
Stori: Francis Godwin, UWAZI
IRINGA: MKAZI wa Kidamali, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, Joseph Balami (pichani) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumua Stani Singaile (42) Oktoba 15, mwaka 2011kijijini hapo kwa kumchoma kisu kusudi wakati wa ugomvi uliotokea kwenye klabu cha pombe za kienyeji.
Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri ambao ulidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 15, mwaka 2011 katika Kijiji cha Kidamali.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mary Shangali alisema amekubaliana na upande wa mashtaka na ushahidi uliotolewa mahakamani ulidhihirisha pasipo shaka kuwa mtuhumuwa alitenda kosa hilo.
“Katika kesi hii upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano na upande wa utetezi ulileta mashahidi wawili ambao ni mtuhumiwa mwenyewe na mke wake, mahakama imekubaliana na upande wa mashtaka kuwa mtuhumuwa ametenda kosa na imemtia hatiani kwa kosa la kuua kwa makusudi,” alisema Jaji Shangali na kuongeza:
“Kwa kuwa adhabu inayotolewa kwa kosa hilo ni moja kwa mujibu wa sheria…,ninakuhukumu kunyongwa hadi kufa,” alisema jaji huyo.
Alisema kulingana na mashuhuda waliotoa ushahidi mahakamani, wamethibitisha bila kuacha shaka kuwa siku hiyo mtuhumiwa alikwenda kwenye kilabu kile na kumfuata marehemu kisha kumchoma kisu kifuani hali inayoonesha alidhamiria kuua.