×

Sitalipa Kisasi- 02

ILIPOISHIA:
Antony na Matlida ni ndugu waliopoteana wakiwa watoto wadogo. Wanakutana ukubwani na kuanzisha uhusiano wa mapenzi bila kufahamiana lakini baadaye wanajikuta katika maisha magumu yenye changamoto kuliko kawaida kisa uhusiano wao huo.
Antony akiwa katika makazi yao kwenye bonde la wachimba kokoto, Wazo, Madale ndani ya kijumba walichojenga kwa magunia na makuti, alfajiri hiyo alikumbuka akiwa mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania aliundiwa kesi za mauaji mfululizo na msichana mwenye roho mbaya Adelina baada ya kukataa kuanzisha naye uhusiano wa mapenzi. Kesi hizo ndizo zilizomfanya kijana huyo kuuza mali zake zote alizokuwa nazo ili kujinusuru na kifungo.
TAMBAA NAYO…

HATA hivyo mbali na Antony kuuza mali zake zote, pesa zilizopatikana hazikuweza kutosha kumnusuru kwenye kesi hiyo iliyokuwa na mlolongo mrefu, hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya Matlida pia kuuza za kwake ili tu kumuokoa mwanaume aliyempenda kuliko kawaida duniani. Japo alifanikiwa, ukweli ni kwamba kesi hiyo iliwaachia kovu kubwa la umaskini.

Siku ambayo Hakimu Benson Bulya alitangaza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Menalia kuwa Antony alikuwa huru baada ya kuonekana hana hatia kwenye madai ya kuua, Adelina aliahidi mbele ya watu wote waliofurika mahakamani hapo kusikiliza shauri hilo kuwa huo haukuwa mwisho wa mapambano yake na wawili hao.

Aliwaambia “Nitahakikisha mnatengana kwa njia yoyote ile, hata kama itagharimu uhai wangu.” Hivyo ndivyo ilivyotokea, Adelina aliwaandama mno Antony na Matlida kwa misukosuko ya kutisha.

Akiwa bado amemkumbatia Matlida huku machozi mengi yakimbubujika yaliyomlowanisha msichana huyo, Antony aliendelea kukumbuka mambo mengi yaliyowatokea kwenye maisha yao kikiwemo kisa cha wao kupoteana wakiwa wadogo jambo lililotengeneza mkasa mwingine kwenye historia yao hiyo yenye machungu tele!
Ilikuwa ni Jumamosi, Aprili 10, mwaka 1982 usiku wa manane ambapo mvua kubwa ilikuwa inanyesha katika anga lote la Kijiji cha Makata, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Hiyo haikuwa mvua ya kawaida kama zilizozoeleka kunyesha, kila mwananchi alitawaliwa na hofu juu ya maafa yaliyokuwa yanatokea maana mvua hiyo iliambatana na radi, ngurumo, upepo mkali na ilikuwa inadondosha mawe makubwa ya barafu, hali ilikuwa inatisha!
“Bibi naogopa,” Antony aliyekuwa na miaka tisa wakati huo alimwambia bibi yake Tekela aliyekuwa amewakumbatia pamoja na mdogo wake Matlida mwenye miaka mitano pembeni ya ukuta.
“Usiogope, Mungu atatusaidia tutasalimika.”
“Hatuwezi bibi mvua haiishi!”
“Itaisha tu! Tuendelee kumuamini Mungu”
“Isipoisha tutakufa?” Matlida naye aliuliza.
“Hatuwezi kufa wajukuu zangu.”
Hali halisi ilikuwa inaogopesha. Hadi yanafika majira ya saa nane za usiku, zilikuwa zimekatika saa tatu tangu mvua iliyoanza kimchezomchezo kunyesha hatimaye kuwa mvua kubwa iliyomtisha kila mmoja.

Nyumba nyingi zilikuwa zinaporomoka na kuezuliwa, mifugo iliteketea kwa kusombwa na maji, mazao yaliharibiwa vibaya, pia watu wengi walikuwa wanakufa kwa kuangukiwa na nyumba zao, katika majira hayo mvua iliyodondosha mawe makubwa ya barafu iliendelea kuchachamaa ikiambatana na upepo mkali.

Puu! Mara kilisikika kishindo kikubwa juu ya paa la nyumba ya bibi Tekela, yalikuwa ni mawe makubwa mawili ya barafu yaliyotua na kutoboa bati kisha yakashuka ndani.

“Mungu wangu!” Bibi Tekela alihamaki. “Tutokeni nje haraka,” alisema huku akiwainua wajukuu zake.
Walitoka na kuanza kukimbia ovyo pamoja na wananchi wengi waliokuwa wanakimbia katika mvua hiyo ambapo watu wengi waliendelea kufa, kujeruhiwa na kusombwa na mafuriko.

Maskini Bibi Tekela! Akiwa anaendelea kukimbia, alishtukia jiwe kubwa la barafu likitua kichwani kwake Tiii! Hakutoa hata sauti kikongwe huyo mwenye miaka 59, alidondoka chini kama mzigo na kunyooka.
“Bibiii!” Antony aliita na kukimbilia alipodondokea.

Alikuwa anatokwa damu nyingi puani mdomoni masikioni na hata kwenye jeraha alilopondwa na jiwe hilo la barafu.
“Antony baba, jitahidi kumtunza mdogo wako!” Hayo ndiyo maneno pekee aliyomudu kuyatamka bibi Tekela kabla ya kukata roho.
Antony alilia sana, kwake na Matlida bibi huyo alikuwa ni mtu muhimu mno, kufa kwake lilikuwa ni pigo kubwa baada ya siku chache tu nyuma kupoteza wazazi wao kwa ajali ya gari, aliendelea kulia huku akiwa amemkumbatia asijue la kufanya.

Hayo yote Antony aliyakumbuka huku machozi yakimbubujika, Matlida alikuwa amelala kifuani kwake wakiwa ndani ya kijumba chao cha magunia na miti katika eneo hilo la machimbo ya kokoto, Wazo, Madale.
“Pole, jikaze, amka twende, kwa kukaa hapa utakufa,” Antony alikumbuka pia jinsi alivyokutana na Thomas. Kijana aliyetokea kumfariji wakati akimlilia bibi yake.
Anakumbuka aliuinua uso wake taratibu na kutazama, macho yake yakagongana na macho ya kijana huyo aliyejitambulisha kwake kuwa ni Thomas.
Je, nini kiliendelea? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

1 Comment

Leave a Comment