×

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-32

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Mimi nafikiri anaweza kuwa ni kichaa. Mtu mzima na akili zake hawezi kufanya hivyo,” nikamwambia huku nikitazama pembeni.
“Kama ni kichaa aliingiaje kwenye geti mahali ambapo palikuwa na askari na alitoka vipi bila kuonekana?”

“Mimi nadhani hawa askari wanalala usiku.”
“Ndiyo nataka kupata taarifa yao ili niweze kuchukua hatua.”
Pakapita kimya kifupi kabla ya waziri huyo kuniambia.
SASA ENDELEA…

“Nilikuita kukupa pole tu baada ya kusikia kuwa gari lako liliibwa usiku.”
“Asante nashukuru sana mheshimiwa.”
“Basi unaweza kwenda kuendelea na kazi.”
“Asante.”

Nikanyanyuka haraka na kutoka ofisini kwake. Wakati natoka nilikuwa nikijiambia, ofisi ile ya waziri mkuu itakuwa yangu muda si mrefu.

Nilipoingia ofisini mle nilikuwa na hofu na wasiwasi lakini nilitoka nikiwa roho nyeupe. Awali nilidhani kuwa waziri alikuwa akiniitia yale masuala ya uchawi. Nilihisi kwamba niligunduliwa na polisi waliomwambia kuwa mimi ndiye niliyemuwekea kinyesi mlangoni.

Kumbe mheshimiwa aliniitia suala jingine kabisa la kunipa pole.
Kweli uchawi wa kwetu Mbogwe si mchezo, nikajisifu kimoyomoyo.
Akilini mwangu nilikuwa na imani kuwa kunusurika kwangu kulitokana na ukali wa uchawi niliokuwa nikiutumia. Kumbe arobaini zangu zilikuwa bado hazijafika.

Nilipojipakia kwenye gari nilimwambia dereva wangu anirudishe nyumbani kwangu.
Wakati gari likiwa katika mwendo mke wangu akanipigia simu.

“Bado hujaondoka tu huko kwa waziri mkuu?” akaniuliza nilipopokea simu yake.
“Nimeshaondoka, niko kwenye gari narudi nyumbani.”
“Uliitiwa nini?”

Mazungumzo mengine sikutaka yule dereva ayasikie, nikamwambia mke wangu.
“Tutakuja kuzungumza nyumbani.”

“Basi usije ukapitia njia nyingine, nakusubiri.”
Akakata simu na mimi nikairudisha simu mfukoni. Waziri mzima nilikuwa na simu ya bei rahisi ambayo haikulingana kabisa na hadhi yangu. Simu ndogo niliyoweza kuitia kwenye mfuko wa shati langu.

Nilipofika nyumbani nilimwambia dereva arudishe gari ofisini.
“Sitahitaji tena gari hili, nitatumia gari langu binafsi kama nitakuwa na safari yoyote,” nikamwambia.

Dereva akaondoka na gari hilo.
Nilipoingia ndani mke wangu alinifuata sebuleni akanilalia mapajani kwangu na kuniuliza.

“Uliitiwa nini kwa waziri mkuu?”
“Ah! Ni masuala ya kazi tu. Kuna kazi ambayo aliniagiza niifanye.”
“Hakukuwa na tatizo lolote.”
“Hakukuwa na tatizo.”

Pakapita ukimya kidogo kabla ya kuniuliza.
“Sasa mume wangu, naona siku zimekaribia. Hivi mimi nitakwenda kujifungulia kwetu au hapahapa?”

“Kwani wewe umepanga vipi?”
“Mimi sijapanga kitu, nakusikiliza wewe.”
“Mimi naona ujifungulie hapahapa kwako.”
“Halafu hapa nitasaidiwa na nani?”
“Kwani huko kwenu ungesaidiwa na nani?”
“Mama yangu.”

“Basi mama yako atakuja hapa akusaidie au unaonaje?”
“Kama umeamua hivyo ni sawa, nitamwambia. Lakini kwa mila za kwetu mimba ya kwanza unakwenda kujifungulia kwenu. Dada zangu wote walikwenda kujifungulia nyumbani kwetu.”

“Mwambie mama yako aje hapa.”
“Kwa hiyo atakaa hapa kwa miezi mitatu.”
“Hakuna tatizo?”

“Sasa ngoja nimfahamishe kabisa hii leo.”
“Mbona mapema sana! Si usubiri angalau ufike mwezi wa tisa.”
“Kwani unajua huu ni mwezi wa ngapi?”
“Mwezi wa saba.”

“Hapana ni mwezi wa nane tena unaenda mwishoni.”
“Basi subiri ufike mwezi wa tisa ndiyo umwambie.”
“Nilitaka nimwambie mapema ili ajiandae.”
“Sawa, mwambie.”

“Nitampigia simu usiku nimfahamishe.”
Siku ile sikutoka tena nyumbani. Ilipofika usiku mke wangu alimpigia mama yake aliyekuwa akiishi Kinondoni. Akazungumza naye na kukubaliana kuwa mama huyo angekuja kukaa kwetu wakati Suzana akijifungua.

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave a Comment