Kila mmoja alisema ni Mungu tu. Si kwa akili zao. Wamepita changamoto nyingi. Wangekuwa legelege wangeshaachana. Walisimama imara. Walimtanguliza Mungu katika kila jambo, ndoto yao ikatimia.
“Kweli kuna wakati nilishaamua iwe mwisho wa penzi letu. Niliona maudhi yamekuwa mengi. Sikuwa na raha ya mapenzi. Daaah! Kama siamini hivi leo tuko pamoja,” Zena alimwambia Seki.
Maisha ya ndoa yakaendelea, mwaka wa kwanza ukakatika. Ukaanza wa pili hadi wa tatu. Ndoa yao haikuwa imezaa matunda. Licha ya jitihada za makusudi walizozifanya, hawakufanikiwa kupata mtoto. Wakalizungumza suala hilo, wakawaona wataalam, wakagundua kuna tatizo upande wa Zena.
Upande wa pili, mawifi nao wakaanza chokochoko. Wakaanza kumsema Zena kwamba hana faida. Hazai. Wakaanza kumlaumu Seki kwa nini alimuoa mwanamke ambaye hawezi kupata ujauzito. Chokochoko zikawa nyingi, majungu, mafumbo yakawa yanamfikia Zena.
Ikifika wakati akachoka. Akaanza kujuta kuolewa. Ndoa ikawa kama kaa la moto. Akiamka anatukunwa, akilala anatukanwa. Seki naye akajikuta naye anaungana na ndugu zake. Badala ya kumpa faraja mwenzake, yeye akaongoza jahazi la kumsema.
Tabia yake ikabadilika ghafla. Akaanza kusaliti. Anatembea na wanawake wengine, mkewe akihoji, anamwambia anyamaze maana hana kitu ambacho kitampa faraja. Kwamba anatafuta kile ambacho kitampa faraja, watoto.
Anadai amechoka kusemwa na ndugu. Amechoka kuona marafiki zake wakiwa na watoto wao. Yeye kila siku anakuwa peke yake. Anatamani na yeye aitwe baba. Anataka na yeye akitoka ndani ya gari, awapeleke watoto wake bichi, awapeleke kutazama muvi na mambo mengine kama hayo.
Hasira zake anazihamishia kwa kutafuta wanawake wengine. Ikafika wakati mke akaamua kuondoka nyumbani.
Akaamua kurudi kwao. Vitimbi vilimfika shingoni. Hakuwa na jinsi. Akaamua kuondoka kwenda kuitafuta amani.
Marafiki zangu, mfano huo unatufundisha kwamba, pendo la kweli linahitaji kujitoa. Linatanguliwa na ubinadamu. Ustamilivu ndiyo silaha ya mafanikio. Kama mlianza safari miaka mingi, huna sababu ya kuikatisha kwa sababu tu mwenzako ana tatizo fulani.
Binadamu tunaijua leo, kesho yetu hatuijui. Ulimpenda mwenzako, mkakubaliana kuoana, huna budi kukubaliana na kila litakalowatokea. Mungu ndiye anayejua kesho yetu. Mungu hawahi wala hachelewi. Kama kweli mnaamini katika yeye, endeleeni kumuomba hata katika wakati mgumu mnaokutana nao.
Mwambieni yeye ndiye anayejua hatima yenu. Mwombeni awajalie mtoto. Muombeni yeye atende muujiza katika familia yenu. Bila kuchoka, muombeni awape watoto. Mwambieni yeye ndiye anayepanga basi ikimpendeza mpate watoto.
Amani kati yenu isitoweke kwa sababu mmoja ana tatizo. Hamuwezi jua Mungu ana kusudi gani kwenye maisha yenu. Pengine amewapa mtihani huo ili awapime imani yenu. Kama mlivyoomba awajalie ndoa, mmeshafunga basi msibaguane.
Msikubali ndugu waingilie ndoa yenu. Nyinyi ndiyo mlikula kiapo. Nyinyi ndiyo mnajuana vizuri. Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu, hamna sababu ya kumlaumu. Ndugu wakiwasema, zibeni masikio. Msiwasikilize maana watawayumbisha.
Waambieni wawaombee. Na nyinyi wenyewe mkazane kuomba. Hakuna linaloshindikana chini ya jua. Kama Mungu amewajalia safari yenu, amewawezesha kufikia hapo mlipo, mshukuruni kwa hilo. Mwambieni asante kwani amefanya kitu maishani mwenu.
Ametengeneza historia. Msikubali kuipoteza kirahisi. Kila jambo lina wakati wake, endeleeni kuomba na ipo siku Mungu atawajalia, mtapata watoto. Tena hamtaamini. Kila jambo Mungu analifanya kwa sababu, shukuruni kwa kila jambo.
Mapenzi ni uzima na maradhi. Hivyo mnapoamua kuanza safari ya ndoa, hamna budi kuelewa kwamba kuna maradhi. Yawezekana mwenzako akaumwa sana, akapata ajali itakayomfanya akatwe miguu pengine, utafanya nini?
Muwe na moyo wa huruma. Muwe na upendo wa dhati. Uvumilivu utawale na Mungu atawasimamia katika kila jambo!
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!