ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Maneno hayo kwangu yalikuwa mageni sana, kweli moyoni nikaanza kuona ugumu wa kazi ya ubaharia.
“Bwana Tolu,” aliniita Nurdin.
“Naam,” niliitika nikijua anataka kuniambia kitu kingine.
ENDELEA MWENYEWE SASA:
“
Nchi kavu hakuna maajabu huku baharini ndiyo funga kazi. Kuna sehemu tutapita, utaona nyumba zimejengwa juu ya bahari, watu wanaishi na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Wakati tunapita eneo hilo, wakituona watatupungia mikono.
“Hata tukipita na giza, wao wapo kwenye mwanga kwani kuna nguzo za taa kila kona. Ni usiku lakini pale unaweza kusema ni mchana.
“Eneo tunalopita sisi mwanga wa taa zao utatufikia, ni jambo la kushangaza sana kuona watu wanatembea na kufanya shughuli zao juu ya maji,” Nurdin aliniambia huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa huruma.
Nilishangaa sana. Meli iliendelea kutembea, ikafika mahali ikawa nzito kama inayotaka kusimama, nikamuuliza Nurdin kama meli ni mbovu au nini? Akasema si mbovu bali tumefika eneo ambalo kama kuna mlima.
“Kwani baharini kuna milima Nurdin?”
“Kuna milima na mabonde bwana Tolu lakini maji yamefunika isionekane. Kukutana na hali hii ni mambo ya maajabu ya Mungu. Sasa sikia hapo, tumepita mlima na tuko kwenye tambarare,” Nurdin aliniambia.
Kulipita ukimya kidogo, meli iliendelea kuchanja maji, hatimaye tulifika Sumatra.
Pale Sumatra tulikaa kwa wiki moja tukishusha mzigo kwenye meli lakini nilijiwa na wazo.
Nilimwambia Nurdin kwamba, moyo wangu unaniambia nisiendelee na kazi ile ya ubaharia, nifanye mpango nirudi nyumbani Tanzania kwa usafiri wa ndege.
Hata hivyo, Nurdin alinikatalia, akasema: “Bwana Tolu, hayo yote unayoyawaza wewe hata mimi nilikutana nayo, lakini nakuapia, ni hali ya kawaida kumtokea mtu. Nakuomba usijaribu kuamua hivyo.”
Nilimwelewa Nurdin, lakini moyo wangu ulikuwa mzito sana kuendelea na kazi ya ubaharia. Kusema ukweli niliyoyaona baharini kwa safari hiyo moja tu, yalitosha kuamua kuachana na kazi ile.
“Oke, nimekuelewa Nurdin, acha nimwombe Mungu.”
Siku ya mwisho ya kulalia kuondoka, maana baada ya kupakua mzigo wote, tulipakia mwingine, makontena yenye nguo mpya, suruali, mashati, viatu vya kike na vya kiume, nguo za ndani na vitu vingine vidogovidogo, Nurdin aliitwa na nahodha wetu, anaitwa Saudi, walizungumza kwa kirefu nikiwa sijui wanazungumza nini. Walipomaliza, Nurdin aliniita kando ya meli, akaniambia:
“Bwana Tolu, uliona nilikuwa nazungumza na nahodha?” nilimjibu ndiyo.
“Ameniambia kuna mtu atakuja, tutaondoka naye kwenda mahali hapahapa mjini, atakutengeneza kwa ajili ya kukukinga na mabaya ya baharini, maana ameniuliza kama ulipokuwa unataka kuanza kazi hii ulijikinga, nikamwambia hapana.
“Kwa hiyo huyo mtu atakuja hapa bandarini, tutaondoka naye. Nahodha ana ndugu Indonesia kwa hiyo ni mwenyeji wa maeneo haya.”
Nilimkubalia Nurdin, tukamsubiri mtu huyo ambaye alitokea kama saa mbili asubuhi. Alitupeleka kwa mzee mmoja anaitwa Jamal Jamalali ni mtaalam wa mambo ya ulimwengu wa giza. Nasema ulimwengu wa giza kwa sababu ni mganga wa kienyeji.
Tulikuta watu wengi nyumbani kwake, lakini tulipoingia sisi, alipopewa habari na wasaidizi wake alituita, tukaingia.
Mazungumzo yangu na yeye kwa lugha ya Kiingereza yalikuwa hivi baada ya kutambulishwa jina langu na madhumuni ya kwenda pale :
“Una mke?”
“Sina.”
“Umewahi kukutana kimwili na mwanamke yeyote wakati wa jua la mchana?”
Nilikumbukakumbuka na kubaini nimewahi mara kadhaa, nikamkubalia.
“Ndiyo nimewahi.”
“Mara ngapi au hukumbuki?”
“Sikumbuki, lakini zaidi ya mara moja.”
Palepale alichukua karatasi jeupe, akaliviringisha kwenye mkono wake kisha akalitumbukiza kwenye maji yenye rangi ya njano, alipolitoa akaniambia nisimame, nikasimama. Akalikamua lile karatasi ndani ya kinywa changu, yale maji yakatoka, akaniambia:
“Meza bila kujali…meza bila kujali.”
Nilimeza bila kujali, maji yale yalikuwa na ladha ya vitunguu swaumu.
“Usioge mpaka siku tatu na maji ya kwanza kuoga yawe ya baharini,” alisema.
Lakini kwa sababu tunaondoka kesho yake nilimwambia itakuaje, Nurdin akamjibia.
“Tutachota maji ya bahari hakuna shaka.”
Nilimwangalia Nurdin kama niliyetaka kumuuliza itawezekanaje?
Yule mganga akadakia yeye: “Kaa chini nikuelekeze namna ya kuoga hayo maji ya baharini na siyo kama alivyosema huyu mwenzako.”
Je, unajua kilichoendelea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Amani, Alhamisi ijayo.