×

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-3

ILIPOISHIA IJUMAA:

Yule mzungu alikuwa akiendelea kuogelea tu na mimi nikimfuatia nyuma. Ghafla nikaona tumetokea kwenye kisiwa kizuri kilichokuwa na minazi mingi.

Tulipofika kwenye ufukwe wa kisiwa hicho tuliona jumba kubwa likiwa mbele yetu. Lilikuwa jumba zuri lililokuwa likimeremeta!

Yule mzungu akaniambia pale ndiyo nyumbani kwake. Akanikaribisha, tukaingia ndani.

Humo ndani tulitokea kwenye chumba kipana kilichokuwa na kitanda na kabati. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa godoro la kitanda hicho pamoja na mto wake zilikuwa ni noti tupu!

Yule mzungu akajilaza kwenye lile godoro la noti. Mimi nikawa nazishangaa zile noti jinsi zilivyokuwa nyingi.

Nikashikwa na tamaa ya kutaka kuchukua zile noti. Hapohapo nikaona kama kivuli cha mtu kwenye dirisha. Nilipotazama vizuri nikamuona marehemu mama yangu amesimama nje ya dirisha akinifanyia ishara nitoke mle chumbani.

SASA ENDELEA…

Lakini alinifanyia ishara hiyo kwa siri na kwa tahadhari ili yule mzungu asimuone.

Sasa mimi sikuelewa kwamba mama alinifanyia ishara ile kwa ajili ya kumkimbia yule mzungu au alitaka nitoke nionane naye kwa vile hatukuwa tumeonana kwa miaka mingi.

Kwa akili yangu nikachukulia kwamba mama alitaka nitoke nikasalimiane naye. Kwa vile dukuduku la kumuona mama yangu lilikuwa limeshanishika nikageuka haraka ili nitoke mle chumbani.

Yule mzungu akamuona mama akichungulia kwenye dirisha, akauliza.

“Nani yule?”

Wakati anauliza hivyo alikuwa akishuka kwenye kitanda ili aende pale dirishani.

Na mimi nikapata nafasi ya kuchukua burungutu la noti kutoka kwenye godoro na kutoka nalo mbio. Huku nyuma nikasikia mzungu akiniita.

“Wewe Enjo hebu rudi hapa!”

Ile sauti ya yule mzungu ndiyo iliyoniamsha usingizini. Nikafumbua macho. Kwa vile niliamka wakati natoka mbio, nilijikuta nikihema huku moyo ukinienda mbio.

Mkono wangu wa kulia ulikuwa kama ulioshika lile burungutu nililokuwa nakimbia nalo. Nikahisi niliamka nikiwa na noti hizo mkononi. Kwa haraka nikayapeleka macho yangu kuutazama mkono wangu.

Sikuona chochote. Mkono huo ulikuwa mtupu!

Nikajiinua na kuketi kitandani huku nikijiuliza kwa nini niliota ndoto ile?

Nikawasha taa ya mchagoni mwa kitanda nikatulia hapo kitandani na kuwaza.

“Kuna uwezekano mkubwa yule mzungu akawa ni tajiri, ndiyo maana nimemuota amelalia godoro la noti,” nikajiambia.

Niliendelea kujiambia kuwa kama nitashikamana naye anaweza kunitajirisha. Wazungu hawana tabia ya ugumu wa pesa.

Asubuhi kulipokucha niliamkia kufua nguo zangu nilizozitumia kwa wiki ile. Nilipomaliza niliinjika chai. Kwa kawaida napendelea kunywa chai ya rangi. Halafu nakunywa maziwa peke yake.

Nilikuwa sipendelei kunywa chai ya maziwa. Baada ya chai kuwa tayari niliimimina kwenye chupa nikaenda kuoga. Baada ya kuoga na kuvaa, nilikwenda mezani, nikapaka siagi slesi za mkate na kujinywea chai yangu.

Wakati nakunywa chai, simu yangu ikaita. Nilikuwa nimemsahau yule mzungu. Alipoona saa tano ilikuwa imefika alisubiri zipite dakika mbili ndipo akanipigia.

Nilipotazama simu, nikaona ni yeye aliyekuwa akinipigia. Ule msemo wa kuwa na ahadi ya kizungu ndipo nilipouthibitisha.

Kabla ya kuipokea simu hiyo nilijiuliza nitamwambia nini mzungu huyo kwa kutotimiza ahadi yangu ya kumpigia simu ikifika saa tano? Sikupata jibu. Nikaacha ile simu iite hadi ikakata yenyewe. Ndipo na mimi nikapiga.

Mzungu akaipokea mara moja.

“Hello Enjo!” akaniita.

“Hello Mr Smith, mambo vipi?”

“Kama kawa, kama dawa!” mzungu akanijibu.

Nikaangua kicheko. Kilichonichekesha hasa si vile alivyotumia maneno hayo ya mitaani bali alikuwa akitamka maneno hayo kwa lafudhi ya Kiingereza.

“Unacheka nini?” akaniuliza.

“Nimefurahi kwa jinsi ulivyonijibu.”

“Nimekosea?”

“Hapana, umepatia sana.”

“Nimeona kimya mpaka nimepiga mimi.”

“Ndiyo. Nilikuwa bafuni wakati unanipigia,” nikatoa uongo.

“Nilifikiri umesahau.”

“Hapana, sikusahau. Nilikuwa nikupigie nikitoka bafuni.”

Mzungu akanyamaza kimya kidogo. Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa kabla ya sauti yake kusikika tena.

“Umeshafikiria tukutane wapi?” akaniuliza.

Nikamtajia hoteli moja ya palepale Sinza lakini ilikuwa mbali kidogo na nyumba ninayoishi.

“Unaweza kufika?” nikamuuliza.

“Ninaweza,” akaniambia.

Akanyamaza kidogo kisha akaniuliza.

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Simulizi yangu ya ‘NILIVYOGEUZWA PAKA’ sasa imetoka kwenye kitabu. Kwa mawasiliano ya kupata kitabu hicho piga namba 0712 777737. Kwa wasomaji wa Tanga wapige namba 0655 340572

Leave a Comment