×

Dunia uliyoiacha nyuma yako – 62

Ufisadi mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, ukiwahusisha viongozi wakuu wa nchi, unamsababishia matatizo makubwa waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa. Inatengenezwa ajali ambayo kama isingekuwa msaada mkubwa wa jasusi wa kimataifa, Grace, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yake.

Anaokolewa kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu na kuwafanya watu wote waamini kwamba amekufa. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa kuna ushahidi unaoonesha kwamba mheshimiwa waziri mkuu alikuwa akihusika kuanzia kwenye ufisadi mpaka kwenye kupanga njama za vifo vya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mwampashi pamoja na Waziri wa Fedha, Abbas Magesa.

Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinakuwa ngumu kutokana na hila anazozifanya na sasa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba aliyekuwa akiongoza uchunguzi wa sakata hilo, anabambikwa kesi ya mauaji na kukamatwa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kitendo cha kukamatwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba kilichokuwa kimegubikwa na utata wa hali ya juu, kilionesha kumfurahisha mno mheshimiwa waziri mkuu, Bandundu Musyoka ‘BM’, akawa na matumaini makubwa kwamba hakuna anayeweza kujifanya kimbelembele wa kumfuatilia kama ilivyokuwa kwa Mandiba.

Kutokana na wadhifa wake mkubwa serikali, akiwa ndiyo mtendaji mkuu wa serikali, maafisa wa ngazi za juu wa usalama waliokuwa wakishirikiana na Mandiba; Pius Kasekwa, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi, walijikuta wakiingiwa na hofu kubwa ndani ya mioyo yao.

Kwa kilichotokea kwa Mandiba, kila mmoja alikuwa akiishi roho mkononi kwa sababu kama isingekuwa ushupavu wake, Mandiba alitakiwa kufa katika tukio lililoandaliwa kwa ustadi mkubwa nje ya nyumba yake. Hata kitendo cha kukamatwa na kupelekwa mahabusu, pia kilimaanisha kwamba usalama wake ulikuwa hatarini na chochote kingeweza kutokea muda wowote.

“Grace si alituhakikishia kwamba atatusaidia? Mbona sasa yuko kimya? Nahisi kifo kimekaribia, muda mwingine natamani hata kutorokea nje ya nchi,” Kasekwa na Ngai walikuwa wakijadiliana, wakiwa kwenye chumba cha siri Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, muda mfupi baada ya Mandiba kukamatwa.

“Nimeanza kuamini alichokisema Mandiba kwamba lazima kuna mtu ambaye yupo karibu kabisa na sisi ndiye anayetoa siri za tunachotaka kukifanya ndiyo maana tunakwama,” alisema Ngai, wazo lililoungwa mkono na mwenzake.
“Sasa tutafanyaje?”
“Hata sielewi, nahisi mwili wangu wote unaishiwa nguvu, sijawahi kukutana na wakati mgumu kiasi hiki tangu nianze kazi miaka thelathini iliyopita.”
*   *   *
“Kuna tatizo kubwa limetokea huko nyumbani.”
“Tatizo gani tena?”
“Waziri Mkuu Bandundu Musyoka anaelekea kuwazidi ujanja Mandiba na wenzake.”
“Kwa nini na wewe umejuaje?”
“Huna haja ya kuhoji sana Magesa, Mandiba amenipigia simu akionesha kuwa kwenye matatizo makubwa, inabidi niondoke sasa hivi kuelekea Tanzania.”
“Mungu wangu, sasa na mimi itakuwaje?”
“Wewe kaa hapahapa wala usihofu ila usitoke kwenda sehemu yoyote mpaka nitakaporudi, kazi ndogo sana hiyo. Nimeshawahi kukutana na kazi ngumu lakini zote nilifanikiwa, siwezi kushindwa kwenye hili.”
“Lakini si na wewe inafahamika kwamba ulikufa?”
“Hilo siyo tatizo Magesa, nilishaahidi kukusaidia kuanzia mwanzo kwa hiyo ni lazima nitimize nilichokianzisha.”
“Naomba ukifika unipelekee salamu kwa wanangu, waambie nawapenda sana na sijafa, ipo siku tutakuja kuonana nao.”
“Hilo suala haliwezekani kwa sasa Magesa, wanatakiwa waendelee kufahamu kwamba umekufa isipokuwa mtu mmoja tu inabidi aufahamu ukweli.”
“Nani?”
“Mkeo Vivian! Ni lazima afahamu hila za Musyoka na amini usiamini yeye ndiye anayeweza kutusaidia kumuangusha.”
“Hapana! Sitaki hata kumsikia, huyo mwanamke ni shetani sana, sitaki hata kumsikia,” alisema Magesa huku machozi yakianza kumtoka. Ni kama Grace alikuwa ametonesha donda ambalo halijapona kwenye mtima wake lakini bado aliendelea kusisitiza kwamba ni lazima aambiwe ukweli.

