×

Ndoa bila watoto haina maana?

Leo na naanza na mfano, tafadhali fuatilia makala haya hadi mwisho uweze kupata elimu:
Mapenzi ya Seki na Zena yalianzia chuoni. Seki alimpenda kwa dhati Zena, Zena naye ndiyo usiseme. Penzi lao lilichanua kila uchwao. Japo hawakuwa darasa moja lakini walisaidiana kwa kila jambo.

Ndoto yao ilikuwa ni kuishi kama mke na mume. Waunganishe familia zao. Mungu awajalie watoto, wazae na kuwa na familia bora. Walivuta picha ya mbali. Walijua wote ni wasomi. Walifikiria kwamba hata watoto wao watakuja kuwa wasomi.

Watajinyima kwa kila namna ilimradi watoto wao waweze kusoma. Kama maisha yalivyo na changamoto, penzi lao nalo lilikuwa na changamoto za hapa na pale. Kuna wakati waligombana. Wakanuniana lakini baada ya muda wakasemeshana, penzi likarudi kwenye mstari.

Seki alikuwa akimkubusha ahadi yao Zena kila wakati. Zena naye alifanya hivyo pale walipokuwa wakitofautiana, alimkumbusha kwamba wanapaswa kuwa makini kwani ugomvi wao hauna thamani kubwa kufananisha na matunda ya ndoto yao.

Walijikuta wakisonga mbele. Wakiyafurahia maisha kama marafiki. Walikuwa wakisomana tabia. Wakirudishana kwenye mstari. Kila mmoja alikuwa msaidizi wa mwenzake. Kumwambia mwenzake asifanye kitu fulani kwani ni kibaya.

Kwenye sherehe walifurahi pamoja. Kwenye majonzi pia walihuzunika pamoja. Hakukuwa na kificho katika penzi lao. Ndugu jamaa na marafiki waliufahamu uhusiano wao. Waliuheshimu, waliwatakia kila lakheri katika safari yao.

Katika safari yao walimtanguliza Mungu. Kila walilokuwa wakilifanya waliamini Mungu ana kusudio na wao. Waliamini ili kufikia azma yao, Mungu lazima awapiganie. Walimuomba awajalie afya njema, awajalie pumzi ili wafikie kilele cha mafanikio pamoja.

Maisha ya shule yalifika kikomo. Bahati nzuri wote wakapata kazi. Uchumba wao ukazidi kushamiri. Baada ya miaka miwili mbele, wakafunga ndoa. Historia yao ikawa imetimia. Walijipongeza kwa safari yao.

Kwa kuwa kila mmoja alikuwa na kazi, mbali na familia zao kujimudu, wao wenyewe walichangia kwa kiasi kikubwa kuifanya sherehe yao iwe na hadhi.

“Siamini kama mimi nimekuwa mke halali wa Seki, si kwa akili zetu bali ni neema na rehema zake Mungu, sifa na utukufu tunazirudisha kwako ee Mungu wa majeshi,” Zena alimwambia Seki walipokuwa fungate, Seki naye akajibu:
“Hatuna budi kumshukuru Mungu. Kama kuachana, tungeachana kitambo sana. Tulipitia migogoro mingi lakini tunashukuru leo hii tuko pamoja. Mimi na wewe sasa ni mwili mmoja. Tumeunganisha koo zetu, mimi sasa hivi wazazi wangu ni wale wa kwako na wewe wazazi wako ni wale wakwangu. Furaha ilioje!”
Walikumbushana safari yao.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment