×

Penzi Kabla ya Kifo-25

ILIPOISHIA…
Umaskini umeondoka maishani mwake, bilionea Elizabeth amebadilisha maisha ya mpenzi wake, James. Maisha yanaendelea lakini upande wa pili, Elizabeth ana maumivu makubwa moyoni mwake kwa kuwa tu hana uwezo wa kushika mimba. Kitu kinachomjia kichwani mwake ni kumwambia mwanaume huyo amuoe, je nini kitaendelea?
SONGA NAYO…

Mbali na upendo aliokuwa akipewa, bado Elizabeth alikuwa na mawazo tele kuhusu mtoto, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya ili aweze kupata mtoto, hakuwa na furaha kabisa, kila alipokuwa, mawazo mengi yaliusumbua moyo wake.
Hakukuwa na kitu alichokitamani sana kwa kipindi hicho kama mtoto, hata kama alikuwa tajiri mkubwa ambapo alistahili kuitwa bilionea, alikuwa na jina kubwa lakini bado mtoto alionekana kuwa kila kitu katika maisha yake.
Hakutaka kumuweka wazi James kwa kuona kwamba angeharibu kila kitu, alibaki kimya huku akimuomba Mungu kila siku naye apate mtoto na hatimaye kunyonyesha kama wanawake wengine.
“James….” alimuita mpenzi wake.
“Naam!”
“Kuna kitu ninaomba tukifanye,” alisema Elizabeth.
“Kitu gani?”
“Ninahitaji unioe, ninahitaji uwe baba wa watoto wangu,” alisema Elizabeth, kwa mbali machozi yalianza kumlenga mara baada ya kukumbuka kwamba hana uwezo wa kupata mimba.
“Mbona unalia?” aliuliza James huku akimwangalia Elizabeth usoni.
“Inaniuma.”
“Inakuuma nini tena? Nitakuoa mpenzi.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Nakuahidi hilo, nitakuoa tu,” alisema James huku akijiapiza viapo vya kila aina kwamba angemuona Elizabeth.
Hakujua kile kilichokuwa kikimliza Elizabeth mahali hapo hakikuwa kuolewa kama alivyofikiria bali kile kilichomtoa machozi kilikuwa ni kutokupata mtoto. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia katika maisha hayo.

Hakuwahi kutoa mimba katika maisha yake, alipokwenda hospitali, madaktari hawakuona tatizo lolote lile, hakuwa mgumba, kitu kilichowashangaza wote ni kwa jinsi gani msichana huyo hakufanikiwa kushika mimba.
James alimbembeleza na kumbembeleza, hakupenda kumuona msichana huyo akilia, kwake, alijiona kuwa faraja kubwa katika maisha ya msichana huyo. Elizabeth alifarijika lakini bado moyo wake ulimuuma mno.

Kuna wakati alitamani kumwambia James ukweli kwamba asingeweza kupata mimba hata kidogo lakini kila alipotaka kufanya hivyo, alisita, hakuwa tayari kuweka wazi kwani kama angefanya hivyo basi ilikuwa ni lazima angemuacha kwa kuona kwamba hakukuwa na mwanaume aliyekuwa radhi kuwa na mke asiyekuwa na uwezo wa kuzaa.
“Inaniuma sana James…”
“Inakuuma nini tena jamaniii?”
“Basi tu, inaniuma mpenzi.”
“Niambie, usiogope, kipi kinakuuma?” aliuliza James.
“Glory, kwa nini Mungu ameamua kumtesa hivi?” aliuliza Elizabeth, alibadilisha kila kitu.
“Atapona tu, tufanye kile walichosema madaktari,” alisema James.
Jambo hilo halikuweza kubadilika moyoni mwake, alichukuana na James na kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kufurahia maisha tu, huko, walifanya mambo mengi huku waandishi wa habari wakiwa beneti kuwafuatilia.
Waliwatoa sana katika magazeti na mitandao, kila walipokuwa, kulikuwa na waandishi waliokuwa bize wakiwafuatilia kama ilivyokuwa kwa Kanye West na Kim Kardashian. Magazeti mengi yakawa yakiandika kuhusu wawili hao, kupitia mgongo wa Elizabeth, naye James aliendelea kuwa maarufu.

Wakati hayo yakiendelea, wakiyafaidi mapenzi ndipo jamaa mmoja akaibuka, huyu aliitwa Hamisi, kijana aliyekuwa mzuri wa sura ambaye alivuma sana kutokana na kazi ya mitindo aliyokuwa akiifanya.
Mwanaume huyu kipindi cha nyuma alifanikiwa kuwa mpenzi wa Elizabeth, alipeana naye mapenzi motomoto lakini pale ambapo msichana huyo alimhitaji kwa sana, yeye hakuwa na taarifa naye, hapo ndipo walipoachana.
Kipindi hicho Hamisi alikuwa ameibuka na lake, aliweka wazi kwamba alikuwa na picha za utupu za msichana huyo, aliwahi kumpiga wakati walipokuwa jijini Arusha. Watu wengi wakatamani kuziona picha hizo, marafiki wengi wakamsisitizia Hamisi aziachie ili kila mtu aone kile kilichokuwa ndani ya mwili wa Elizabeth.

Baada ya kuzuka kwa tetesi hizo, hapo ndipo maneno mengine yalipojengwa kwa kusema kwamba msichana huyo alikuwa malaya wa kutupwa. Yalikuwa ni maneno yenye uchungu sana ambapo mara baada ya Elizabeth kuyasikia, alihisi moyo wake ukiumia mno.
Huo wala haukuwa mwisho, maneno hayo yakaenda mbele na kusema kwamba msichana huyo hakuwa na uwezo wa kuzaa.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo hapahapa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment