WAKAZI wa soko la Mabibo jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita walijikuta wakifurahia na kuchangamkia vilivyo Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba inayoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers Ltd baada ya kujitokeza kwa wingi kununua magazeti na kujaza kuponi ili kushiriki shindano hilo.
Maofisa wa Global Publishers walifika katika soko hilo la Mabibo ambapo wafanyabiashara na wanunuzi wakiwemo wabeba mizigo walijitokeza na kununua magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo, kisha kujaza kuponi huku wakijipatia zawadi za kofia zenye nembo ya Shinda Nyumba zilizokuwa zikitolewa.
Akizungumza na wakazi wa maeneo hayo Ofisa Masoko wa Global Publishers, Yohana Mkanda alisema: “Wanachotakiwa kufanya wafanyabiashara wa soko hilo ni kununua magazeti ya Global ambayo ni Uwazi, Championi, Risasi Mchanganyiko, Ijumaa Wikienda, Amani, Risasi Jumamosi na Ijumaa na kujaza kuponi zinazopatikana ndani ya magazeti hayo ambayo huuzwa kwa shilingi mia tano na msomaji anaweza kujishindia nyumba ya kisasa, kila anayejaza kuponi nyingi anajiongezea nafasi ya kujishindia nyumba na zawadi nyingine,” alisema Mkanda.
Naye Ofisa Masoko wa Kampuni ya Shinyanga Emporium, Herman Bernad ambao ni wadhamini wa Bahati Nasibu hiyo na ni wauzaji wa pikipiki aina ya Sky Mark na Bajaj za Piaggio, alisema kuwa pikipiki bado zipo nyingi licha ya mwezi uliopita kupatikana mshindi mmoja.
Mshindi huyo Lucy Swai wa Kibaha alijishindia pikipiki aina ya SkyMark baada ya kushinda katika droo ndogo ya pili na Bernad akasisitiza; “Pikipiki hizo ni bora zaidi kwa matumizi ya familia na hata kwa shughuli za biashara kama bodaboda.”