Asalaam aleykhum!
Leo shoga yangu nataka kuzungumza na wenzetu ambao utulivu kwao ni ziro yaani ambao licha ya kwamba wapo kwenye ndoa hawajiheshimu hivyo kutoka na wanaume wengine bila hofu.
Shoga yangu mwenye tabia hiyo usipojirekebisha utaondoka kwa Ukimwi ambao hivi sasa mjini unaitwa degedege la ukubwani; natumai utakuwa umewasikia watu wakisema f’lani kafa kwa degedege la ukubwani.
Kama bado hujasikia, basi habari ndiyo hiyo ukisikia watu wanasema kafa kwa degedege la ukubwani ujue kishaondoka kwa Ukimwi ambao umebatizwa majina kibao kama ngoma, umeme, miwaya, ugonjwa wa kisasa, moto nk.
Ingawa safu yetu hii ni maalum kwa mada za mashamshamu ya mapenzi, nimeona niuzungumzie Ukimwi a.k.a degedege la ukubwani kwa sababu chanzo chake ni hayo mashamshamu ya malovee.
Shoga uliyeolewa tena na mwanaume mwenye nguvu zake ambaye mkiwa eneo lenu la kujidai anakukata vilivyo kiu yako na kukuacha umechoka kiasi cha kushindwa hata kufanya kazi zingine, kwa nini unachepuka?
Huko nje unatafuta nini kama siyo degedege la ukubwani? Kama ni fedha si ridhika na kipato cha mumeo aliyekupenda kwa dhati na kukutoa kwa wazazi wako kwa heshima na kuamua kuishi nawe.
Hivi hujui degedege la ukubwani ni maradhi ya aibu yanayowatesa watu na kuwafilisi achilia mbali kuwaacha watoto wenu yatima, kisa ni wewe kutotulia na mumeo nyumbani?
Shoga yangu mwenye tabia hiyo hebu jirekebishe na tulia na mumeo, kama amekumbwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume msaidie kupata tiba na si kuchepuka. Bye!