Wiki iliyokatika alielezea harakati zake za kusaka nafasi katika bendi ya Koffi Olomide. Baada ya kukubaliwa kuingia katika bendi hiyo, Bella alisema haikuwa kazi rahisi kupata nafasi, Koffi alimpiga bechi, lakini hakukata tamaa, alizidi kukomaa.
Bella akaendelea kusimulia kuwa, mambo yalipoanza kukaa poa katika bendi ya Koffi alitokea jamaa mmoja anayeitwa King Dodoo akamshawishi wakaruka mpaka Bongo kwa ajili ya kuanzisha bendi.
Je, ni bendi gani hiyo? Nini kitaendelea kwenye maisha ya Bella? Teremka naye…
BAADA ya kufika Bongo Bella anasema kila kitu kilikuwa kigeni kwake. Kuanzia mazingira mpaka mawasiliano na Wabongo vilikuwa ni kati ya vitu vilivyompa shida sana mwanzoni lakini taratibu akaendelea kuyazoea mazingira na ikamlazimu kufanya juu chini ili ahakikishe anafahamu lugha adhimu ya Kiswahili.
“Kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kumwambia paka ajifunze kuwika kama jogoo, niliuona kuwa ni mzigo mkubwa kwangu, lakini watu wangu wa karibu walinipa moyo juu ya hilo na kwa kuwa nilikuwa naipenda kazi yangu maana ili kuwakosha Wabongo, tulitakiwa kuimba kwa Kiswahili. Ilinilazimu kufanya juu chini niifahamu lugha hiyo,” anasema Bella.
Kuhusu bendi iliyofanya mpaka King Dodoo amfuate Kongo anasema ilikuwa ni Akudo Impact ‘Wazee wa Masauti’, baada ya kujiunga nayo alichaguliwa kuwa rais wa wanamuziki wenzake.
Bella anasema, akiwa na Akudo Impact maisha yalikuwa poa sana, nyimbo za kwanzakwanza kutunga zikiwa Bomoabomoa, Safari Siyo Kifo na Yako Wapi Mapenzi.
“Combination yangu na wasanii wa Akudo kipindi hicho kina Kanal Top, Allen Kabasele, Tarsis Masela na wengine wengi ilikuwa poa sana, lakini kitu kimoja ambacho kilikuwa kinaniumiza kichwa ilikuwa ni kuhakikisha tunafanya kazi na kuvuka mipaka ya Tanzania.
“Hiyo ilikuwa ni kazi ngumu sana, kama unavyofahamu umaarufu wa bendi nyingi hata kama ni za Kikongo lakini zikiwa Bongo zinazofanya muziki wa dansi ni humuhumu Tanzania, zinafahamika sana Morogoro, Mwanza na Tunduma lakini hazivuki mipaka,” anasema Bella na kuongeza kuwa;
Jambo hilo yeye lilikuwa linamuumiza mno kichwa chake. Anasema alikuwa hafurahii hata kidogo kupiga shoo zaidi ya tano kwa muda wa wiki moja kwenye kumbi tofauti jijini.
Anaongeza kuwa alifahamu kwa mwendo huo ilikuwa ni rahisi kuzoeleka machoni kwa wapenzi wa burudani jambo ambalo lingesababisha wao kama wasanii kupoteza mapema mvuto hatimaye kukosa soko na kuua vipaji vyao.
Anaendelea kusema kuwa kwa sababu malengo yake ilikuwa ni kufanya muziki ambao ungemtambulisha sehemu tofauti duniani, ilimlazimu kuwaza kuachana na mambo ya kuajiriwa kwenye bendi na kufanya muziki akiwa ‘solo artist’ ili aweze kutimiza malengo yake na kuitunza thamani yake kama msanii.
Bella anaongeza kuwa mwanzoni kuutekeleza uamuzi huo lilikuwa jambo gumu mno. Ugumu huo anasema ulitokana na kutakiwa kujisimamia mwenyewe kwa kila kitu tofauti na ilivyokuwa kwenye bendi, kila kitu kilikuwa kinasimamiwa na wadhamini waliomwaga pesa za kutosha.
“Suala hili ilinibidi nilifikirie mara mbili, kwa kuwa nilikuwa nimekwisha amua sikuhitaji kurudi nyuma, baada ya kuyapanga mambo yangu freshi niliamua kuachana na Akudo.
“Maneno mengi yalisemwa, waandishi wa habari wa vituo mbalimbali walizungumza na kuandika mambo tofauti kuwa nilikuwa na ugomvi na baadhi ya viongozi wa Akudo lakini ukweli ni kwamba nilitoka katika bendi hiyo nikiwa sina tatizo na mtu yeyote yule,” anasema Bella.
Baada ya kutoka Akudo mwaka 2012, aliamua kupata mapumziko kwa kwenda kumjulia hali mkewe ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Sweden, kwa wakati huo alikuwa na ujauzito mkubwa na alikaribia kujifungua.
Bella anasema akiwa nchini humo jambo ambalo hatalisahau katika maisha yake yote ni namna alivyolazimika kumshuhudia mkewe wakati wa kujifungua. Anadai suala hilo lilikuwa na sababu, alijitahidi ‘kulikacha’ lakini ilimlazimu.
Je, nini kiliendelea? Ni sababu zipi zilimfanya Bella kumshuhudia mkewe akijifungua? Usikose wiki ijayo.