
Mmoja wa kigogo wa unga maarufu mama Leila anayedaiwa kutoroka.
Stori: Oscar Ndauka na Hashim Aziz, UWAZI
DAR ES SALAAM: Hali si shwari kwa wafanyabiashara haramu wa madawa ya kulevya ‘unga’ nchini ambapo kufuatia msako mkali unaoendeshwa na Jeshi la Polisi Tanzania Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, wengi wao wanatajwa kutorokea nje ya nchi wakikwepa kukamatwa.
Kwa mujibu wa vyanzo, kamatakamata ya wauza unga inayoendelea kwa kasi nchini, imewafanya wengi wanaohusika na biashara hiyo kutelekeza familia zao, mali zao huku wengine wakifunga biashara zao na kutorokea mafichoni.
KISIKIE CHANZO CHETU
“Unajua hii serikali ya Rais Magufuli (John Pombe) siyo kama zilizopita.
Rais hataki utani kabisa na akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kitwanga (Charles) alishaapa kuwashughulikia wauza unga wote na kweli ndani ya kipindi kifupi tunaambiwa kwamba zaidi ya watu 3,000 wamekamatwa wakihusishwa na biashara hiyo, sasa hata kama ni wewe utaendelea kukaa nchini?
“Wengi wamekwenda kujificha nchini Afrika Kusini, Dubai, Msumbiji na nchi za Ulaya. Wamekimbilia huko wakiogopa kukamatwa maana wanajua Magufuli hana simile na wauza unga,” kilisema chanzo kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
WATELEKEZA FAMILIA
Chanzo kingine kilichojitambulisha kwamba kinaishi jirani na mfanyabiashara mmoja mkubwa wa unga, Kinondoni jijini Dar, kilifunguka:
Ali Khatibu Haji ‘Shkuba’
“Kwa muda mrefu tunajua kwamba huyu jirani yetu anajihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Si unaona hata mjengo aliojenga hakuna anayemfikia mtaa mzima!
“Cha ajabu, tangu kamatakamata ianze, huu ni mwezi wa tatu jamaa haonekani mtaani. Kama angekuwa amekamatwa tungejua lakini taarifa zilizopo ametorokea Afrika Kusini. Hapa kuna mkewe na watoto tu, nao wanaonekana kwa machale.”
BIASHARA ZAFUNGWA
Uchunguzi uliofanywa na kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers, umebaini kuwa, biashara nyingi ambazo wamiliki wake walikuwa wakihusishwa na biashara ya unga, zimefungwa huku sababu zikiwa hazijulikani.
“Si unaona lile duka la jumla pale barabarani, mmiliki wake ni (akalitaja jina). Huyu anatajwa kuwa ni kigogo wa unga. Tangu jamaa asikie anafuatiliwa, amekimbia nchi na biashara zake amefunga.
“Anamiliki baa nyingine mbili, moja ipo Ilala, nyingine Kinondoni lakini nasikia zote zimefungwa,” kilisema chanzo chetu kilipoongea na OFM.
UWAZI OFISINI KWA KAMANDA MSIKHELA
Baada ya taarifa hizo, gazeti hili kama ilivyo kawaida yake, lilitafuta mzani wa habari upande wa pili kwa kufunga safari mpaka Ofisi za Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Kurasini Dar.
Askofu.
Hata hivyo, kamanda wa kikosi hicho, ACP Mihayo Msikhela alisema bado hajakabidhiwa rasmi ofisi hivyo hawezi kuzungumza chochote lakini akalitaka Uwazi kumtafuta aliyekuwa akiongoza wa kitengo hicho, CP Robert Boaz ambaye alikuwa na haya ya kusema:
“Tunajua, serikali ina mkono mrefu hivyo hakuna mtu yeyote anayejihusisha na biashara ya unga atakayeweza kukwepa. Dawa pekee ni kuacha biashara hiyo kwani hivi sasa tumejipanga sawasawa dunia nzima.
“Mtu akitoroka nchini tuna njia nyingi za kumfikia. Kwa mfano, tunaweza kuwatumia Polisi wa Kimataifa (Interpol) hivyo hakuna njia ya kukwepa.”
Ili kujua mikakati zaidi ya serikali kuhusu waliyoikimbia nchi, Ijumaa iliyopita, Uwazi lilimsaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ambaye aliomba kutafutwa baada ya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Jumapili iliyopita.
WANAOSHIKILIWA
Mpaka sasa, Uwazi lina majina kumi ya watu wanaoshikiliwa na serikali kwa madai ya kufanya biashara hiyo haramu ambao ni Muharami Abdallah ‘Chonji’, Ali Khatibu Haji ‘Shkuba’, Emeka Nwachukwu, Doreen John, Fred William ‘Chonde’, Christina Naphtali, Moreen Lyumba, Hemed (jina moja) na Mohamed Khariri, Salma Omar na Leila (jina moja).