Ilipoishia wiki iliyopita
Katika watu waliokuwa ndani ya baa hiyo, akina Bata hawakuweza hata kumhisi kijana anayemsubiri Mwani, na walipomuona akija kwa madaha, wakajifanya kutokuwa na habari naye. Mtu mgeni asingeweza kujua kama wanafahamiana. Sasa endelea…
Sule alimlaki Mwani kwa bashasha, kama ambavyo mwanaume yeyote aliyempata mwanamke aliyemtamani kwa muda mrefu. Alisimama na kufungua mikono na kumkumbatia. Kwa mara ya kwanza, akahisi joto la aina yake, pale matiti yaliyojaa ya Mwani yalipogusa kifua chake kikakamavu. Mapigo ya moyo wa Sule yalisimama kwa muda, maana ulikuwa ni wakati ambao hakuwahi kuwa nao kabla katika maisha yake ya kimapenzi.
Mwani aliwaona akina Bata, lakini naye alijifanya kutowatambua, ingawa walipeana ishara walizozijua wenyewe kuwa walikuwa pale pamoja. Kwa Sule, kichwa chake hakikuwa na kitu kingine zaidi ya mawazo ya jinsi gani ataifurahia siku hiyo akiwa na msichana aliyempenda kwa dhati ya moyo wake.
Sule alikuwa akinywa bia, lakini Mwani hakuwa mpenzi wa kilevi, yeye alibadilisha juisi moja baada ya nyingine na hadi ilipofika saa tatu kasoro usiku, boksi la juisi ya Apple lilikuwa mezani kwake!
“Mwani nafikiri huu ni muda muafaka tuondoke twende sehemu nyingine, au unasemaje?” Sule alimwambia msichana aliyekuwa mbele yake, akiwa hana uhakika na jibu atakalopewa.
“Wapi tena saa hizi jamani Sule, mimi nadhani kwa leo siku yetu iishie hapa, then mambo mengine tuangalia ustaarabu kuanzia kesho, sawa?” Mwani alijitetea, akifahamu fika ni jinsi gani kijana aliyekuwa mbele yake alivyokuwa akimtamani.
“Ni sawa usemayo, lakini siku zote mimi huamini fursa inapojitokeza mara ya kwanza, nimejifunza madhara ya kuremba, tafadhali,” Sule alijieleza kwa sauti yenye kubembeleza.
“Kwani unataka twende wapi usiku huu wakati wewe unajua kabisa kuwa mimi ni mtoto wa mama, kwanza nimeshachelewa na nikiendelea, itasababisha nifungiwe ndani kabisa nisiwe natoka, bora ujikaze leo ili niwe napata muda mapema mchana tunamaliza mambo yetu,” Mwani alimweleza mwenzake, ambaye alitingisha kichwa kuelewa.
“Sasa sikia, kesho kuna sherehe flani ndogo inafanywa na mabosi wangu pale kwao, tunaweza kukutana mapema sehemu au utakuja pale?” Sule alimuuliza, swali ambalo lilimfanya Mwani alipukwe na moyo wake, lakini hakuonyesha, ilikuwa ni fursa nzuri kwa lengo lao kutimia.
“Mimi nadhani tuwasiliane kesho mchana, tutajua la kufanya,” Mwani alimjibu Sule, kisha wote wakainuka na kuanza kutembea taratibu hadi walipozifikia teksi zilizokuwa zimeegeshwa.
**
Mwani, Bata, Jully na Ellina walikuwa wamekaa kwenye meza moja pale kwenye mgahawa wa akina Bata, wakiwa kama wateja wengine, huku vijana wawili walioajiriwa wakitoa huduma kwa wote waliokuwa wakifika hapo.
“Kwa hiyo ndiyo hivyo jamani, jamaa kasema leo jioni kuna sherehe pale kwa mabosi wake, anataka tutoke, tunafanyaje?” Mwani aliwaambia wenzake baada ya kuwasimulia kwa kirefu mambo yote yaliyotokea tangu jana yake.
“Na kama nimekuelewa fresh, unasema ile chemba iko vizuri na watu wanaweza kuingia pasipo tatizo?” Bata alimuuliza Mwani, ambaye alitingisha kichwa kumaanisha alichokuwa akizungumza.
Baada ya kubadilishana maneno mawili matatu, wakakubaliana kwamba Mwani asikubali kuondoka na jamaa kwenda sehemu yoyote, bali atake kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa ajili ya sherehe na waondoke baadaye shughuli ikiisha. Lengo kubwa ilikuwa ni kufanya uchunguzi wa jinsi gani nyumba hiyo ilivyo, usalama wake na kama wanaweza kuwa salama wakiingia kupitia chemba hiyo.
Baada ya kumaliza kupanga mikakati yao, Mwani alimpigia simu Sule na kumweleza kuwa alikuwa tayari kushiriki naye kwenye shughuli nyumbani kwa mabosi wake na kwamba wangeweza kuondoka kuelekea sehemu nyingine baada ya sherehe kumalizika. Ilikuwa moja kati ya simu chache zilizowahi kumsisimua Sule katika maisha yake.
Bata alikuwa mitaa ya Gerezani, Kariakoo jijini Dar es Salaam nyumbani kwa kijana mmoja aliyeogopeka sana miongoni mwa watoto wa mjini, Gasto. Alipelekwa hapo na rafiki yake baada ya kumweleza lengo lake la kutaka kulipa kisasi, kwa mauaji ambayo hataki kumpa kazi hiyo mtu mwingine, lakini hataki atambulike.Itaendelea wiki ijayo