×

The Beginnig of My End (Mwanzo wa Mwisho wangu-11)

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.

Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani, anafaulu kwa kiwango cha juu na baada ya kuhitimu kidato sita, anaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Gladness aliendelea kumganda kama ruba huku mikono yake laini ikivinjari sehemu mbalimbali za mwili wake, Ben akawa anatoa miguno ya hapa na pale.
“Samahani kwa usumbufu, chakula chenu kipo tayari,” sauti ya mhudumu wa hoteli hiyo iliyokuwa ufukweni mwa bahari, ndiyo iliyowazindua wawili hao kutoka kwenye ulimwengu wa tofauti kabisa, harakaharaka wakaachiana huku kila mmoja akijihisi aibu kubwa kwani hawakujua ni kwa muda gani yule mhudumu alisimama pale.
“Haya ahsante tunakuja,” alisema Ben, mhudumu huyo akaondoka na kuwaacha bado wamekaa palepale.
“Ooh! Utanisamehe Ben kama nimekukwaza kwa hiki kilichotokea. Hata sielewi ilikuwaje.”
“Usijali Glad!” alisema Ben kwa kifupi huku akionesha kwamba hakuwa tayari kuendelea kujadiliana kuhusu suala hilo, akainuka na kumpa mkono msichana huyo mrembo, akamshika na kumuinua, taratibu wakaanza kutembea kuelekea kule walikoandaliwa chakula.
“Gladness! Sijawahi kuwa na hisia kama nilizonazo sasa juu yako, hata sielewi ni nini.”
“Umenikatisha tu muda ule Ben kabla sijamaliza kukwambia nilichotaka kukisema, ila kiukweli mimi pia sielewi nini kimetokea kwa sababusiyo kawaida yangu kupenda lakini kwa kifupi nimejikuta nikivutiwa na wewe, natamani uwe mchumba wangu na tukimaliza masomo tufunge ndoa na kuishi pamoja kama mume na mke!
“Sijawahi kuwa na ujasiri wa kumtamkia mtu yeyote maneno haya lakini kwako nimejikuta sina ujanja, tafadhali naomba unielewe,” alisema Gladness kwa sauti ya upole iliyoonesha kubeba ujumbe mzito.

“Naomba tule kwanza tutaendelea na mazungumzo tukishashiba,” alisema Ben huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akakata kipande cha mnofu na kumlisha Gladness ambaye naye aliachia tabasamu pana, wakaanza kula huku kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

“Unajua kwamba wewe ni mzuri sana Gladness! Natamani uje kunizalia watoto wazuri kama wewe,” alisema Ben, kauli iliyomfurahisha sana msichana huyo mrembo, akacheka kwa muda mrefu huku uzuri wake ukizidi kujidhihirisha.
Waliendelea kula huku wakipiga stori za hapa na pale mpaka walipomaliza. Wakarudi tena kule ufukweni walikokuwa wamekaa mwanzo ambapo safari hii Ben ndiye aliyeanzisha tena mazungumzo kuanzia pale walipokuwa wameishia. Ilikuwa siku ya furaha sana kwa Gladness kumsikia Ben akimsifia na kumwambia maneno ya kimapenzi kwani kwa muda mrefu alikuwa akiomba jambo hilo litokee.

“Sina namna ya kuielezea furaha niliyonayo ndani ya moyo wangu Ben, nakuahidi kwamba nitakupenda na kukulindia heshima yako siku zote za maisha yangu,” alisema Gladness huku machozi ya furaha yakimtoka, Ben akamsogeza kwenye kifua chake na kumkumbatia.
“Ukweli ni ni kwamba nilikupenda kuanzia siku ya kwanza nakuona na ndiyo maana sikuona hatari kukusemesha na kukuomba uwe rafiki yangu,” alisema Glad huku akimtazama Ben kwa macho yake mazuri, aibu za kikekike zikiwa zimetawala kwenye uso wake.

