Mwandishi Wetu, Morogoro
KIPA Juma Kaseja hatoichezea Mbeya City dhidi ya Simba, kesho Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuongezewa muda zaidi wa kushughulikia mambo yake ya kifamilia.
Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri amethibitisha kuwa Kaseja hatokuwa sehemu ya wachezaji wake watakaocheza dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Phiri alisema mwanzo ilikuwa waungane na Kaseja, jana asubuhi kwenye kambi ya muda hapa mkoani Morogoro lakini amemuongezea kipa huyo muda zaidi wa kuwa karibu na familia yake ili kushughulikia masuala kadhaa ya kifamilia.
“Wakati anaondoka siku tano zilizopita tulikubaliana aungane nasi leo (jana), lakini nilipozungumza naye asubuhi (jana) kuna mambo muhimu ya kifamilia amenieleza hivyo basi nimemuongezea siku za kubaki nyumbani kushughulikia mambo ya kifamilia.
“Ni imani yangu ataungana na kikosi mara tu tutakaporejea Mbeya kujiandaa na mchezo dhidi ya Stand United,” alisema Phiri.
Kaseja aliondoka Mbeya baada ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Prisons baada ya mkewe kujifungua watoto mapacha.