×

Kamatakamata mali za vigogo…

Na mwandishi wetu

Risasi Jumamosi

DAR ES SALAAM: Matumbo joto! Hiyo ndiyo kauli unayoweza kuitumia kuelezea hali waliyonayo wadaiwa 16 waliokwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya zoezi la kukamata mali zao na kufilisiwa kuanza juzi (Alhamisi), likisimamiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart.

Wananchi mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili baada ya kuanza kwa zoezi hilo la kukamata mali za wadaiwa hao na kuzifilisi, wametoa maoni yao, wengi wakionesha kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa jinsi inavyosimamia kikamilifu mapato ya serikali.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kwamba zoezi hilo limeitikisa nchi nzima kwa maana kwamba, japokuwa wahusika wengi wanaodaiwa wapo jijini Dar es Salaam, mali zao nyingi zipo mikoani na baada ya kutangazwa kazi ya kuanza kuwafilisi, nao wameanza kujihami kwa kuzidi kuzichimbia mali zao vijijini ili isiwe rahisi kukamatwa.

“Nchi inatikisika, watu wanahaha kuficha mali zao, wengine wanazitoroshea mikoani kwa ndugu zao wakiogopa kufilisiwa. Naipongeza sana serikali, mambo kama haya yalipaswa kuanza kufanywa na marais waliopita lakini bado hatujachelewa,” alisema  Pius Mwambene, mkazi wa Mabibo jijini Dar.

Naye Pastori Kiswaga, mkazi wa Wanging’ombe, Njombe ameliambia gazeti hili kwamba tangu kutangazwa kwa amri ya kuwafilisi wadaiwa wote, pilikapilika zimeongezeka kijijini kwao.

“Naona magari mengi yameletwa huku na kuegeshwa, mengine yanashusha mizigo ya thamani, unajua huku kuna wafanyabiashara wengi ambao wanaishi Dar es Salaam lakini asili yao ni huku, yaani wengi wamechanganyikiwa vibaya,” alisema Kiswaga.

Hatua hiyo ya kukamata mali za wafanyabiashara hao, imekuja kufuatia msamaha wa siku saba uliotolewa na mheshimiwa rais kwa wadaiwa wote wa kodi kulipa kwa hiyari ambapo mwisho ulikuwa ni Desemba 12, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono iliyopewa kazi ya kufuatilia wadaiwa hao, Yono Kevella, wadaiwa 16 waliokwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kutorosha kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, ambao mali zao zimeanza kukamatwa ni hawa wafuatao:

“Said Ahmed Said, Strauss International, Farid Abdallah Salum,  Nasir Saleh Mazrui, Simbo Yona Kimaro, Ally Masoud Dama, Juma Kassem Abdul, Salum Link Tyres, Tybat Trading Co.Ltd, IPS Roofing Co.Ltd, Tuff Tyres General Co Ltd, Swalehe Mohamed Swalehe, Rushwheel Tyre General Co Ltd, Said Ahmad Hamdan, Ahmed Saleh Tawred na Farida Abdullah Salem.”

Leave a Comment