×

Simba hawafiki… hawafiki popote

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
KASI ya Simba katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara hivi sasa haikamatiki kutokana na matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata katika mechi za hivi karibuni, lakini Yanga wamewabeza na kutamka kuwa wapinzani wao hao hawatafika popote.

Simba inawania vikali ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikichuana na Yanga pamoja na Azam FC. Simba kwa sasa ndiyo inayoongoza  msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24, inafuatiwa na Yanga (pointi 50, mechi 21) na Azam (pointi 50, mechi 21).

Hata hivyo, uongozi wa Yanga umetoa msimamo wake kuwa haubabaishwi na kasi hiyo ya Simba kwani itakumbana na kizingiti kikubwa hivi karibuni kitakachoifanya iendelee kuandika rekodi ya kumaliza ligi hiyo ikiwa nyuma ya timu mbili.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro, alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zao zote za viporo, baada ya kuimaliza kazi kubwa iliyokuwa ikiwakabili hivi karibuni dhidi ya APR ya Rwanda.

“Tunamshukuru Mungu kazi kubwa ilikuwa ikitunyima usingizi tumeimaliza na sasa tunarejea ligi kuu kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, hata hivyo kasi ya Simba ambayo wanayo hivi sasa haitubabaishi kwani tunaamini kuwa muda si mrefu itakumbana na kizingiti kwa sababu kikosi chao bado ni kichanga.
“Kwa upande wetu Yanga tumejipanga kuhakikisha timu yetu inashinda katika mechi zake zote za viporo na zile zisizokuwa za viporo itakazocheza nyumbani na ugenini hata kwa bao la mkono,” alisema Muro.

Leave a Comment