×

Kuzuia na kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu -2

d661ed60289e4f1e0f16622b055a9d8e_XL

Wiki iliyopita nilianza kuelezea namna ya kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu, leo nitaendelea na mada hiyo ili kukupa ufahamu zaidi wa tatizo hilo.

WATU ambao ni wazito kupita kiasi kwa asilimia 30 wanaweza kupata tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu. Uchunguzi mbalimbali unaonesha kwamba kula vyakula vingi vyenye potasiamu na kalisi kwaweza kupunguza shinikizo la damu.
Uvutaji wa sigara unaweza kusababisha utando mgumu wa mafuta kwenye kuta za mishipa, ugonjwa wa kisukari, mshtuko wa moyo na kiharusi.
Kwa hiyo, mvutaji wa sigara aliye na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu anaweza kupata magonjwa ya moyo. Ijapokuwa uthibitisho unapingana, mfadhaiko na kafeini inayopatikana katika kahawa, chai na vinywaji vya kola yaweza kusababisha tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu.
Kwa kuongezea, wanasayansi wanajua kwamba kunywa kileo mara nyingi na kupita kiasi na kutofanya mazoezi kwaweza kuongeza shinikizo la damu.

KUTUNZA AFYA
Si jambo la busara kungoja hadi upate tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu ndipo uanze kuchukua hatua zinazofaa. Mtu anapaswa kutunza afya tangu anapokuwa kijana. Kutunza afya sasa kutafanya maisha yako yawe mazuri wakati ujao.
Watafiti wa Brazil wameeleza kuwa, yapo madokezo ya mabadiliko fulani maishani ambayo yanaweza kupunguza tatizo hilo. Madokezo hayo yatawasaidia watu wasio na ugonjwa huo na wale wanaougua ugonjwa huo.
Watafiti walipendekeza kwamba watu walionenepa kupita kiasi wanapaswa kula lishe kamili isiyo na kalori nyingi, kufanya mazoezi ya kiasi na kuepuka mbinu za kupunguza uzito haraka. Walipendekeza kwamba watu watumie gramu sita tu za chumvi au kijiko kidogo cha chumvi kila siku. Hiyo inamaanisha kutumia kiasi kidogo cha chumvi wakati wa kutayarisha mlo, na pia kutokula sana vyakula vinavyouzwa makoponi, nyama baridi zilizopikwa (salami, soseji na kadhalika), vyakula vilivyokaushwa kwa moshi. Mtu anaweza kupunguza matumizi yake ya chumvi kwa kuepuka kuongeza chumvi anapokula na kwa kuchunguza vibandiko vilivyowekwa kwenye makopo ya vyakula vilivyotengenezwa viwandani ili kuona kiasi cha chumvi ambacho kimetumiwa.
Vilevile, utafiti kutoka Brazil umedokeza kuwa; kula vyakula vingi vyenye potasiamu kwa kuwa vinaweza “kuzuia kupanda kwa shinikizo la damu.” Kwa hiyo, lishe bora yapaswa kuhusisha “vyakula vilivyo na chumvi kidogo na potasiamu nyingi,” kama vile maharage, ndizi, matikitimaji, karoti, viazi-sukari, nyanya na machungwa. Ni muhimu pia kutokunywa kileo kupita kiasi. Watafiti fulani wanasema kwamba wanaume walio na ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 30 za kileo kila siku; wanawake na vilevile watu ambao si wazito sana hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 15 za kileo.
Utafiti huo ulieleza kwamba, kufanya mazoezi ya mwili kwa ukawaida hupunguza shinikizo la damu na hupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu. Kuna faida ya kufanya mazoezi kwa kiasi kama vile, kutembea, kuendesha baiskeli na kuogelea kwa siku tatu hadi tano kila juma kwa muda wa dakika 30 hadi 45.
Mambo mengine yanayochangia afya bora ni kuacha kuvuta sigara, kudhibiti ugonjwa wa kisukari na kiasi cha mafuta katika damu (kolesteroli na triglyceride), kula vyakula vyenye kalisi na magnesi ya kutosha na kuepuka uchovu na kufadhaika kupita kiasi.
Dawa fulani zaweza kuongeza shinikizo la damu, kama vile dawa za kuzibua pua, dawa za kutuliza kiungulia zilizo na sodiamu nyingi, dawa za kudhibiti hamu ya kula na dawa za kumaliza maumivu ya kichwa na kichefuchefu zilizo na kafeini.
Kwa wazi, iwapo shinikizo la damu yako hupanda, daktari wako anaweza kukushauri kuhusu lishe na mazoea yako kulingana na mahitaji yako binafsi.

MUHIMU
Mambo yanayoweza kusaidia kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu;
• Punguza uzito wa mwili
• Punguza kiasi cha chumvi unachotumia
• Kula vyakula vingi vyenye potasiamu
• Usinywe sana vileo
• Fanya mazoezi kwa ukawaida
• Tumia vidonge vyenye kalisi na magnesi
• Kula vyakula vyenye makapi mengi tu
• Dhibiti mfadhaiko
• Acha kuvuta sigara
• Dhibiti kiwango cha kolesteroli mwilini
• Dhibiti ugonjwa wa kisukari
• Usitumie dawa zinazoweza kuongeza shinikizo la damu.

Leave a Comment