×

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-42

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas aliyepata tatizo la kutosikia vizuri baada ya mama Bite kumpiga makofi ya masikioni alipomfahamisha mama huyo aliyemkebehi kwamba kama hakusikia vizuri yeye afanyeje? Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Kauli hiyo iliniumiza sana, kulipokucha kabla hawajaamka nikaenda mtaa wa pili alipokuwa akiishi dada aitwaye Stellah niliyekuwa naelewana naye sana na alijua mambo yangu mengi.
Nilimwelezea suala zima la kupigwa na manyanyaso niliyopata na kumuomba anisaidie fedha ili nirudi Mbeya kwa mama mkubwa.

Stellah aliyekuwa akifanya biashara alihuzunika sana, alinipatia shilingi 30,000 na alinifahamisha kuwa nina bahati sana kwani jioni ya siku hiyo angehamia kwenye nyumba yake huko Kimara na flemu yake pia angeihamishia huko, akasema kabla sijaenda Mbeya alitaka nikapafahamu makazi yake mapya ili iwe rahisi siku nikitaka kurudi Dar nifikie kwake.

Alinieleza kuwa sikutakiwa kabisa kuendelea kuishi kwa yule mama mkatili, akasema nikifika nyumbani nikusanye vitu vyangu halafu niende dukani kwake ambako nilimuacha anapakia kila kitu tayari kwa kuhama kwenda Kimara.
Nilifurahi sana, nilipofika nyumbani wote walikuwa bado wamelala, nilichukua begi langu na vitu vyangu vyote nikaenda kwa dada Stellah ambaye nilimkuta yuko tayari, tuliondoka na kuelekea Kimara.
Alfajiri dada Stellah alinisindikiza Ubungo akanikatia tiketi ya kwenda Mbeya, nikiwa safarini niliwaza mambo mengi ila kubwa ni kumsimulia mama mkubwa masaibu yaliyonikuta kwa yule rafiki yake wa Shinyanga.
Niliwasili Mwanjelwa, Mbeya saa 12.15 jioni, nilipanda daladala za kwenda Soko Matola nikashuka Kituo cha Sinde  na kukatisha njia ya mkato kuelekea kwa mama mkubwa, njiani nilikutana na mama Ambokile, alishangaa aliponiona na kunipongeza kwa kuwa mkubwa.

Licha ya kuzungumza mawili matatu na mama huyo alionesha alikuwa na jambo moyoni mwake, nilipomuuliza mama mkubwa hajambo aliniambia hajambo na alinifahamisha kwamba alihamia Usangu, akanitaka nikalale nyumbani kwake ili kukicha nianze safari ya kwenda Usangu.
Usiku tukiwa tumekaa jikoni tukiota moto baada ya kumaliza kula chakula, mama huyo aliyekuwa mjane aliniambia kuna jambo alitaka kuniambia lakini niwe jasiri kwa sababu hakuona sababu ya kunificha.
Nikiwa mwenye shauku ya kujua jambo hilo, alinifahamisha kwamba mama yangu mkubwa alifariki dunia kwa ajali ya kugongwa na gari miezi mitano iliyopita.

Taarifa hiyo ilinifanya nianze kulia kwani sikujua hatima ya maisha yangu ingekuwaje, mama Ambokile alinipa pole. Nilipomuuliza alizikwa wapi japo nikalione kaburi lake akaniambia kijijini kwao Tukuyu.
Hakika niliona dunia imenitenga, nililia sana lakini hakuna kilichobadilika ukweli ulibaki vilevile kuwa mama mkubwa kipenzi cha mama yangu naye alifariki dunia. Nilikaa Mbeya siku tatu ndipo yule mama akanipa nauli nikarudi Dar kwa dada Stellah aliyenipokea kwa upendo.

Nikiwa naishi kwa dada Stellah aliyekuwa ananipenda na kuahidi kunisomesha na kuishi nami katika maisha yake yote, kadiri siku zilivyokwenda masikio yangu yalipoteza uwezo wa kusikia.
Baada ya kuhangaikia tiba bila mafanikio alinipeleka Muhimbili ambapo nilifanyiwa vipimo na kugundulika masikio yangu yalipata matatizo makubwa hivyo nisingeweza kupona na huenda ningekuwa kiziwi.
Siku hiyo nililia sana na kumuuliza Mungu kwa nini niliandamwa na matatizo katika maisha yangu, wakati nazungumza hivyo dada Stellah aliyenishawishi nitoe kisa changu gazetini ili jamii ijifunze, alinisikia na kuniambia nisiseme hivyo kwa sababu misukosuko katika maisha ni jambo la kawaida.

Nilimwambia sikatai lakini kwangu ilikuwa imezidi akaniambia niwe na amani ipo siku nitapona na kusahau yote yaliyonitokea na nitakuja kushangaa siku nitakayokutana na baba pamoja na ndugu zangu.
Msomaji mpendwa, kwa mujibu wa dada Stellah niliyekuwa nawasiliana naye, miezi michache baadaye Dorcas alipoteza kabisa uwezo wa kusikia, kitendo hicho kilimuumiza sana akawa hali vizuri hivyo kudhoofika kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele. Machi 31, 2016, usiku alipatwa na malaria kali akakimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya vipimo aligundulika kuwa na upungufu wa damu na maji mwilini kwa kiasi kikubwa, akalazwa.
Taarifa mbaya ya kuumiza niliyopewa na dada Stellah ni kwamba, mpendwa wetu Dorcas alifariki dunia Aprili 5 wakati madaktari wakipigania uhai wake ambapo msiba huo ulikuwa nyumbani kwake.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina. Kama una maoni, nipigie kwa namba hizo hapo juu.
MWISHO.

Leave a Comment