×

Uchaguzi umeisha, Tatizo bado lipo!

UCHAGUZI wa marudio wa Zanzibar umefanyika na kumalizika Jumapili iliyopita katika Visiwa vya Unguja na Pemba. Hadi makala haya yanaandikwa, matokeo rasmi yalikuwa bado hayajatangazwa, lakini ni wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaibuka kidedea.

Marudio ya uchaguzi huu yanafuatia kufutwa kwa matokeo ya awali, yaliyofanyika kote Tanzania Oktoba 25, mwaka jana, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha  (pichani) kudai kuwepo kwa dosari kadhaa.

Wote tunajua, baada ya tamko la Jecha, kumekuwa na maneno mengi, lakini hasa msimamo usiobadilika wa chama kikuu cha upinzani visiwani, CUF waliodai kwamba hawatashiriki marudio hayo, kwa kile wanachodai kuwa uchaguzi ulishafanyika na kilichopaswa kufanywa ni kutangazwa kwa matokeo.

Kumekuwa na juhudi nyingi za kuhakikisha suala hili linamalizika kwa amani, ndiyo maana hapo awali, vilikuwepo vikao baina ya CCM na Cuf ili kupata muafaka, lakini katika hali ya kusikitisha, vikao hivyo vikaota mbawa na hatimaye Jecha kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi.

Ni kweli, uchaguzi umefanyika na kumalizika, lakini kama Mtanzania, lazima niseme kuwa kilichotokea kule visiwani Jumapili iliyopita ni kuliongezea uzito tatizo lililopaswa kufanywa wepesi ili liishe.

Siku zote, tatizo linamalizwa kwa mazungumzo. Hakuna sehemu yoyote duniani ambako hila au majeshi yaliwahi kumaliza matatizo. Na bahati mbaya sana, wakati kila mmoja duniani anafahamu kuhusu jambo hilo, lakini mara zote, wanasiasa huja kufanya mazungumzo baada ya hila na nguvu kushindwa, wakati ambao tayari hasara nyingi zimeshajitokeza.

Zanzibar kuna tatizo. Kisiasa, kisiwa hiki kina wafuasi wa vyama viwili tu, CCM na Cuf. Wengine, hata wenyewe wanajua, ni wasindikizaji. Kufanya uchaguzi ambao mojawapo ya vyama hivi havishiriki ni kutoitendea haki Zanzibar.

Nchi bora haiwezi kujengwa kwa ubabe, hila au nguvu. Tumeona uchaguzi ulivyofanyika, hauna watu, hauna shamrashamra na wala hauna hamasa. Upande mmoja wa wananchi unapokuwa umesusa, hata ushindi wa washindi hauna ladha.

Kitu cha msingi kinachopaswa kufanywa na watawala wapya wa Zanzibar ni kulifanyia kazi tatizo wanalolijua. Kujifanya hatulioni tatizo na kwamba kila kitu kiko sawa ni kujidanganya wenyewe.
Ni kweli kwamba wananchi walionekana wakienda kupiga kura katika vituo vyao huku hali ya hewa ikiwa safi kabisa, bila fujo wala vitisho vya askari wenye silaha. Watu waliendelea vizuri na shughuli zao hata kwa wale ambao hawakwenda katika vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, amani na utulivu ule haukuwa halisi. Katika nchi ambazo demokrasia imekubalika, uchaguzi huu ungekuwa na shamrashamra nyingi kuliko ule wa awali. Kuna kitu kipo nyuma ya utulivu huu ni jukumu la viongozi wetu kukiona kitu hicho na kukifanyia kazi kwa maana ya kusawazisha mambo.

Tatizo la Zanzibar siyo la Maalim Seif na Dk. Mohammed Shein bali ni la kihistoria, ndiyo maana hata kukawepo katika katiba yao inayotaka uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa. Na serikali hii ya umoja, wala siyo kati ya viongozi hawa wawili, bali ni kati ya jamii mbili kubwa miongoni mwa Wazanzibari.
Wanatakiwa aina ya viongozi wanaofahamu jambo hili kwa dhati na wao wawe tayari kulimaliza. Watu wanaweza kuwa watulivu kwa sababu ya hofu na hili linapotokea ni kosa kubwa kuamini kuwa hii ni amani.

Kitu kinachowakwamisha viongozi wengi wa Afrika ni kuweka ukomo wa mazungumzo. Mjadala unaohusu ustawi wa taifa hauwezi kuwekewa ‘deadline’ kwa sababu unahusu maisha ya watu. Mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar siyo jambo la kumalizwa ndani ya wiki mbili ili mambo mengine yaendelee, hili ni jambo kubwa linalohitaji muda wa kutosha!

Kama ni madai ya Cuf kuibiwa kura, mbona hata wapinzani wa Bara wanalalamika lakini hali haiwi tete kama Zanzibar? Kwa nini hali haitulii kila baada ya uchaguzi? Ukweli mchungu ni kuwa lipo tatizo la msingi ambalo sanduku la kura pekee halitoshi kulitatua.
Baada ya marudio haya, tunahitaji viongozi waliochaguliwa kuandaa mazingira ya kurejea meza ya majadiliano kwa faida ya Wazanzibar wote!

Leave a Comment