Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Said Ally, Dar es Salaam
LICHA ya kuwa kikosi chake kinaibuka na ushindi katika michezo yake mbalimbali, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm ameibuka na kutamka kuwa haridhishwi na aina ya kiwango kinachoonyeshwa na washambuliaji wa klabu hiyo kwa kushindwa kuwa makini katika kumalizia nafasi ambazo wamekuwa wakizitengeneza na kujikuta wakiambulia mabao machache.
Pluijm amekiongoza kikosi chake kutinga hatua ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuifunga Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, baada ya ushindi wa mabao 2-0 nyumbani na ule wa 1-0 ugenini ambapo sasa wanatarajia kuvaana na APR ya Rwanda katika hatua hiyo.
Akizungumza na Champioini Jumatano, Pluijm alisema licha ya kikosi chake kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo sambamba na mingine lakini wachezaji wake wamekuwa wakifanya uzembe wa kushindwa kufunga mabao mengi licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.
“Hatukuwa makini kabisa katika mchezo ule dhidi ya Cercle de Joachim kwa upande wetu siyo kwa kucheza vibaya hapana ila tumepoteza nafasi nyingi za kufunga ukilinganisha na idadi ya mabao ambayo tumeyapata ambapo kama tungeongeza umakini kidogo hasa kwa washambuliaji, naamini mambo yangekuwa tofauti na matokeo yalivyokuwa.
“Sijui hata wapi tatizo hili linaibuka kwani mara nyingi nimekuwa nikiwapa mbinu pamoja na kuwafundisha katika mazoezi jinsi ya kumalizia mipira kama ile wanayopata nje ya eneo la wapinzani lakini naona bado tatizo linaendelea.
Lakini nitalifanyia kazi tena kabla ya kwenda katika raundi inayofuata kwani huko ndipo najua kuna ugumu zaidi na kama tukishindwa kulitatua kwa sasa linaweza kutukosti kwa siku za baadaye,” alisema Pluijm.
Washambuliaji wa Yanga ambao wamekuwa wakionyesha kiwango cha juu msimu huu ni pamoja na Amissi Tambwe, Donaldo Ngoma na Malimi Busungu.