×

The Beginning of My End (Mwanzo wa mwisho wangu)- 10

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo.
Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.
Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.
Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani, anafaulu kwa kiwango cha juu na baada ya kuhitimu kidato sita, anaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Ben alibaki amepigwa na butwaa kwani ukiachilia mbali mambo mengine, hakuwahi kukumbatiwa na msichana hata mara moja katika maisha yake, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida.
“Ooh! Im sorry if I’ve annoyed you!” (Ooh! Samahani kama nimekukera!) alisema msichana huyo huku akijitoa kwenye kifua cha Ben na kurudi nyuma hatua moja baada ya kuyaona mabadiliko aliyokuwa nayo kijana huyo. Akawa anamtazama usoni, Ben akawa anababaika huku aibu zikijionesha dhahiri kwenye uso wake.
“Im Gladness! Nice to meet you Mr Benjamin Semzaba!” (Naitwa Gladness! Nimefurahi kukutana na wewe Bwana Benjamin Semzaba) alisema msichana huyo huku akinyoosha mkono kumpa Ben, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Ben naye alijikakamua kiume, akanyoosha mkono na kumpa msichana huyo huku tabasamu lililochanganyikana na hofu likichanua kwenye uso wake.

Msichana huyo alimuomba wakakae meza moja kama hatajali, Ben akakubali huku akipoteza kabisa hali ya kujiamini.
“Hebu niambie, uliwezaje kuwa mwanafunzi bora wa nchi nzima?”
“Aah! Kawaida tu, ukijituma hakuna kisichowezekana,” alisema Ben huku akikaa vizuri kwenye kiti chake, mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea huku msichana huyo akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake. Alimueleza kwamba yeye ni mzaliwa wa Dar es Salaam na baba yake alikuwa akifanya kazi kwenye Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania.
Ben naye alieleza kwa kifupi historia yake, hakufurahishwa sana na jinsi msichana huyo alivyokuwa anaendelea kumhoji maswali mbalimbali kuhusu familia yao, ikabidi akatishe mazungumzo hayo, wakaendelea na mazungumzo ya kawaida na huo ukawa mwanzo wa wawili hao kufahamiana.

Gladness Brian Mchome alikuwa msichana mweupe, mrefu kiasi na mwenye umbo lililojengeka kikekike haswaaa! Kifua chake kilipendezeshwa na ‘vifuu’ viwili vilivyojaa vizuri na kuchongoka upande wa mbele huku miguu yake iliyonawiri vizuri ikimfanya apendeze sana hata anapovaa sketi fupi.
Kwa kumtazama tu, alionesha dhahiri kwamba ametoka katika familia bora inayojiweza kiuchumi. Muda wote alikuwa akipendeza, alivaa mavazi mazuri ya kisasa na kunukia marashi ya bei mbaya, huku fedha ndogondogo za matumizi zikiwa siyo tatizo kwake.

Uzuri wa kipekee aliokuwa nao, ulimfanya awe gumzo kubwa chuoni hapo, wanaume wengi, wakiwemo wanachuo wenzake mpaka wahadhiri wakawa wanampapatikia, kila mmoja akitaka nafasi ya kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
Hata hivyo, mwenyewe hakujali wala hakubabaishwa na chochote, muda mwingi alikuwa akipenda kuwa karibu na Ben. Japokuwa kwa kuwatazama hawakuwa wakiendana, Ben akionesha dhahiri kwamba anatokea kwenye familia duni na amekulia maisha ya kimaskini, Gladness hakujali chochote.
“Oya mwanangu yule demu anamchomolea kila mtu anayemtokea hapa chuo kumbe kisa ni yule mshamba anayeitwa Ben!”
“Mi mwenyewe nimesikia mwanangu, jamaa mwenyewe mshamba tu, hata kupiga pamba kali hajui, sijui kamshobokea kwa kipi!”
“Inaweza kuwa ndumba, nasikia mshikaji anatokea huko karibu na Sumbawanga, si ajabu kamuendea kwa babu kumroga ndiyo maana mtoto mzuri kamzimikia,” vijana kadhaa waliokuwa wakisoma chuoni hapo, walikuwa wakimsimanga Ben, muda mfupi baada ya kuonekana akitoka kantini, akiwa ameongozana na msichana huyo mrembo.

