×

Njia rahisi ya kupunguza unene zingatia haya-2

Leo naendelea kuelezea njia rahisi ya kupunguza unene, fuatana nami katika elimu hiyo.

PENDEKEZO LA 2
Ugali kwa samaki; mboga ya majani ya matango kwa nyanya. Usiweke chumvi kwenye mboga hiyo mbichi ya majani.

2-UNYWAJI MAJI
Waafrika hatunywi maji, hasa wanawake. Wanaokunywa maji zaidi ni wacheza michezo. Wengi wetu hunywa zaidi soda zilizojaa gesi inayoleta vidonda tumboni; na chai kuliko maji.
Na maji haya hutakiwa kunywa dakika 10-20 kabla ya chakula au nusu saa kuendelea baada ya chakula. Ukila chakula huku unashushia maji humaanisha mtu una kiu. Ulaji chakula na unywaji maji ni vitu viwili tofauti.
Ila utawaona watu wanakula huku wakibugia maji. Unapokula chakula huku unakunywa maji unapunguza nguvu za chakula, unajaza tumbo maji na kuchelewesha mmeng’enyo wa chakula (digestion). Chakula kisipomeng’enywa vizuri kinaketi tu tumboni.
Matokeo wengi wetu tuna matumbo makubwa. Kama hufanyi mazoezi lile tumbo linakwenda pembeni (chini ya mbavu) hasa kwa watu wa makamo linaleta maradhi kama kisukari, kiungulia, kuvimbiwa, uyabisi wa tumbo, n.k.

3-SUALA LA UMENG’ENYAJI
Chakula huanza kumeng’enywa au kusagwa (kwa lugha iliyozoeleka) mdomoni. Mate yako mdomoni ni chanzo cha uchambuaji chakula. Unapobugia chakula bila kutafuna sawasawa unasababisha mambo mawili. Moja chakula kutochambuliwa vizuri, pili chakula kwenda kukaa tu tumboni, au kama kikipita hakisaidii lolote mwilini.
Utafunaji wa taratibu husaidia umeng’enyaji. Chakula kinapofika tumboni hukaa pale dakika ishirini. Hapo huchanganywa na asidi (ya manjano iitwayo Hydrochloric) inayokibadilisha tayari kupelekwa katika utumbo mkubwa, kupitia kongosho.
Kule uchafu utapelekwa chini na rutuba kusafirishwa na utumbo mdogo kuelekea katika uwengu, moyo. Moyo utadunda chakula kilichoshageuzwa damu kuelekea mwilini kufanya kazi na akiba hubakishwa katika ini.
Sasa kama usipotafuna vizuri, ukila huku unakunywa sana maji au vinywaji vingine chakula hakimeng’enywi vizuri. Ndiyo maana unawaona watu wengine wanakula sana lakini hawana afya. Wanaugua hovyo, wanatoka jasho hovyo, wana matumbo makubwa, wanavimbiwa, wanakaa siku nyingi bila kwenda choo (inatakiwa mtu kwenda haja kubwa mara moja au mbili kwa siku) nk.

4-ULAJI WA VYAKULA VYA MAFUTA
Mafuta ni suala muhimu sana mwilini. Ila ulaji wake shurti uwe wa mpangilio. Yaani unaowiana.
Lazima mtu uwe na wastani mzuri wa vyakula vya nguvu, yaani “wanga” (ugali, ndizi, wali, viazi mbalimbali, mikate, mahindi, n.k), ujenzi yaani “protini” (mboga na nyama), “madini” (mbegumbegu mbichi si za kukaanga sana na chumvi) na “vitamini” (matunda, maziwa, mayai, nk).
Waafrika tunapenda nyama. Nyama ni muhimu sana maana ina madini aina ya chuma (nyama nyekundu) protini, nguvu na mafuta. Ila mafuta yaliyoko katika nyama mara nyingi si mazuri kwani hayatoki, huganda.
Chukua nyama ya kuku na samaki ambayo huwa na ngozi. Wengi wetu hupenda sana kula ile ngozi ya wanyama hawa kwa kuwa tamu. Lakini haya ni mafuta mabaya.
Mafuta ya samaki ni mazuri. Samaki anayo mafuta ya Omega-3 ambayo husaidia mwili na kinga dhidi ya maradhi mwilini.
Tunapokula nyama choma au ya kukaanga, lazima tule pia mboga za majani (mbichi) na si vizuri kula nyama kila siku. Kama huwezi kukaa bila kula nyama kila siku, fanya mazoezi ya mwi

PENDEKEZO LA 3
Kula mbegumbegu za korosho, karanga (ziwe mbichi badala ya kukaanga na chumvi) katikati ya siku. Haya ni mafuta yenye rutuba mwilini kuliko nyama za mafuta.
5-MAZOEZI YA MWILI NA VIUNGO
Mazoezi ni mfalme wa kupunguza unene. Ukiwauliza wengi watakuambia wanafanya kazi ngumu za sulubu (wanachuruzikwa jasho) kwa hiyo hayo ni mazoezi. Ila kazi na mazoezi ni vitu viwili tofauti. Ingekuwa kufanya kazi ni mazoezi basi kusingekuwa na wastani mfupi wa maisha kwa maskini hasa sisi Waafrika.

