Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.
Wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha. Maandalizi ya harusi yanazidi kupamba moto.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
“Uko tayari kuishi na wanangu na kuwaonesha mapenzi kama waliyokuwa wakioneshwa na mama yao nitakapokuoa?” Msuya alimuuliza Arianna lakini badala ya kumjibu, msichana huyo alimkumbatia Msuya kimahaba na kumbana kwenye kifua chake, wakawa wanatazamana kimahaba.
“Nimekupenda wewe Msuya, kwa nini nisiwapende na wanao? Nitawatunza na kuwajali pengine kuliko hata mama yao alivyokuwa anafanya,” alisema Arianna, kauli iliyoamsha furaha ya ajabu ndani ya moyo wa Msuya, wakagusanisha ndimi zao na kuanza kuelea kwenye ulimwengu tofauti.
“Basi nashukuru sana kusikia hivyo, nilitaka kukwambia jambo hilo, nashukuru sana Arianna,” alisema Msuya na kumbusu tena Arianna kwenye paji la uso.
“Na wewe hakuna jambo lolote unalotaka kuniambia kabla hatujaingia kwenye ndoa?” Msuya alimuuliza Arianna huku akimtazama usoni, msichana huyo akashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, macho yao yakagongana.
“Sina chochote cha kukwambia Msuya zaidi ya kusema nakupenda sana,” alisema Arianna, wakakumbatiana tena kimahaba.
Siku hiyo ilipita, kesho yake maandalizi yakazidi kupamba moto huku ndoa ya wawili hao ikizidi kuwa gumzo ndani ya jiji lote la Arusha. Hakuna mtu aliyepelekewa kadi ya mchango wa harusi kama zilivyo harusi nyingi za Kitanzania, kwa kuwa fedha haikuwa tatizo kwake, Msuya aligharamia kila kitu yeye mwenyewe.
Kadi zilizotolewa zilikuwa za mialiko tu ambazo nazo zilitolewa kwa watu maalum pekee, wakiwemo wafanyabiashara wenzake, viongozi wa kiserikali na watu maarufu. Siku zikawa zinasonga mbele huku kila mmoja akisubiri kwa shauku kubwa harusi hiyo.
Hatimaye ile siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa, iliwadia ambapo Arianna na Msuya, walipanda madhabahuni na kufunga ndoa rasmi ya Kikristo katika tukio lililovuta hisia za wakazi wengi wa Jiji la Arusha.
Baada ya kufunga ndoa hiyo kanisani, ilifuatiwa na sherehe kubwa ambayo ilienda kufanyika kwenye hoteli kubwa iliyokuwa ndani ya mbuga za wanyama za Serengeti, wageni waalikwa wapatao mia mbili wakajumuika pamoja katika sherehe hiyo iliyoweka historia ya kipekee jijini humo.
“Siamini Msuya, siamini kama kweli umetimiza ahadi yako.”
“Nakupenda Arianna, nilikuahidi na ilikuwa ni lazima nitimize ahadi yangu,” alisema Msuya na kumkumbatia Arianna ambaye machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka na kulowanisha uso wake.
Sherehe iliendelea kupamba moto, watu wakala, kunywa na kusaza sambamba na kucheza muziki mzuri mpaka usiku wa manane ambapo usafiri maalum ulitumika kuwarudisha wageni wote makwao.
Baada ya watu wote kuondoka, Msuya na mkewe walibaki hotelini hapo kwa sababu walipanga kulala hapo mpaka kesho yake asubuhi ambapo wangeianza safari ya kwenda kula fungate (honeymoon) kwenye Visiwa vya Hawaii kama walivyokubaliana.
“Kesho tunasafiri kama tulivyokubaliana.”
“Sijawahi kupanda ndege tangu nipate akili zangu timamu, naona nitaota,” alisema Arianna na kusababisha wote wacheke kwa furaha. Kesho yake asubuhi, wawili hao waliondoka hotelini kwa kutumia usafiri maalum na kusindikizwa na wapambe wao mpaka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) ambako walisafiri kwa ndege ndogo mpaka jijini Nairobi.
Baada ya kuwasili Nairobi, hakukuwa na muda wa kupoteza, wakaunganisha na ndege nyingine kubwa, mali ya Shirika la Fly Emirates na safari ya kuelekea Hawaii ikaanza. Kwa kuwa Msuya alikata tiketi za daraja la kwanza, kutokana na uchovu waliokuwa nao, wawili hao walitumia muda mwingi wa safari kulala.
Sauti ya mhudumu wa ndege iliyokuwa inasikika kutoka kwenye vipaza sauti vilivyokuwa ndani ya ndege hiyo, ndiyo iliyowashtua wawili hao baada ya mhudumu kutangaza kwamba walikuwa wakikaribia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Honolulu, kwenye Visiwa vya Hawaii.
“Tumefika mpenzi wangu,” alisema Msuya huku akimbusu Arianna kwenye paji la uso, wote wakakaa vizuri na kufunga mikanda, ndege ikainama upande wa mbele na kuanza kushuka chini, hatimaye ikatua salama kwenye uwanja huo wenye hadhi ya kipekee.
Kwa kuwa tayari Msuya alishaandaa mipango yote, walipofika uwanjani hapo waliwakuta wahudumu wa hoteli kubwa ya Hilton Worldwide wakiwa wanawasubiri, wakawapokea kwa uchangamfu na kuwapeleka mpaka kwenye gari maalum la hoteli hiyo. Safari ya kuelekea kwenye hoteli hiyo iliyokuwa ufukweni mwa bahari ikaanza.
“Whaoo! Huku kuzuri sana, sijawahi kuona sehemu nzuri kama hii,” alisema Arianna huku akichungulia nje kupitia dirisha la gari lililowabeba, mandhari ya visiwa hivyo yalikuwa mazuri mno kiasi cha kumfanya Arianna ashindwe kuzificha hisia zake.
Hatimaye waliwasili kwenye hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano, wakapokelewa kwa uchangamfu na wahudumu wengi wakarimu na kupelekwa moja kwa moja mpaka kwenye vyumba vilivyotengwa kwa ajili yao.
“Ahsante kwa kunipenda Msuya, hata sijui nitakulipa nini.”
“Usijali Arianna, kukupenda ni jukumu langu na naahidi kukutunza kama mboni ya jicho langu,” alisema Msuya, wakiwa ndani ya chumba kizuri cha hoteli, kilichokuwa kimepambwa maalum kwa ajili ya maharusi hao, Arianna na Msuya wakakumbatiana kwa hisia nzito huku msichana huyo akiendelea kutokwa na machozi ya furaha.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.