Kila mmoja alikuwa akimsema vibaya Ben kutokana na kumuonea wivu! Hata hivyo, wakati kila mmoja akiamini kwamba wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi, hali ilikuwa tofauti kabisa kwa Ben ambaye alikuwa akimchukulia Gladness kama rafiki wa kawaida tu.
Ukaribu kati yake na Gladness, ulizidi kuongezeka na kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo walivyozidi kuzoeana, ikawa Gladness hawezi kufanya jambo lolote bila Ben kuwepo. Kwa kuwa fedha hazikuwa tatizo kwenye familia yao, mara kwa mara alikuwa akitoka na Ben, hasa siku za mwisho wa wiki na kwenda kufanya ‘shopping’ ndogondogo za nguo na mahitaji mengine muhimu.

Taratibu Ben akaanza kubadilika, akaanza kuvaa nguo nzuri na kunukia manukato mazuri aliyokuwa anapewa na msichana huyo. Kwa kuwa pia Ben alikuwa akipenda sana kufanya mazoezi, muda wa jioni akawa anajumuika na wanachuo wenzake kwenye michezo mbalimbali hususan kunyanyua vitu vizito, hali iliyolifanya pia umbo lake libadilike na kuwa na misuli mingi iliyojengeka vizuri.

“Ni mabadiliko hayo ndiyo yaliyofanya ule utanashati wake wa asili aliozaliwa nao Ben, uanze kuonekana na kumzidishia mvuto. Upande wa darasani, kama ilivyokuwa kawaida yake, alikuwa akisoma kwa bidii na baada ya muda, naye akaanza kuwa gumzo chuoni hapo.

Watu ambao awali walikuwa wakimsema kwa mabaya, wakaanza kumvulia kofia kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa anauonesha darasani. Hata wale ambao awali hawakuwa wakijua kwamba Ben ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora wa kidato cha sita kwa mwaka huo, walianza kumjua, umaarufu wake na Gladness ukazidi kuongezeka.
“Ben!”
“Naam!”
“Hivi ni kweli mimi ni mrembo?”
“Mh! Ina maana hujui kama wewe ni mzuri sana Gladness?”
“Mh! Mbona sijawahi kukusikia wewe ukinisifia zaidi ya watu wengine?”
“Wewe ni mzuri sana Gladness, naona Mungu alikuumba siku ambayo hakuwa na kazi nyingi, hongera kwa hilo,” alisema Ben na kumfanya Gladness acheke mno kwa furaha, hakuna kitu alichokuwa anakipenda kama kusifiwa na Ben.
“Basi naomba uwe unanisifia mara kwa mara, nasikia raha mwenzio,” alisema Gladness huku akimkumbatia Ben kifuani, wakiwa wanapunga upepo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jioni moja ya mwisho wa wiki.

Katika hali ambayo Ben hakuitegemea, alishangaa kuona Gladness akizidi kumng’ang’ania kwenye kifua chake kipana kisha akambusu mdomoni. Kitendo hicho kilimfanya Ben ahisi hali ambayo hakuwahi kuihisi hata mara moja, alipomtazama Gladness usoni, macho yake yalikuwa mithili ya mtu aliyebanwa na usingizi mzito.
Macho yao yalipogongana, Gladness aliita tena lakini safari hii sauti yake ilikuwa ikitokea puani.
“Ben! Samahani kama nimekukosea, kuna kitu nimekaa nacho moyoni kwa muda mrefu sana, naomba leo nikwambie,” alisema Gladness kwa sauti ya chini iliyobeba ujumbe mzito, Ben akajikuta akisisimka mwili mzima.

“Niambie Gladness, nakusikiliza,” alijibu kwa sauti nzito ya kiume, badala ya kumueleza alichotaka kusema, msichana huyo mrembo alimvutia Ben kifuani kwake na muda mfupi baadaye, wakagusanisha ndimi zao.
Kitendo hicho kilikuwa kigeni kabisa kwa Ben, hakuwahi kukifanya hata mara moja maishani mwake, ukiachilia mbali ukweli kwamba hakuwa akimjua mwanamke, akajihisi kama anapaa kwenye mbingu ya tofauti kabisa. Gladness aliendelea kumganda kama ruba huku mikono yake laini ikivinjari sehemu mbalimbali za mwili wake, Ben akawa anatoa migumo ya hapa na pale.

“Samahani kwa usumbufu, chakula chenu kipo tayari,” sauti ya mhudumu wa hoteli hiyo iliyokuwa ufukweni mwa bahari, ndiyo iliyowazindua wawili hao kutoka kwenye ulimwengu wa tofauti kabisa, harakaharaka wakaachiana huku kila mmoja akijihisi aibu kubwa kwani hawakujua ni kwa muda gani yule mhudumu alisimama pale.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment

Leave a Comment