezi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.

Leave a Comment