Mashabiki wa timu ya Yanga.
Nicodemus Jonas, Dar es Salaam
KWA mara nyingine, Yanga wiki iliyopita ilifanikiwa kupenya hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0.
Sasa inakutana na APR ya Rwanda kwenye hatua ya kwanza, katika safari yao ya kufuta rekodi mbaya ya kuishia hatua za mwanzo kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika. Yanga wanaanzia ugenini Machi 12, mwaka huu kabla ya kurudiana pale Taifa wiki moja baadaye.
Wakiendelea na mazoezi.
Kwa takwimu tangu msimu wa 2006-07, zinaonyesha itakuwa mara ya kwanza timu hizi kukutana kwenye michuano hii, hata hivyo, kwa dalili zilivyo, Yanga ina nafasi ya kusonga mbele na uwezekano wa asilimia 90, watakutana na Wamisri, Al Ahly watakaocheza na FC Libolo ya Angola.
Rekodi za Yanga kimataifa
Tangu 2006, Yanga imecheza mechi 16 na kufunga jumla ya mabao 33 na kuruhusu mabao 14. Katika mechi hizo, nane ilikuwa Taifa ambapo imeshinda mechi nne, sare mbili na kupoteza mbili, wakati nane nyingine ilikuwa ugenini ambapo imeshinda mechi tatu na zilizobaki ni vichapo tu.
TAKWIMU KWA WAARABU
Yanga haijawahi kuitoa timu yoyote ya Kiarabu katika awamu nne ilizocheza dhidi yao katika kipindi hicho.
Ilitolewa nje na ES Tunis ya Tunisia Aprili 2007. Mechi ya awali, Yanga ilifungwa 3-0 ugenini, kisha kusuluhu hapa nyumbani. 2009 ilikutana na Al Ahly ya Misri ambapo ilifungwa nje-ndani, wakianzia ugenini kwa kichapo cha mabao 3-0 kabla ya kufungwa Taifa 1-0.
2012 wakakutana na Zamalek ya Misri ambayo mchezo wa awali pale Taifa timu hizo zilifungana 1-1, kabla ya kuchapwa bao 1-0 ugenini, kisha mwaka 2014 kutolewa kwa mikwaju ya penalti na Al Ahly ambapo Yanga walishinda pale Taifa 1-0 lakini wakalala idadi hiyo ugenini na hatua ya matuta ikaamua mbabe, wakatupwa nje.
Rekodi zinaonyesha, nje ya Waarabu, Yanga si ya kuchezea na imekuwa ikizitesa timu za mataifa mengine. Kwenye awamu nne, sawa na mechi nane ilizocheza, Yanga imeshinda mechi sita na kufungwa mbili tu. Imetolewa mara moja tu na Lupopo ya DR Congo, iliyowafunga nje-ndani mwaka 2010.
Ilifungwa Taifa mabao 3-2 na ugenini ikalala kwa bao 1-0.
Mwaka 2009, ilifuzu dhidi ya Etoile d’Or ya Comoro kwa jumla ya mabao 14-1, kabla ya kuwaonea tena Wacomoro wengine, Komorozine mwaka 2014 kwa jumla ya mabao 12-2 na juzi dhidi ya Wamauritius, Cercle de Joachim kwa mabao 3-0.
Hii inaonyesha kuwa Yanga wana nafasi kubwa ya kuitupa nje APR, lakini pia wanaweza kuitupa nje Al Ahly kwa kuwa kadiri siku zinavyozidi kusogea Waarabu hao wanapata ugumu kila wanapovaana na Yanga.
Kwa nini Yanga itapenya mbele ya APR?
Tofauti na misimu mingine, safari hii imeonekana kudhamiria kabisa kufika mbali kwenye michuano hii. Hii inatokana na idadi kubwa ya wachezaji wa kimataifa wenye msaada mkubwa kikosini baada ya kuongezewa idadi kutoka watano hadi saba, wachezaji kama Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima wana kiu ya mafanikio huku wakiwa na uwezo wa juu zaidi wa kuisaidia timu hiyo.
Pili, hali shwari ya kiuchumi, tofauti na miaka mingine ambako ilikuwa inalia njaa, Yanga ya sasa hakuna tena vilio vya njaa kwa wachezaji wala benchi la ufundi, hali ambayo inawafanya wafanye kazi kwa utulivu mkubwa. Hii inakwenda sanjari na menejimenti nzuri kutoa motisha kwa wachezaji ambako hupewa hela nzuri wanaposhinda mechi kubwa kama hizi.
Uzoefu wa kocha Hans van Der Pluijm. Kadiri anavyozidi kuwa na kikosi ndivyo anavyopata uzoefu wa mazingira sahihi ya soka la Tanzania na michuano hii kwa ujumla kwani ni msimu wake wa tatu sasa hali ambayo inaonyesha hawezi kuwa na sababu kuendelea kuonewa.
Uzoefu wa wachezaji, kikosi kizima cha Yanga kinachoanza kina wachezaji wazoefu, kuanzia kwa makipa wake, hadi kwa washambuliaji, wote ni wazoefu wa michuano hii mikubwa.