×

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-20

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
Kule sebuleni, Nancy alipoona Neema anachelewa kurudi na yeye anataka kuondoka, alisimama kumfuata chumbani kwa Aisha…
“Wala hatuna ahadi yoyote ile,” alikanusha Neema…
TAMBAA NAYO SASA…

Nancy alisimama mlangoni akisikiliza baada ya kumsikia Neema akisema ‘wala hatuna ahadi yoyote ile.’
“Sasa ndiyo kuvaa gani kule Neema? Kigauni kama changudoa bwana. Wanawake wengine wamepinda kwelikweli,” aligandamiza Aisha…

“Mimi mwenyewe nilitamani kumwambia moja kwa moja kwamba wewe ni matroni wangu lakini hiki kivazi chako cha leo loo! Nikahisi anaweza kuona namuingilia uhuru wake,” alisema Neema, wakacheka kwa chinichini.
“Sema kwa kuwa ni wewe, ningekuwa mimi wala nisingemkawiza, ningemchana laivu ili siku nyingine asirudie uvaaji wake wa kichangudoa,” Asha aliongeza, wakacheka kwa chinichini kama awali.

Nancy alipojiridhisha kwamba wawili hao walikuwa wakimsema yeye, aliondoka, akafika sebuleni akamwambia Bony…
“Mimi nakwenda, nitakutafuta…”
“Kha! Kwani Neema yuko wapi, si ulimfuata huko?”
“Neema amepanda bei siku hizi, ananisengenya na huyo mke mwenzake.”
“Kweli?” alihamaki Bony na kusimama lakini Nancy alishafika getini na kuondoka zake…
“Ngo ngo ngo,” Bony aligonga mlango wa chumbani kwa Aisha…
“Bee,” aliitika Neema na kufungua mlango…
“Vipi darling?”
“Hebu wote njooni sebuleni.”
“He! Kuna nini sweet?” aliuliza Neema akiwa ameanza kutoka, Aisha akamfuatia.
***
Nancy akiwa kwenye Bajaj alijifikiria jambo moja kwamba, Neema aliyeonesha nia ya kumpigania akiwa anaishi na mwizi wa mume wake bila kujijua, ndiye aliyeongoza kumsema vibaya…
“Yule dawa yake moja tu, mumewe nimweke mikononi mwangu. Nimfanyie kila kitu kuhakikisha anamsahau mke wake,” aliwaza moyoni Nancy.
***
Neema alipokuta Nancy hayupo, kwanza alijua amekwenda chooni…
“Sweet Nancy yuko wapi?” aliuliza Neema akizungusha kichwa…
“Niwaulize nyie,” alijibu Bony…
“Sisi kivipi sasa?” aliuliza Aisha.

“Nancy alisema anakwenda kuna sehemu anachelewa, akasimama kumfuata huko ndani. Alipotoka akasema anaondoka, nikajua mmeshaagana naye…”
Kabla Bony hajamaliza kusema, Neema na Aisha wakaangaliana kwa macho ya mshangao, kichwani Neema akayarejea yale maneno waliyokuwa wakiyaongea chumbani…
“Mimi mwenyewe nilitamani kumwambia moja kwa moja kwamba wewe ni matroni wangu lakini hiki kivazi chako cha leo loo! Nikahisi anaweza kuona namuingilia uhuru wake.”
Aisha naye akawaza alivyoongea yeye…
“Sasa ndiyo kuvaa gani kule Neema? Kigauni kama changudoa bwana. Wanawake wengine wamepinda kwelikweli.”
“…sema kwa kuwa ni wewe, ningekuwa mimi wala nisingemkawiza, ningemchana laivu ili siku nyingine asirudie uvaaji wake wa kichangudoa.”
Bony akaendelea…

“…nikamuuliza Neema yuko wapi? Maana nilijua si rahisi aondoke bila wewe kumsindikiza mgeni wako, akasema Neema amepanda bei siku hizi, ananisengenya na huyo mke mwenzake.”
Neema alijishika kichwani akainama…
“Mungu wangu…Mungu wangu…atakuwa amesikia kila kitu,” alisema Neema…
“Kwani hakuingia chumbani?” aliuliza Bony…
“Hajaingia shemeji. Halafu sisi siyo kwamba tulikuwa tunamsema vibaya bali ni kile kivazi chake,” alisema Aisha kwa sauti iliyotawaliwa na aibu…
“Sasa nyie mtamsemaje mgeni ambaye amekuja ndani kwenu, hamuoni kama kitendo mlichokifanya siyo kizuri?” alikuja juu Bony…

“Kweli nimemkosea sana matroni wangu, itabidi nimpigie simu kumwomba msamaha,” alisema Neema.
“Ukifanya hivyo itakuwa vizuri maana alivyoondoka ameonesha kama kuna jambo limemkwaza,” Bony alimwambia Neema.
“Kweli kabisa kwa ninavyomfahamu Nancy asingeondoka bila hata ya kuniaga, moja kwa moja atakuwa amesikia tulivyokuwa tukimsema kuhusu alivyovaa kachukia,” Neema alimwambia mumewe.

***
Nancy alipofika nyumbani kwake huku akiwa na hasira kufuatia kitendo cha Neema na Aisha kumsema vibaya, alifungua jokofu na kutoa wine akamimina kwenye glasi na kukata mafunda mawili kisha akaiweka glasi mezani.
Baada ya kufanya hivyo aliamua kumtumia meseji Bony. Alianza…
“Baby.”
Wakati meseji hiyo inaingia, Bony alishamaliza kusema na wapenzi wake hao kwa hiyo akaanza kuchati na Nancy…
“Niambie sweeet…”
“Hapo hatukumaliza mchezo sawasawa, mimi bado kabisaaa. Plz, njoo nyumbani sasa hivi ufurahie dunia nyingine kutoka kwa Nancy na ndiyo utajua kumbe umekuwa ukikosa raha kwa muda mrefu.”

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumatatu ijayo.

Leave a Comment