Tunaendelea kuchambua matatizo ya macho.Tatizo la macho liitwalo kitaalam Presbyopia humuathiri karibu kila mtu anayevuka miaka 45. Watu wengi hutumia miwani ya kusomea au lenzi zenye kukuza herufi Bifocal au Progressive Lenses.
Lakini pia kuna tiba za upasuaji macho kwa tatizo hili. Hii ni kwa watu ambao tiba hiyo inawafaa.
Tatizo sugu la ukavu wa macho Chronic Dry Eye huyaathiri macho yako kwa namna nyingi ikiwa ni pamoja na kufifiliza na kubadilisha-badilisha uoni wa macho.
Wakati ambapo machozi ya bandia Artificial Tears huweza kusaidia, tatizo la ukavu wa macho linapozidi kiwango laweza kuhitaji dawa za kuandikiwa na daktari au vilainishio vya kulainisha macho na kuyaweka katika afya nzuri Punctal Plugs.
Ujauzito. Kufifia kwa uoni wa macho ni tatizo la kawaida katika kipindi cha ujauzito na wakati mwingine huambatana na uoni wa vitu viwili-viwili-kuona dabodabo Diplopia.
Mabadiliko ya homoni huweza kubadili muundo na upande wa konea ya jicho lako, na kusababisha uoni wako kufifia. Ukavu wa macho pia ni jambo la kawaida kwa wajawazito na huweza kusababisha uoni hafifu wa macho.
Mara zote unapaswa kuripoti kwa daktari matatizo yoyote ya macho katika kipindi cha ujauzito. Wakati ambapo uhafifu wa kuona, katika baadhi ya kadhia si jambo la kutisha, lakini kwaweza kuwa dalili ya magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu.
Usikose kufuatilia mwendelezo wa makala haya wiki ijayo.