Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.
Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito wa Diego, baadaye wanapanga njama za kutoroka. Arianna anakuwa wa kwanza kuvuka mpaka na kuelekea Kenya lakini akiwa huko, anakutana na janga jingine na kunasa ndani ya kituo cha polisi kinachoungua baada ya kuvamiwa na magaidi wa Kisomali. Anaponea kwenye tundu la sindano na sasa anajiandaa kutoroka lakini kazi haiwi nyepesi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Saa nane za usiku, Diego akiwa amelala kwenye hoteli moja iliyokuwa jirani na Barabara Kuu ya Namanga- Nairobi, alishtuka usingizini baada ya kuanza kusikia milio mingi ya risasi na mabomu ya kutupwa kwa mkono. Kwa kuwa alikuwa anajua jinsi serikali ya Kenya ilivyokuwa inahangaika kupambana na magaidi kutoka Somalia, alijua kwa vyovyote pande hizo mbili zinapambana vikali.
Hakutaka kujishughulisha na chochote kwa sababu aliamini hayamhusu, akajificha chumbani kwake mpaka mapambano yalipotulia, muda ukaendelea kuyoyoma na hatimaye kukapambazuka. Diego aliwahi sana kuamka siku hiyo kwa sababu hakuwa na muda wa kupoteza.
Cha ajabu, alipotoka nje ya gesti aliyofikia, alikuta watu wengi wakiwa nje, tena wakiwa wamejikusanya makundimakundi, huku askari wengi waliovalia sare na wale waliovalia kiraia, wakirandaranda huku na kule, akawa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimetokea.
“Rafiki eti kuna nini kimetokea?”
“Wakora wamevamia police post ya Kianai, wamewakomboa mateka wao na ku-set ablaze (kuchoma) kituo,” alisema mwanaume mmoja kwa lafudhi ya Kikenya, harakaharaka Diego akajichanganya kwenye makundi ya watu ili kupata taarifa za kilichotokea kwa kina.
Alichoambiwa awali ndicho kilichokuwa kimetokea na muda mfupi baadaye, Runinga ya Taifa, KBC ilianza kuonesha picha za tukio hilo, kila mtu akaacha kila alichokuwa anakifanya na kukimbilia kwenye runinga iliyokuwa karibu.
Taarifa ziliendelea kusambaa kwa kasi, kila mtu akawa anazungumzia tukio hilo na kuwalaani vikali magaidi waliohusika. Mpaka inafika saa moja za asubuhi, vikosi vya uokoaji vilikuwa vikiendelea kuhangaika kutoa mabaki ya mahabusu kadhaa walionasa ndani ya kituo hicho kilipochomwa na magaidi hao.
Watu wote ambao ndugu zao walikuwa wakishikiliwa na polisi kwenye kituo hicho siku ya tukio, walitakiwa kujitokeza kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao au kufanyiwa vipimo vya DNA ili kuitambua miili ya ndugu zao kwani kuna wengine ambao walikuwa wameteketea na kubaki mifupa mitupu, jambo lililosababisha hofu kubwa kila sehemu.
“Taarifa tulizozipokea hivi punde, zinaeleza kwamba askari waliobadilisha zamu usiku kabla ya kutokea kwa tukio hilo, walifanikiwa kuondoka na orodha ya majina ya watu waliokuwa wakishikiliwa kwenye kituo hicho cha polisi na yatatajwa hivi punde, usitoke kando ya runinga yako,” mtangazaji mahiri, Waikechi Nyambura wa Runinga ya Taifa alisema katika mwendelezo wa ‘breaking news’, watu wote wakatulia kando ya runinga zao, Diego akiwa miongoni mwao.
Majina yalianza kutajwa ambapo kila aliyekuwa akishikiliwa, alitajwa kwa jina na sehemu anayotokea ambapo wengi walionesha kuwa ni kutoka Somalia ambao duru za kipolisi zilionesha kwamba ndiyo waliokuja kuokolewa na wenzao.
Baada ya kumaliza kuwataja raia hao wa Somalia, mtangazaji alianza kutaja majina ya watu wengine waliokuwa ndani ya kituo hicho, katika kile ambacho Diego alishindwa kukiamini, alisikia jina la Arianna Joseph Ndaki nalo likitajwa.
“Mungu wangu, Arianna? Haiwezekani! Labda ni majina tu yamefanana,” alisema Diego lakini kabla hajamalizia kauli yake, mtangazaji alieleza kwamba Arianna alikuwa ni Mtanzania aliyekuwa akishikiliwa kituoni hapo kwa madai ya kukutwa na silaha.
“Ni yeye! Ni yeye!” alisema Diego kiasi cha kuwafanya watu waliokuwa wameelekeza akili zao kwenye runinga kumgeukia.
“Kwa yeyote anayemfahamu yeyote kati ya waliotajwa, anaombwa kuwasiliana na maafisa wa polisi walio jirani naye,” alihitimisha mtangazaji huyo. Bila kupoteza muda, Diego alitoa simu yake ya mkononi na kumpigia Msuya kwani kwa hali ilivyokuwa, alijua mipango yote imeshavurugika na ili kuendelea kujenga uaminifu kwa Msuya, ilikuwa ni lazima ajikombe na kumwambia alichokigundua.
“Unasema? Haiwezekani! Nasema haiwezekani,” alisema Msuya baada ya kupigiwa simu, na yeye akaonesha kuchanganyikiwa kuliko kawaida.
***
Alfajiri na mapema, Arianna alifanikiwa kuondoka na yule dereva wa bodaboda lakini kwa sababu tayari polisi wengi walishasambaa mitaani, Arianna alimuelekeza kuhakikisha wanapita njia za panya ili isiwe rahisi kushtukiwa na mtu yeyote, jambo ambalo dereva huyo wa bodaboda alilikubali.
Wakaingia njia ya mkato ya kukatika katika mapori ya Taveta, safari iliyokuwa ngumu na ya kuchosha sana. Baada ya kusafiri kwa saa nyingi, wakati mwingine Arianna akilazimika kushuka na kusaidiana na dereva huyo wa bodaboda kuivusha kwenye maeneo korofi, hatimaye walifanikiwa kufika kwenye Mji wa Bisil, uliokuwa mbali sana na pale kulipotokea tukio lile.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, Arianna alimlipa dereva huyo wa bodaboda na kuelekea kwenye kituo cha mabasi ya kuelekea jijini Nairobi, huku akijitahidi sana uso wake usionekane. Hatimaye alifanikiwa kupanda kwenye Basi la Taveta Safari lililokuwa linaondoka dakika kadhaa baadaye kuelekea jijini Nairobi.
Mara kwa mara Arianna alikuwa akigeuka huku na kule kuhakikisha kama hakuna mtu aliyekuwa akimtazama. Kwa bahati nzuri, dakika kadhaa baadaye safari ilianza, akashusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu wake kwani aliamini hatimaye yupo salama.
Hata hivyo, furaha yake ilikuwa ni ya muda mfupi tu kwani kilometa kadhaa mbele, walikutana na kizuizi cha askari, abiria wote wakatakiwa kushuka kwa ajili ya ukaguzi, Arianna akawa anatetemeka mno kwani aliamini hatimaye hawezi tena kuchomoka salama kwenye mikono ya askari hao.
“Jina lako nani?” askari mmoja mwenye mwili mkubwa, mweusi kama mkaa, alimuuliza Arianna kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazetila Ijumaa.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1
eeeh,shigongo unanirusha roho mmmh sijui atafanikiwa afu hii hadithi ungeitengenea filamu!!!!