Japokuwa mara kwa mara Ben alikuwa akisita kuingia mzimamzima kwenye uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo, hasa alipokuwa akifikiria hali ya kifukara ya nyumbani kwao, mwisho aliamua liwalo na liwe. Huo ukawa mwanzo wa kufungua rasmi ukurasa mpya wa mapenzi!
Walikaa mpaka jioni hotelini hapo, wakipunga upepo wa bahari, kucheza na kufurahi pamoja huku mara kwa mara wakikumbatiana na kupigana mabusu, mambo ambayo yalikuwa mageni kabisa kwa Ben. Jioni walirejea chuoni huku kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.
Siku hiyo ilipita na wawili hao wakawa wameingia rasmi kwenye ulimwengu wa kimapenzi, huku wakipeana ahadi kemkemu juu ya maisha yao ya baadaye.

Japokuwa vijana wengi uwezo wao wa kitaaluma hushuka wanapoanza kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi, hali ilikuwa tofauti kwa Ben ambaye kwa sababu ya Gladness, alizidisha juhudi katika masomo maradufu, akiamini ni elimu pekee inayoweza kumtoa kwenye lindi la umaskini ili aishi vizuri na mwanamke huyo wa maisha yake.
Mapenzi kati yao yalizidi kunoga, ikafika mahali ikawa siyo siri tena, kila mtu chuoni hapo akawa anajua kwamba wawili hao wana uhusiano wa kimapenzi kwani halikuwa jambo la ajabu kuwakuta wakiwa wanatembea huku wameshikana mikono au kubusiana hadharani, mambo ambayo Ben hakuwahi kuyafanya awali kwa sababu hakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote tangu alipobalehe.

“Baby, wikiendi hii naomba nikupeleke nyumbani kwetu ukapajue na wazazi wangu wakujue,” alisema Gladness, kauli iliyomshtua sana Ben ndani ya moyo wake. Maisha ya kifukara aliyoishi kwa muda mrefu yalimfanya apoteze kabisa kujiamini. Japokuwa kimuonekano alikuwa amebadilika sana kutokana na juhudi kubwa za Gladness kumnunulia nguo nzuri na viatu, bado mwenyewe alikuwa hajiamini hata kidogo.

“Wazazi wako wakiniona si watakukataza kuendelea kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi?”
“Usiwe na wasiwasi kuhusu hilo Ben, mambo yote niachie mimi na huna haja ya kuogopa chochote,” alisema msichana huyo kwa kujiamini, akamkumbatia Ben na kumbusu kwenye paji la uso wake.

Siku ziliendelea kusonga mbele huku wawili hao wakizidisha juhudi kwenye masomo yao kwani kitendo cha muda mwingi kushinda akiwa na Ben kilimfanya Gladness na yeye awe na juhudi kubwa kwenye masomo.
Hatimaye mwisho wa wiki uliwadia, kama walivyokuwa wamekubaliana, wawili hao walijiandaa, Ben akavaa shati zuri na suruali aliyonunuliwa na msichana huyo, akapendeza kuliko siku nyingine zote. Wakatoka na kukodi teksi iliyowapeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwa wazazi wa msichana huyo.

“Hapa ndiyo nyumbani kwetu, jisikie upo nyumbani mume wangu mtarajiwa,” alisema Gladness baada ya teksi waliyopanda kuwafikisha mbele ya jumba moja la kifahari lenye ghorofa mbili, geti kubwa lililokuwa likifunguliwa kwa mitambo maalum lilifunguka baada ya Gladness kubonyeza kitufe maalum ukutani, wakapokelewa na mlinzi aliyekuwa amevalia sare maalum, mkononi akiwa na bunduki.

“Ooh! Karibu Gladness, pole na masomo,” alisema askari huyo huku akimpokea msichana huyo mkoba wake mdogo aliokuwa amebeba, akawaongoza kuelekea ndani. Ben ambaye alikuwa nyuma, alibaki amepigwa na butwaa, akiwa haamini kama hapo ndiyo nyumbani kwa msichana huyo.

Kila kitu kilikuwa katika ubora wa hali ya juu, kuanzia nyumba yenyewe, mandhari ya kuzunguka nyumba hiyo mpaka magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye maegesho ndani ya nyumba hiyo, akabaki amepigwa na butwaa. Alijaribu kufananisha na maisha aliyokulia, akajikuta akizidi kukosa kujiamini.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment