×

Madenti Waandamana Kupinga Udhalilishaji

Na Stephano Mango RISASI mchanganyiko

SONGEA: Wanafunzi 106 wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wameandamana kwenda kumwona mkuu wa mkoa Said Mwambungu kumpelekea malalamiko dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa na mmoja wa walimu wa shule hiyo (jina lake linahifadhiwa).
Mwalimu huyo anadaiwa kutoa vitisho na lugha za matusi kwa wanafunzi, kuchapa viboko visivyo na idadi,kuingia kwenye bweni la wanafunzi wa kike nyakati za usiku bila kuongozana na matroni na vitendo vingine vya kidhalilishaji.

Wanafunzi hao waliandamana umbali wa zaidi ya kilometa 16 kiongozi huyo wa serikali, lakini kabla ya kumfikia, askari polisi kutoka Namtumbo kuwazuia wasiendelee na maandamano.

Wanafunzi hao walikutwa kijiji cha Mlete kilicho nje kidogo ya manispaa ya Songea ambapo askari polisi waliwaamuru wasimame polisi waliwataka waeleze sababu za kufanya maandamano bila kibali, ndipo walipodai kuwa walishatoa malalamiko yao kwa mkuu wa shule, lakini hawajawahi kusikilizwa.

Muda mfupi baadae alifika katibu tawala wa Namtumbo, Alkwine Ndimbo na kusikiliza malalamiko yao, walipotamka kuwa hawamtaki mwalimu huyo, anayedaiwa pamoja na mambo mengine, amekuwa akitaja majina ya wanafunzi wanaohisiwa kuathirika na ugonjwa wa Ukimwi.

Walisisitiza pia shule yao kukosa miundombinu mizuri, wakidai vyoo ni vibovu havifai kutumika, baadhi ya madarasa hayana sakafu pamoja na kwamba wanalazimika kwenda umbali mrefu kufuata maji.Baada ya viongozi hao kusikiliza malalamiko ya wanafunzi, waliwataka warudi shuleni ili wakatoe maamuzi mbele ya wanafunzi wote pamoja na walimu jambo ambalo wanafunzi walikubali na kusitisha maandamano.

Kwa upande wake Afisa elimu wa sekondari wilaya ya Namtumbo, Patrick Atanasi ambaye aliyefika kwa kuchelewa wakati tayari katibu tawala wa wilaya hiyo Ndimbo ameshakubaliana na wanafunzi warudi shuleni, alisema kitendo walichofanya wanafunzi cha kuandamana ni kosa kubwa na utovu wa nidhamu na inapaswa kilaaniwe.

Leave a Comment