×

Waziri Kigwangalla atumbua jipu la uchafu Hospitali ya Moro

Stori: Dustan Shekidele, Morogoro
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kingwangalla (pichani) juzikati alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kubaini uwepo wa uchafu (jipu) kwenye hospitali hiyo.

Kigwangalla alifanya ziara katika hospitali hiyo Jumanne iliyopita, majira ya saa 10 jioni na kutembelea wodi ya wazazi, maabara na chumba cha upasuaji ambapo kwenye maeneo hayo, alibaini uchafu uliokithiri.

“Hili la usafi nalo mnataka kuwezeshwa au kusimamiwa na serikali? Tumeamua huduma ziwe za kulipia sasa mtu atalipaje wakati wodi zenu zimejaa mabuibui, vyoo vichafu, maabara taa zina mwanga hafifu? Natoa siku 60 mrekebishe, nikija tena nikikuta hali hii naifunga hospitali na mzee wa kutumbua majipu Magufuli atafanya kazi yake,” alisema Kigwangalla.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wagonjwa ‘walimng’ata’ sikio mwandishi wetu wakisema: “Siku zote tulitakiwa kuja hapa hospitali na mashuka na mito tunashangaa nusu saa iliyopita manesi walihenyeka kutandika mashuka mapya wakati waziri huyo akiwa wodi ya wazazi, hata hivyo hakufanikiwa kutinga kwenye wodi namba 8 tungemwambia laivu tukio hilo,” alisema mmoja wa wagonjwa hao.

Leave a Comment