×

Matokeo ya kidato cha nne na kitu cha kujifunza

Ni hivi juzi tu tangu tuliposikia matokeo ya kidato cha nne yametangazwa huku asilimia za ufaulu zikishuka tofauti na mwaka 2014.

Nafahamu fika kuwa kwenye kila matokeo makubwa na muhimu kama hayo wapo wahitimu ambao wameanguka vibaya kwa kufeli na wengine waliokuwa na furaha ya kufaulu vizuri.

Wanafunzi makini hutakiwa kujifunza kupitia hali hizi mbili, kwa namna moja au nyingine na wao wataifikia steji hiyo katika  kipindi cha masomo yao ambapo watatakiwa kusubiri na kupokea matokeo muhimu hasa ya mitihani ya mwisho ambayo wameifanya.

Ni wazi kuwa wanafunzi wengi kwa nyakati tofauti wameshapitia hatua hii na wanajua changamoto zake hasa pale wanapokuwa wamefeli, vilevile wanafunzi wanafahamu jinsi furaha inavyokuwa pindi wanapokuwa wamefaulu.

Kwa namna yoyote ile mwishowe utagundua kuwa unachotakiwa ni kusoma tu ili kusonga mbele kwa kuwa hisia za kufeli huumiza zaidi na sidhani kama kuna mwanafunzi mwenye malengo ambaye angependa kukutwa na hali hiyo katika kipindi cha kujifunza kwake.

Kwa machache hayo, nitangulize pole kwa wahitimu wote wa kidato cha nne ambao wameanguka hali kadhalika niwape pongezi wale ambao wamefaulu na kati yao wale waliokuwa wakiwasiliana na mimi moja kwa moja kwa ushauri wa mara kwa mara hasa katika kuwaongezea mbinu za kusoma na kufaulu.

Vuta picha jinsi furaha ilivyo kwa msichana mdogo, Butogwa Shija ambaye ni mwanafunzi aliyeongoza Tanzania nzima kwa ufaulu wa juu wa mitihani yake ya kidato cha nne; hata wewe unaweza kufikia ndoto hiyo. Siri kubwa ni kujifunza kupitia yeye na kugeuza wivu ulionao kuwa wa maendeleo kwa kusoma kwa bidii zaidi.

Leave a Comment