Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
ARUSHA: Mtu mmoja aitwaye Hamisi Mohamed,47, (pichani) Mkazi wa Kondoa Mkoa wa Dodoma, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha akidaiwa kukutwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyokuwa anaisafirisha kwa mtindo wa aina yake huku magunia 270 ya bangi yakikamatwa wilayani Arumeru.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo lilitokea hivi karibuni eneo la Mianzini.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anasafirisha madawa hayo kwenye gari aina ya Fusso lenye namba za usajili T 577 BFM ambapo aliihifadhi kwenye magunia mawili huku juu na pembeni ya magunia hayo akiweka viatu.
“Katika magunia yale alikuwa ameweka viatu na katikati aliweka viroba 36 vya madawa hayo aina ya mirungi ambayo alikuwa anasafirisha toka nchini Kenya kupeleka Kondoa mkoani Dodoma hivyo ukiangalia unaweza kusema ni viatu pekee,” alifafanua Kamanda Sabas.
Alisema tukio hilo lilifanikiwa kutokana na mahusiano mema yaliyopo kati ya jeshi hilo na raia wema ambao walitoa taarifa iliyofanyiwa kazi haraka na asakari wa jeshi hilo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana jumla ya magunia 270 ya bangi yalikamaywa Arumeru na ekari 25 za mashamba yake ziliteketezwa.
“Katika kipindi hicho pia katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha jumla ya kilo tatu za dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine na kilo 1,800 za mirungi zilikamatwa,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Alibainisha kuwa watu 180 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya na 160 kati yao wameshafikishwa mahakamani, alikuwa akitoa taarifa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) huku akipongeza vyombo vya usalama kwa kazi nzuri.