Mpaka Grace anaondoka kwa safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, bado hawakuwa wamefikia muafaka kama Vivian aambiwe ukweli kwamba Magesa hakuwa amekufa au la!
Alichoendelea kusisitiza mwanamke huyo ni kwamba kama Magesa anataka kuisaidia nchi yake na wote wanaonyanyaswa na kundi la mafisadi wachache wanaofaidi utajiri wa nchi, ilikuwa ni lazima akubali kumsamehe mkewe na kuweka pembeni tofauti zao kisha washirikiane kumuangusha Mheshimiwa Musyoka. Magesa hakuwa tayari kabisa kwa suala hilo.

Grace aliondoka na kuelekea mpaka uwanja wa ndege ambapo japokuwa hakuwa amekata tiketi mapema, alipoonesha kitambulisho chake na kueleza kwamba alikuwa kwenye kazi muhimu, alipewa nafasi kwenye Ndege ya Shirika la Comoro Airways na muda mfupi baadaye, alikuwa ndani ya ndege kubwa ya Airbus 380A kwa safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.

Kwa jinsi alivyokuwa amevaa, isingekuwa rahisi kuhisi kwamba Grace alikuwa mtu mzito kiasi hicho. Kwa makusudi kabisa, alivaa kaptura fupi iliyoyabana mapaja yake makubwa, juu akavaa fulana ya kisasa kofia kama wafanyavyo wanawake wengi wa kisasa, akavaa na miwani ya rangi nyeusi ambayo ilimfanya isiwe rahisi kwa mtu yeyote kumtambua.
Baada ya kusafiri kwa saa kadhaa, hatimaye sauti ya mhudumu ndani ya ndege hiyo, ilisikika ikiwataarifu abiria wote kufunga mikanda na kuzima vifaa vyote vya kielektroniki wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Muda mfupi baadaye, ndege ilianza kuinama upande wa mbele na kuanza kushuka chini kwa kasi, hatimaye ikatingishika kidogo kuonesha kwamba ilishagusa ardhi ya Tanzania, ikakimbia na dakika kadhaa baadaye, tayari ilishasimama mbele ya jengo kubwa la uwanja huo wa ndege.

Abiria wakaanza kuteremka, Grace akiwa miongoni mwao. Baada ya kukamilisha taratibu zote uwanjani hapo, Grace alibeba begi lake la ukubwa wa wastani na kutoka hadi kwenye maegesho ya teksi, akakodi teksi moja na kumuelekeza sehemu ya kumpeleka.
*   *   *
Baada ya kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jordan Ngai aliamua kwenda kujiliwaza kwenye Hoteli ya Coral Cliff kwani alihisi kichwa chake kimeelemewa na mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea kwenye sakata la Magesa.

Kwa kawaida, anapokuwa na msongo wa mawazo, Ngai alikuwa akipenda kuogelea na kuendesha boti maalum za kwenye maji zinazofanana na pikipiki, akapanga kwamba siku hiyo akifika kwenye hoteli hiyo, atakula, kunywa na kisha kuelekea baharini mpaka jioni kabisa ndiyo arudi nyumbani kwake.

Hakumuaga mtu yeyote, hata mkewe hakuwa akijua yupo wapi zaidi ya kuamini kwamba anaendelea na shughuli zake za kikazi kama kawaida.

Akiwa anaendesha gari lake kwa mwendo wa wastani, alishtuka kuona gari dogo jeusi likija kwa kasi kubwa nyuma yake huku dereva akipiga honi na kuwasha taa na kuzizima kama anayemhimiza aongeze kasi. Kutokana na jinsi alivyokuwa na msongo wa mawazo, Ngai hakutaka kufanya kama yule dereva wa gari lililokuwa nyuma yake alivyokuwa anataka kwani alihisi anaweza kusababisha ajali.

Alichokifanya, aliwasha ‘indiketa’ ya upande wa kushoto akimpa ishara yule dereva apite na kuendelea na safari zake, akalisogeza gari lake mpaka pembeni kabisa ya barabara na kusimama lakini tofauti na alivyotegemea, gari lile halikupita na badala yake nalo likasimama nyuma yake.

Mwanaume mwenye mwili mkubwa akashuka na kuanza kulisogelea gari hilo, Ngai aliyekuwa amepigwa na butwaa, alimuona mwanaume huyo akija kupitia vioo vya pembeni (side mirrors), akawa anajiuliza maswali yaliyokosa majibu.

Alichokifanya, aliingiza mkono kwenye dashboard ya gari lake na kutoa bastola, harakaharaka akaikoki na kuiweka tayari kwa chochote, akatulia nyuma ya usukani. Ghafla alisikia kioo cha upande wake kikigongwa kwa nguvu, alipogeuka kumtazama aliyekuwa anagonga, aligundua kuwa ni yule mwanaume aliyetoka kwenye gari la nyuma yake akimtaka ashushe kioo, akashusha.

“We mzee kwa nini unaendesha gari kama unajifunza? Yaani unatuchelewesha kwenye mambo yetu kwa sababu ya uzembe wako, una akili timamu wewe?” alisema mwanaume huyo kwa ukali huku akimsukuma Ngai na kidole kichwani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

 

Leave a Comment