Wengine watadai kwamba walipokuwa wadogo shuleni walifanya mazoezi sasa wamekuwa watu wazima (miaka 40 kuendelea) kwamba eti mazoezi ni suala la ujana; kumbe kadiri unavyokuwa ki-umri ndivyo unavyotakiwa kufanya mazoezi na kujitazama zaidi kiafya.

Mazoezi ni shughuli inayokufanya kwanza uheme (mapafu na moyo kwenda kasi), viungo na mifupa kujinyoosha (stretching), kutoka jasho na usafishaji wa damu.

Mazoezi yanayosaidia haya ni pamoja na kutembea kasi, kukimbia, kuogelea, michezo mbalimbali ya riadha (kama mpira wa miguu, nyavu, kikapu, mikono, n.k); michezo ya kupigana na kujilinda (karate, kung fu, judo, capoeira, krav maga, jiu jitsu, systema, kickboxing, thai boxing, kempo, kalari payatu, aikido, nk.
Ni muhimu mwanadamu ufanye mazoezi makali ya viungo mara mbili tatu kwa juma. Si vizuri kufanya kila siku kwani misuli na mishipa inahitaji kupumzika na kukua.

Kama unapenda kuinua vyuma lazima uwe na mwalimu wa kukuelekeza; na si vizuri kufanya kila siku. Wastani wa mara mbili tatu kwa juma inatosha kabisa.

6-UPO UFANYAJI MAZOEZI WA AINA MBILI
Mazoezi ya nguvu ya kuhema niliyotaja hapo juu (cardio-vascular) na yale laini ya kujinyoosha yaani ambayo hutumia zaidi nguvu za ndani na pumzi. Haya ya pili ni kama Yoga (India), Tai Chi Chuan (China) na aina mpya mazoezi iliyoanza nchi za wenzetu miaka ya karibuni yaani Pilates (hutamkwa hivyo hivyo ilivyoandikwa Pilates). Haya laini yanawafaa zaidi watu wazima na nchini China na Japan mathalan utawakuta wazee wa miaka 80 hadi 90 bado wanayafanya. Husaidia moyo, damu na akili.

Michezo na mazoezi ya mwili ni njia kuu ya kupunguza unene, kurefusha maisha, kuchangamsha ubongo, kupunguza ulevi, uvutaji sigara, dawa za kulevya, tabia mbaya za uvivu, ugomvi, n.k. Mataifa yenye watu wanaofanya mazoezi kama Japan, Brazili, India na China huwa na wachapa kazi wengi na wananchi wanaoipenda jamii yao.
7-KULA SANA CHUMVI SI VIZURI
Ulaji chumvi mwingi hutokana na suala la ladha. Kisayansi vyakula vyote vina chumvi asilia sema tu tumezoea kuongezea madini hii iitwayo Sodium. Sodium inachangia sana kufupisha maisha.
Huifanya mishipa ya damu ichoke; ni kama bomba lolote la maji ukilitazama baadaye hugeuka rangi kutokana na yale maji kupita pale kila siku.

Kwa wale tunaoishi nchi za joto na kutoka sana jasho kula chumvi ni muhimu. Ila tatizo letu ni kwamba hatunywi maji ya kutosha. Mtu ukiwa na kiu unakunywa soda au kinywaji cha sukari; inakuwa kama unaendelea kuutesa mwili.
Kwa vipi? Mishipa inayopitisha damu mwilini badala ya kusaidiwa kwa maji inawekewa kazi zaidi ya kusafisha sukari na chumvi. Ndiyo maana vifo vingi vinatokea mapema; wastani wetu wa maisha haupiti miaka 50.

Utafiti uliofanywa chuo kikuu cha California, Marekani mwanzoni mwa 2010, umethitibisha kwamba vifo vingi duniani husababishwa na maradhi ya moyo na saratani ambavyo hutokana na uvutaji sigara, unene, ulevi na ulaji sana wa chumvi na sukari. Tukipunguza ulaji wa chumvi tunasaidia pia kupunguza maradhi ya moyo, utafiti unasema.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment