×

The Beginning of My End (Mwanzo wa Mwisho wangu-07)

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.

Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.

Historia ya makuzi ya Ben, inamfanya Jordan ahisi kwamba Ben hajaua ila ameamua kukubali kwa sababu ambazo yeye mwenyewe ndiye anayezijua. Jitihada zake za kutaka kuufahamu ukweli ili amnasue rafiki yake huyo kutoka kwenye kitanzi kilichokuwa kinamsubiri, zinagonga mwamba kutokana na Ben kukataa kutoa ushirikiano, muda wote aking’ang’ania kwamba ni yeye ndiye aliyeua.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma. Anahitimu kidato cha nne na kufaulu kwa kiwango cha juu.Je, nini kitafuatia? Ben atapewa hukumu gani?

SONGA NAYO…

Miezi miwili baadaye, majina ya wanafunzi na shule walizochaguliwa kujiunga na kidato cha tano yalitoka, Ben akachaguliwa kwenda kujiunga na Shule ya Sekondari ya Vipaji Maalum ya Mzumbe.
Fedha alizokuwa anahifadhi kidogokidogo, ukichanganya na zile alizochangiwa na wanafunzi pamoja na walimu wake siku ya kupongezwa, zilitosha kununua mahitaji yote muhimu, likiwemo godoro dogo, sanduku la chuma, madaftari na vifaa vingine vingi vya kutumia shuleni.

Japokuwa alikuwa anaenda kupiga hatua kubwa kitaaluma, mama yake alilia sana wakati Ben anajiandaa kwa ajili ya kuelekea shuleni. Kilichomliza zaidi, alikuwa hajui ataishije na wanaye waliosalia bila uwepo wa Ben.
Kwa kipindi chote alichokuwa akiugua, Ben ndiyo alikuwa kichwa cha familia, ni yeye ndiye aliyewezesha familia hiyo kula, kupata mahitaji yote muhimu na mama yake kupata dawa.

“Usilie mama, Mungu ndiye anayejua namna mtakavyoishi. Tazama ndege wa angani hawalimi wala kufanya kazi yoyote lakini wanakula na kuishi vizuri, Mungu atawasimamia,” alisema Ben akiwa amekumbatiana na mama yake, akimbembeleza kwani alikuwa akilia sana.

Akamuahidi kwamba akiwa shuleni, atakuwa anajitahidi kutafuta kazi ndogondogo na akilipwa, atakuwa anawatumia fedha kwa ajili ya kuwasaidia mahitaji madogomadogo. Kauli hiyo kidogo ilimridhisha mama yake, akapunguza kulia na kuanza kumpa mwanaye mwongozo wa namna ya kuishi ugenini.
“Ukawaheshimu wakubwa kwa wadogo, usimdharau mtu yeyote kwa sababu hujui ni nani atakayekusaidia. Elekeza nguvu zako zote kwenye masomo, si unaona hali uliyotuacha nayo hapa nyumbani? Nakuombea kwa Mungu atakusimamia mwanangu,” alisema mama yake Ben na kumbusu mwanaye kwenye paji la uso kama ishara ya kumbariki.

Aliendelea kumueleza mambo mengine mengi ya msingi, Ben akawa anamsikiliza kwa makini huku akiahidi kuyafanyia kazi yote aliyokuwa anaambiwa. Siku zilizidi kusonga mbele na hatimaye siku ya kuondoka Ben iliwadia. Kama alivyokuwa ameahidi, mwalimu Tung’ombe alimpa fedha za kulipia ada pamoja na za matumizi mengine muhimu.
Ikabidi Ben agawe zile fedha za matumizi, nyingine akamuachia mama yake na nyingine akaondoka nazo. Ilikuwa safari ndefu sana kutoka Tunduma mpaka Morogoro. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Ben kusafiri, tena safari ndefu kiasi hicho.

Hatimaye aliwasili shuleni, Mzumbe ambapo alifuata taratibu zote za msingi na kusajiliwa rasmi kuwa mwanafunzi wa shule hiyo. Wanafunzi wengine waliendelea kuwasili na wiki moja baadaye, masomo yalianza rasmi. Kwa jinsi Ben alivyokuwa na usongo, aliongeza juhudi kuliko kawaida.

Mazingira ya kusomea yalikuwa tofauti sana na kule alikotokea ambapo kwa kuwa shule ilikuwa ni ya bweni, muda wote wanafunzi walikuwa hapohapo shuleni, Ben akawa na muda mrefu wa kujisomea kuliko alipokuwa akisoma shule ya kutwa.
Kutokana na jinsi alivyokuwa na bidii katika masomo, wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania kwamba ametumwa na kijiji kuja kusoma ndiyo maana alikuwa akikesha darasani akisoma. Mwenyewe hakujali utani huo, akaendeleza juhudi na miezi michache baadaye, matunda ya juhudi zake yalianza kuonekana.

Walipofanya mtihani wa kwanza, Ben aliibuka kidedea na kushika nafasi ya kwanza, akiwaacha wenzake kwa mbali licha ya kwamba darasa zima lilikuwa limejaa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kiakili.
Hali hiyo ilimfanya aanze kuwa maarufu, walimu wakawa wanampenda huku wanafunzi wenzake nao wakianza kumkubali kwani wakati mwingine, alikuwa akiwafundisha yale masomo wanayoshindwa kuyaelewa kwa urahisi. Siku zilizidi kusonga mbele, Ben akaendelea kuwa tishio miongoni mwa wanafunzi wenzake kwani kwenye kila mtihani, alikuwa akishika nafasi ya kwanza.

Hatimaye mwaka wa kwanza uliisha, wakafanya mtihani wa mwisho wa kuingilia kidato cha sita kisha shule zikafungwa. Kwa kuwa hiyo ilikuwa likizo ndefu, na tangu ajiunge na shule hiyo hakuwahi kurudi nyumbani, Ben alilazimika kusafiri kurejea nyumbani. Fedha za akiba alizokuwa nazo zilimtosha kwa nauli.
Akafunga safari mpaka Tunduma huku njia nzima akiwafikiria ndugu zake pamoja na mama yake. Aliwanunulia zawadi nyingi ambazo aliamini wakiziona, watafurahi sana. Baada ya kushuka kwenye stendi ya mabasi ya Tunduma, Ben aliongoza moja kwa moja mpaka nyumbani kwao.

Kabla hajafika, alishangazwa na jinsi watu waliokuwa wanamfahamu walivyokuwa wakimtazama. Ilionesha dhahiri kwamba kulikuwa na jambo lisilo la kawaida limetokea nyumbani kwao. Hata hivyo, alipiga moyo konde na kuendelea na safari yake. Alipofika jirani na kibanda chao kikuukuu, alishtushwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yao, moyo ukamlipuka paa!
“Mungu wangu, kuna nini tena,” alijiuliza huku akihisi mwili wake wote kuwa mzito.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment