×

Penzi Kabla ya Kifo-24

Mambo yamebadilika! Bilionea Rasheed anatoka nchini Morocco na kumfuata bilionea Elizabeth nchini Ujerumani, anapofika huko, anamwambia ukweli kwamba anampenda, kitu kinachomsikitisha ni kwamba msichana huyo anamwambia amechelewa kwani tayari amepata mwanaume mwingine, Rasheed anakasirika.
SONGA NAYO…

Rasheed alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokisikia kwamba alichelewa kwa kuwa tayari msichana huyo alimpata mwanaume mwingine ambaye alisema kwamba alimpenda kwa moyo wa dhati. Alipomwangalia, alitamani kulia, alitamani kumpigia magoti na kumsisitizia awe mpenzi wake kwani hakukuwa na msichana aliyekuwa akimpenda kama yeye.
“Elizabeth.”
“Ndiyo hivyo Rasheed. Sitaki kukuumiza baadaye kwa kuwa nilikuficha ukweli ni bora uumie sasa hivi huku ukiufahamu ukweli. Nisamehe kwa hilo,” alisema msichana Elizabeth, tabasamu halitoka usoni mwake.
Hakuwa na jinsi, japokuwa alijitahidi sana kumwambia msichana huyo namna alivyokuwa akimpenda lakini bado msimamo wa Elizabeth ulikuwa uleule kwamba hakutaka kuwa naye kwa kuwa alikuwa na mwanaume mwingine aliyempenda kuliko wote.
Alichokifanya Rasheed ni kurudi nchini Morocco huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali, kukataliwa na Elizabeth kilikuwa kitu ambacho hakutaka kukubaliana nacho kirahisi, aliamua kufanya jambo moja, mwisho wa siku ampate msichana huyo.
***
“Kila kitu tumefanya, sidhani kama tunatakiwa kufanya zaidi ya hapa,” alisema Dk. Zeus.
“Kivipi?”
“Tumejitahidi kumtibu, hakuna tunachoweza kufanya zaidi, tumemaliza kila kitu, cha msingi, naomba mrudi nyumbani, ataendelea kupona kadiri siku zitakavyokwenda mbele,” alisema Dk. Zeus.
“Cha kuzingatia?”
“Mumpe sana kongoro ale, zitasaidia kuurudisha uti wa mgongo katika hali ya kawaida,” alisema
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kila kitu, madaktari walijitahidi kwa miezi mitatu mfululizo kumtibu Glory na mwisho wa siku waliona ni bora kumruhusu kurudi nyumbani kwani hawakutegemea kama kungeweza kutokea muujiza mwingine zaidi ya hapo.

Hawakuwa na jinsi, baada ya siku mbili, safari ya kurudi nchini Tanzania ikaanza mara moja. Siku ambayo walikuwa wakifika uwanja wa ndege jijini Dar es Salaa, tayari idadi kubwa ya watu walikuwa mahali hapo, walipata taarifa juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.

Walimpenda Elizabeth, alikuwa msichana maarufu, alijulikana zaidi ya alivyokuwa akijulikana rais wa nchi hiyo. Uwanjani hapo, waandishi wa habari hawakuwa mbali, walifika mapema sana kwa ajili ya kupiga picha kile ambacho kingeweza kutokea uwanjani hapo.

Ndege ilipotua na kusimama, wakateremka huku kukiwa na watu wawili waliowasaidia kukishusha kiti alichokuwa amekalia Glory. Wakaanza kutoka nje ya uwanja ule ambapo mara baada ya kuingia ndani ya jengo la uwanja huo, wakapigwa na mshangao baada ya kuwaona watu wengi wakiwa wamekusanyika, walipoonekana tu, kila mtu akaanza kwenda kule alipokuwepo.

Pasipo msaada wa walinzi waliokuwa mahali hapo hali ilionekana kuwa mbaya sana. Walinzi hao wakawazuia watu na kuwaambia wafuate utaratibu uliotakiwa kufuatwa. Miale ya kamera iliendelea kumulikwa na waandishi wa habari ambao walikuwa bize wakipiga picha matukio kadhaa.
“Anaendeleaje?” aliuliza mwandishi mmoja.
“Nani?” aliuliza Elizabeth.
“Huyu msichana.”
“Anaendelea vizuri, si mnamuona kidogo anatabasamu.”
“Tunafurahi kuona hivyo!”
Hawakutaka kukaa sana uwanjani hapo, walichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani. Huko, James hakutakiwa kurudi alipokuwa akiishi bali safari hiyo alichukuliwa na kupelekwa nyumbani kwa Elizabeth.
Maisha yake yalibadilika ghafla, hakuamini kama kweli katika kipindi hicho alikuwa na msichana bilionea ambaye aliyabadilisha maisha yake kwa asilimia mia moja. Muda mwingi alibaki akimshukuru Mungu kwani kila kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa muujiza mkubwa.
Mapenzi yalikuwa motomoto, Elizabeth alijisikia uhuru na kila siku katika maisha yake hakukuwa na mtu aliyempenda na kumthamini kama alivyokuwa James. Kwake, hakukuwa na mtu aliyeuteka moyo wake vilivyo kama mwanaume huyo.
Kila siku, kama njiwa walikuwa pamoja, James akawa huru, akawa anatumia pesa za Elizabeth alivyopenda. Ili kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa akimpenda mpenzi wake huyo, Elizabeth akamuingizia kiasi cha shilingi bilioni moja katika akaunti yake benki.
James akachanganyikiwa, fedha zile zikaongeza mapenzi zaidi na kumchanganya vilivyo.

Je, nini kiliendelea? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment