×

Mkurugenzi akanusha kutumbuliwa jipu na Magufuli

SONGWE: Aliyekuwa     Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani hapa kabla ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kumsimasisha kazi hiyo, Halima Ajali ameibuka na kusema hakutumbuliwa jipu (kufukuzwa kazi) bali amepumzishwa kazi  kutokana na barua yake inavyoeleza.

Ajali alihoji kuwa, serikali ingemsimamisha kazi kwa kosa lipi alilofanya ambalo yeye halijui?
Kuhusu madai ya madiwani wa halmashauri hiyo kutokuwa na imani naye, alisema ndiyo serikali iliamua kumpumzisha kazi ili ijaribu kuchunguza kujua matatizo yapo kwa watu gani, madiwani au yeye.

“Nawaomba wananchi wa Jimbo la Tunduma kutoamini maneno ya watu ambayo hayana ukweli wowote. Wengi wao hawamjui hata mwajiri wangu na wakae wakijua mimi siyo mwanasiasa bali ni mtendaji wa serikali na ninateuliwa na siyo kuchaguliwa kama wanasiasa,” alisema mwanamama huyo.

Aliongeza: “Barua yangu ya kupumzishwa inasema nimesimamishwa kazi na sitakiwi kuondoka katika kituo changu cha kazi. Kama nitaondoka basi niwe na kibali maalumu kutoka kwa mwajiri wangu  kwamba nakwenda sehemu fulani ili niruhusiwe.”
Mkurugenzi huyo ambaye kwa sasa yupo nyumbani tu, alisema baada ya kupumzishwa kazi, serikali imemkaimisha mkurugenzi wa muda mpaka itakapofanya uteuzi wa mkurugenzi hivyo imemteua Erick Mapunda  kukaimu nafasi hiyo.
“Wananchi acheni  kuzungumza vitu ambavyo havina faida kwenu huku mkiwa mnapewa maneno kutoka kwa watu wachache ambao lengo lao ni kutaka kunichafua nionekane ni mtendaji mbovu wakati ni njama za watu wachache,’’ alisema.
Februari, mwaka huu, Serikali ya Rais John Pombe Magufuli kupitia kwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, alimsimamisha kazi Ajali kwa madai ya kukiuka maadili ya uongozi.

Leave a Comment